. Picha na Edwin Mjwahuzi
Kwa ufupi
Mkosamali ambaye pia ni mjumbe katika Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, alisema ni vyema sheria
ikasema wajumbe wa Bunge hilo watatoka katika taasisi zipi.
Dodoma. Miswada ya Sheria ya Marekebisho ya
Mabadiliko ya Katiba na wa Kura ya Maoni inayotarajiwa kuanza
kuwasilishwa bungeni kesho inaonekana kuwa kaa la moto kwa Serikali
kutokana na wabunge wengi kujipanga kupinga baadhi ya vifungu.
Vyanzo mbalimbali viliwaambia waandishi wetu jana
kuwa kumekuwapo na mvutano mkali miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya
Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge kiasi cha kuilazimisha Serikali
kukubali baadhi ya mapendekezo muhimu.
Habari zimeeleza kuwa kutokana na mvutano huo,
wiki iliyopita wajumbe wa kamati hiyo walirudisha miswada hiyo kwa
Serikali ili kuifanyia marekebisho na kuirudisha tena mbele ya kamati.
“Hata sasa hivi tunapozungumza (jana mchana),
kamati inakutana ili kupitia tena vipengele vya miswada hiyo,”
kilidokeza chanzo chetu bila kufafanua kama ilikuwa inajadili vipengele
vipya au la.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo,
William Ngeleja alisema hakukuwa na mvutano wowote kati ya kamati yake
na Serikali bali, majadiliano ya kawaida tu ili kuweka mambo sawa.
“Unajua kwenye maandalizi ya miswada mara nyingi
kunakuwapo mashauriano mengi kati ya Serikali na kamati husika,” alisema
Mbunge huyo wa Sengerema (CCM).
Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe
alikiri kupokea mapendekezo kutoka kwa wabunge na hasa kwenye Sheria ya
Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba akisema wametaka kuangaliwa upya kwa
kipengele cha Kamati ya Uteuzi ya viongozi wa Bunge la Katiba. Alisema
sasa wataweka sifa za mwombaji wa nafasi hizo na wasiokuwa nazo
hawatagombea.
Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter
Msigwa alisema moja ya mambo ambayo yanabishaniwa ni hatua ya Tume ya
Taifa ya Uchaguzi (NEC), kupewa mamlaka ya kusimamia kura ya maoni
wakati taasisi hiyo inalalamikiwa kwa kutokuwa huru.
Alisema kipengele kingine ni siku 30
zinazopendekezwa na sheria za kufanya kampeni kwa wananchi kwa ajili ya
kupiga kura ya Ndio au Hapana akisema ni muda mdogo mno.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, moja ya mambo
yanayopingwa na wabunge ni ile sheria ya kuwapata wajumbe wa Bunge la
Katiba hilo kutoka katika makundi ya jamii.
Muswada wa Katiba ya Mabadiliko ya Katiba unataka
wawakilishi kutoka makundi ya Jamii kuwa 166 katika Bunge la Katiba
lakini wabunge wanataka idadi iwe 200.
Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi)
alisema uzoefu katika nchi nyingine unaonyesha Mabunge ya Katiba
hushirikisha watu wengi ili kupata uwakilishi mpana tofauti na
mapendekezo ya miswada hiyo.
Mkosamali ambaye pia ni mjumbe katika Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Katiba, Sheria na Utawala, alisema ni vyema sheria ikasema wajumbe wa
Bunge hilo watatoka katika taasisi zipi.
Kifungu kingine ni kile kinachohusu Kamati ya
Uteuzi wa Mwenyekiti na Makamu wake ambao kwa mujibu wa muswada itaundwa
na Spika wa Bunge la Jamhuri na Spika wa Baraza la Wawakilishi,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (AG) na
yule wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Waziri wa Katiba na
Sheria Tanzania Bara na Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar na
Kiongozi Rasmi wa Kambi ya Upinzani Bungeni.
Mkosamali alisema muswada huo wa Mabadiliko ya
Katiba unasema mwenyekiti wa muda atakuwa Spika wa Bunge lakini akataka:
“Mwenyekiti wa muda atokane na Chama cha Majaji wastaafu maana wao
hawafungamani na upande wowote.”
Kuhusu Muswada wa Sheria ya Kura za Maoni,
alieleza kuwa unasema wananchi wa Zanzibar watahusika kupiga kura katika
mambo 22 ya Muungano yaliyopo katika Katiba ya sasa tu... “Wapigie kura
mambo yote yaliyo katika Katiba kwa sababu hii ni ya Jamhuri ya
Muungano.”
Pia katika muswada huo, madaftari ya orodha ya
wapigakura yatakayotumika ni yaleyale yanayoratibiwa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC) na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ambayo bado
hayajaboreshwa.
“Kwa Zanzibar ili uandikishwe katika daftari la
wapiga kura lazima uwe na vigezo vya ukaazi lakini huku Bara kama
Kariakoo kuna Wapemba wengi wafanyabiashara hawa utawatenganisha vipi
katika upigaji wa kura?” alihoji.
Alisema miswada hiyo imepangiwa siku mbili na kila mmoja utajadiliwa kwa siku moja, muda ambao alisema ni mdogo.
source: Mwananchi
source: Mwananchi