Tuesday, 3 September 2013

Serikali ikomeshe umiliki holela wa silaha

 
Posted  Jumatatu,Septemba2  2013  saa 21:31 PM
Kwa ufupi
Ndio sababu matumizi ya bastola katika vitendo vya uhalifu katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha Manyara na mikoa inayopakana na nchi za Maziwa Makuu yamekuwa yakiongezeka.


Mwishoni mwa wiki tulichapisha habari za uchunguzi kuhusu jinsi tatizo la rushwa katika baadhi ya vyombo vya dola linavyowezesha watu wasio na sifa kumiliki silaha ndogondogo, hasa bastola. Uchunguzi huo wa muda mrefu katika mikoa mbalimbali hapa nchini, ikiwamo iliyo mipakani umeonyesha kwamba bastola zinamilikiwa na watu pasipo kufuata taratibu na kwamba nyingi zinatumika katika vitendo vya uhalifu.
Uchunguzi huo umebaini pasipo kuacha shaka kwamba kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu wa kutumia silaha pia ni matokeo ya udhaifu wa Jeshi la Polisi nchini katika kusimamia utekelezaji wa sheria husika. Katika uchunguzi huo, imebainika kwamba hivi sasa hata vibaka ambao awali walikuwa wakitumia visu, nondo na mbao za misumari kupora watu, sasa wanatumia bastola kufanya uhalifu huo.
Kama uchunguzi huo ulivyobainisha, tatizo la kuzagaa kwa bastola ni kubwa na haliko mijini pekee, bali pia vijijini. Wahamiaji haramu katika mikoa inayopakana na Rwanda, Burundi, Uganda na DR Kongo wamethibitika kuingiza nchini silaha za kila aina na kuziuza kwa bei ndogo kwa watu wanaozitumia kufanya vitendo vya uhalifu.
Uchunguzi umeonyesha kwamba moja ya njia ambazo zimekuwa zikitumika kuwapa silaha watu wasiokuwa na sifa ni kutumia mawakala au baadhi ya maofisa wa polisi kuwatafutia vibali vya kumiliki silaha.
Taratibu za kuomba kumiliki silaha zinajulikana lakini zinapindishwa kutokana na udhaifu uliomo katika sheria husika. Waombaji wanatakiwa kujadiliwa na kuhojiwa na kamati za ulinzi na usalama za vijiji, wilaya na mikoa na kujiridhisha kama mwombaji anazo sifa za kumiliki silaha, kwa maana ya kutokuwa na rekodi yoyote ya uhalifu. Hata hivyo, uchunguzi umegundua kwamba katika mikoa mingi baadhi ya wafanyabiashara, wakiwamo vijana wadogo wana vibali vya kumiliki bastola, ingawa hawakupitia katika mchakato huo.
Ndio sababu matumizi ya bastola katika vitendo vya uhalifu katika mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro, Arusha Manyara na mikoa inayopakana na nchi za Maziwa Makuu yamekuwa yakiongezeka. Vibali vya kumiliki silaha vinapatikana kirahisi kutoka kwa baadhi ya maofisa wa Jeshi la Polisi, Makao Makuu na baadhi ya wale waliopo mikoani kwa Sh1.5 milioni, vyanzo vyetu vya habari vilisema kwa sharti la kutotajwa majina gazetini kutokana na kuhofia usalama wao. Vyanzo hivyo pia vinasema hali hiyo ndio chimbuko la ufyatuaji ovyo wa risasi katika maeneo mengi ya starehe mijini na sehemu zinazozunguka migodi.
Ulegevu na udhaifu wa dola katika kudhibiti matumizi na umiliki holela wa silaha umetoa mwanya kwa baadhi ya wamiliki kukodisha silaha zao na kurudishiwa silaha hizo mara baada ya kuzitumia katika uhalifu. Baadhi ya watu waliohojiwa kuhusu sababu za watu kumiliki silaha kwa kutumia njia za mkato wanapinga dhana kwamba ukiritimba katika upatikanaji wa silaha ndio sababu ya kuwapo hali hiyo.
Wananchi wengi wanaamini kwamba iwapo Serikali itaendesha operesheni iliyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete ya kuwarudisha makwao wahamiaji haramu, upatikanaji wa silaha kirahisi utapungua kwa kiasi kikubwa.
Serikali sasa inapaswa kutafuta mbinu na mikakati ya kuendesha misako ili kukamata silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria. Hii ni pamoja na kuweka udhibiti wa kutosha ili watu wasimilikishwe silaha bila kuwa na sifa.

Source:Mwananchi