Kwa ufupi
Fedha zinazodaiwa kufichwa na baadhi ya vigogo wa Serikali ya Tanzania.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za
Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amesema Bunge litaunda kamati ya kufuatilia
vigogo walioficha mabilioni ya fedha nchini Uswisi, kama Serikali
ikishindwa kuwasilisha taarifa ya uchunguzi wake katika mkutano wa Bunge
unaoendelea mjini Dodoma.
Wakati Zitto akisema hayo, Mbunge na mjumbe wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali, PAC kutoka Sudan Kusini, Goc
Mukleac Mayol, alirusha makombora kwa wahisani na nchi zilizoendelea,
akiwatuhumu kuwafundisha Waafrika tabia ya wizi na ufisadi wa fedha na
rasilimali za umma.
Kabwe ambaye yuko mjini Arusha kuhudhuria mkutano
wa wabunge wa Kamati ya Hesabu za Serikali katika nchi za Kusini mwa
Afrika (Sadcocap), alisema kwa mujibu wa maazimio ya Bunge, Serikali
inapaswa kuwasilisha taarifa yake katika mkutano wa sasa.
“Awali taarifa ilikuwa iwasilishwe katika mkutano
wa Bunge la mwezi wa nne, ikasogezwa mbele hadi Bunge la Bajeti, lakini
wakaomba taarifa iwasilishwe katika Bunge hili. Hata hivyo kwenye ratiba
ya vikao vya Bunge linaloendelea, taarifa ya Serikali kuhusu walioficha
fedha Uswisi haipo,” alisema mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini.
Alisema hata hivyo, anaamini taarifa hiyo
itawasilishwa bungeni kwa kuzingatia kuwa uchunguzi unakwenda vizuri na
kwamba imebainika kuwa fedha za aina hiyo, zimefichwa pia katika benki
za Dubai na Mauritius.
“Binafsi nimekutana nao wachunguzi, wamefanya kazi
nzuri sana. Kuna fedha nyingi katika nchi za Dubai na Mauritius tena
zimewekwa katika miaka ya karibuni,” alisema Kabwe.
Alisema katika hoja yake kuhusu fedha hizo, Bunge
liliagiza Serikali kufanya uchunguzi na kupeleka taarifa bungeni kwa
hatua zaidi.
Naye Mayol akichangia mada kuhusu utorashaji wa
fedha za umma na ukwepaji kodi Afrika, alisema ni tabia ya wizi na
ufisadi haukuwahi kuwa sehemu ya utamaduni ya Mwafrika bali imerithiwa
kutoka kwa baadhi ya watawala wa kikoloni wanaoendelea kutumia uwezo wa
kiuchumi wa nchi zao na uelewa mdogo wa Waafrika kupora fedha na
rasilimali kuzihamishia nchini mwao.
Hoja hiyo ilionekana kuchafua hali ya hewa
ukumbini kiasi cha aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao wakati huo, Nehemiah
Modubule ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa SADCOPAC, kuingilia kati kumtaka
asubiri mada inayofuata ya Zitto Kabwe inayozungumzia utoroshaji wa
fedha na rasilimali nje ya Afrika.
Mayol aliyeonekana kuzungumza kwa hisia kali
aliwambia wajumbe zaidi ya 300 wa mkutano wa kumi wa umoja wa SADCOPAC,
kuwa kwa kawaida kijana mdogo (mtoto), hawezi kuwa mwizi hadi pale
anapofundishwa na kaka yake, akihusishwa mfano huo na tabia ya wizi
Afrika kuigwa kutoka kwa nchi zilizoendelea.
Akiwasilisha mada ya utorashaji wa fedha na
rasilimali za umma nje ya nchi zinazoendelea, Mwenyekiti wa PAC
Tanzania, Zitto Kabwe aliunga mkono hoja ya mbunge Mayol kwa kusema kati
ya mwaka 2000-210 zaidi ya dola dola za Kimarekani 844 bilioni
zilitoroshwa kutoka nchi zinazoendele kwenda nchi za Ulaya na Marekani
huku asilimia 69 sawa na dola za bilioni 582 zikitoroshwa kutoka barani
Afrika.
Kwa mujibu wa Zitto ambaye ni mbunge Kigoma
Kaskazini (Chadema), njia zinazotumika kutorosha fedha na rasilimali za
nchi zinazoendelea zikiwemo za Kiafrika ni pamoja na wizi, rushwa,
bakshishi kupitia mikataba ukwepaji kodi na ushushaji thamani wa bidhaa
maligafi kutoka Afrika.
Source: Mwananchi
Source: Mwananchi