Friday 20 September 2013

Taarifa za kiitelijensia zinavyookoa tembo


Na Daniel Mjema, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Septemba19  2013  saa 13:5 PM
Kwa ufupi
419 Idadi ya tembo waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini.
 1,645Mbao zilizokamatwa baada ya kuibwa katika hifadhi  nchini

Kinapa inatakiwa kutoaelimu zaidi ya ujasiriamali kwa jamii ili kuwapa uwezo wa kuanzisha miradi.
Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (Kinapa) ni moja ya hifadhi 16 nchini ambayo imefanikiwa kudhibiti vitendo vya ujangili wa tembo ambao wamekuwa wakiuawa na wahalifu wanaotafuta vipusa.
Takwimu zilizotolewa na Mhifadhi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa nchini (Tanapa), Mtango Mtahiko zinaonyesha kati ya 2009 hadi 2012, wanyamapori 15,227 waliuawa ndani ya hifadhi hizo.
Kati ya wanyamapori hao, 419 ni tembo waliouawa katika hifadhi mbalimbali huku hifadhi ya Ruaha ikiongoza kwa tembo 131 kuuawa ikifuatiwa na Serengeti 92, Tarangire 53, Katavi 36 na Mikumi 30.
Mkuu wa Idara ya Ulinzi na Uokoaji Kinapa, Sebastian Gambares anasema ujangili wa tembo umepungua kwani mwaka 2012/2013 hakukuwa na tukio la kuuawa kwa tembo ndani ya hifadhi hiyo.
“Hata matukio ya nyuma ya kuuawa kwa tembo yalihusisha matukio ya kuuawa nje ya hifadhi, Kinapa tumekuwa makini sana katika kudhibiti Majangili,”anabainisha mhifadhi huyo.
Anasema wanapobaini kuwapo kwa tembo katika eneo fulani hasa tembo wanaotoka Hifadhi ya Amboseli nchini Kenya, basi kikosi cha kupambana na ujangili kinakuwapo karibu na maeneo hayo.
Naye Mkuu wa Hifadhi ya Kinapa, Kanda ya Kaskazini Magharibi, Imani Kikoti anasema moja ya mikakati iliyosaidia udhibiti wa ujangili ni kubadilishana taarifa za kiitelejensia kwenye maeneo ya mipakani.
Kikoti anasema Kinapa imeamua kudhibiti ujangili wa tembo kwa kuwa wanaweza kutoweka kama udhibiti makini hautakuwapo katika maeneo waliopo.
Kwa mujibu wa Kikoti, katika kipindi  cha 2009 hadi 2012, idadi ya majangili wanaokamatwa imekuwa ikipungua kutoka 320 mwaka 2009 hadi majangili 278 mwaka 2012/2013.
Anasema mikakati ya kukabiliana na ujangili inahusisha pia ujangili wa mazao ya misitu, kuwasha moto kwenye hifadhi na uingizaji mifugo kwenye maeneo ya hifadhi kwa uharibifu huo unaathiri  vyanzo vya maji.
Kikoti anasema kushuka kwa idadi ya mbao na nguzo zinazokamatwa ni dalili tosha kwamba vitendo vya ujangili wa mazao ya misitu ndani ya hifadhi vimekuwa vikidhibitiwa kwa kiasi kikubwa.

CHANZO: GAZETI LA MWANANCHI