Thursday, 12 September 2013

Sakata la Diamond, Dayna na Baba Levo

Dyna 
Na Herieth Makwetta, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Septemba12  2013  saa 10:20 AM
Kwa ufupi: Mpaka sasa msanii Mwanaisha Nyange maarufu ‘Dayna’ amedai kuwa Diamond amemwibia mdundo wa wimbo wake aliohitaji kumshirikisha, huku mwanahiphop Clayton Revocatus ‘Baba Levo’ akidai kuibiwa kibwagizo cha wimbo huo. 


Dayna aamua kukomaa, apanga kumpeleka mtayarishaji Mahakamani iwapo hatakuwa na majibu ya kueleweka kuhusiana na sakata hilo
Dar. Wakati video ya wimbo mpya wa mwanamuziki Naseeb Abdul maarufu kama Diamond, ‘Number One’ ikizidi kuchana mawimbi nchi mbalimbali barani Afrika na kuangaliwa na watu wengi mtandaoni, wasanii mbalimbali wamejitokeza wakidai kwamba nyota huyo ameiba mawazo yao na kwenda kutengeneza wimbo huo.
Mpaka sasa msanii Mwanaisha Nyange maarufu ‘Dayna’ amedai kuwa Diamond amemwibia mdundo wa wimbo wake aliohitaji kumshirikisha, huku mwanahiphop Clayton Revocatus ‘Baba Levo’ akidai kuibiwa kibwagizo cha wimbo huo. Dayna anasema miezi sita iliyopita alifika katika studio ya Burn Records ambako alitengenezewa mdundo.
“Nilifika kwa Sheddy miezi kama sita au saba hivi iliyopita nilitengeneza demo (mfano wa wimbo unavyotaka uwe) na kwenda kumpa Diamond ili nimshirikishe kwenye wimbo wangu, nashangaa tuhuma za Sheddy anazozitoa sasa kwani yeye amemfahamu Diamond kupitia mimi na si kama anavyozungumza kwenye vyombo vya habari sasa hivi,” aling’aka Dayna.
Anasema mdundo wa wimbo huo alikuwa nao tayari na kwamba kauli za prodyuza huyo zinazidi kumpa maumivu
Baba Levo
Clayton Revocatus maarufu ‘Baba Levo’ naye analalamika kuhusu wimbo huo akidai kuwa kibwagizo cha wimbo huo ni wazo lake aliloliwakilisha kwa Diamond lakini amemzunguka.
“Zamani nilikuwa nikisikia mtu analalamika kaibiwa wimbo. Nilikuwa naona ni kama maigizo na mtu kutafuta sehemu ya kujipatia umaarufu. Ila leo nasema wazi Diamond Platnumz amechukua korasi (kibwagizo/kiitikio) ya wimbo wangu niliopanga kufanya naye. Wimbo huo unaitwa Sweety Sweety, lakini yeye ameuingiza kwenye wimbo wake mpya Number One, alinizungusha sana kumbe alikuwa na lengo lake, ila mimi sina neno na nimeamua kumsamehe tu,” alisema Baba Levo.
Kauli ya Diamond
Mwananchi pia lilimtafuta mhusika mkuu ambaye ni Diamond (pichani kulia) aliyewasili akitokea nchini Kenya Nairobi mwanzoni mwa wiki hii ambaye hakutaka kuwajibu wasanii hawa wanaolalamika zaidi ya kuhitaji apewe muda wa kumpumzika na maneno.
Diamond alisema kwa sasa hawezi kushughulika na kazi ya kujibu tuhuma za kila siku, ambazo kwa mujibu wa nyota huyo zinampotezea muda.
“Kwa kweli tuhuma hizi nimezisikia na hata Baba Levo aliamua kuandika kwenye ukurasa wake wa facebook. Lakini mimi sina cha kusema kwa sasa maana tuhuma zinazoelekezwa kwangu kwa sasa zimekuwa nyingi binafsi nimeamua kukaa kimya,” alisema nyota huyo.

Prodyuza
Mtayarishaji wa wimbo huo anayetuhumiwa kuhamisha mdundo kutoka kwa msanii mmoja kwenda kwa mwingine Shedy Clever wa Burn recods alisema;
“Beat hii nilitengeneza mimi kwa mawazo yangu mwenyewe, alivyokuja Dayna akaupenda ule mdundo, na mimi sikumnyima akafanya demo lakini hakulipia kabisa. Ikapita zaidi ya miezi sita kila nikimuuliza vipi anasema bado atakuja kufanya.
“Kuna siku Diamond alikuja studio, akataka kusikia midundo nikacheza midundo tofauti, akavutiwa sana na ule ambao Dayna alifanya demo.
“Nikampigia Dayna na kumwelezea kwamba Diamond kapenda kufanya kazi katika ule mdundo, Dayna akakubali nashangaa yeye kusema Diamond kamwibia wakati alikubali.
source: mwananchi