MKAZI wa Temeke Mikoroshini, Dar es Salaam, Mwanaidi Mruma amemwagiwa maji yanayodaiwa kuwa tindikali na shemeji yake na kumsababishia uoni hafifu.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Mwanaidi alidai kuwa tukio hilo lilitokea Jumapili jioni nyumbani kwao akijiandaa kupika mlo wa usiku kwa ajili ya familia yake.
Akizungumza na mwandishi wetu jana, Mwanaidi alidai kuwa tukio hilo lilitokea Jumapili jioni nyumbani kwao akijiandaa kupika mlo wa usiku kwa ajili ya familia yake.
Kwa sasa jicho lake la kushoto limevimba huku lingine likifunguka lakini yote yakitoa machozi muda wote.
Akisimulia, alidai kuwa kabla ya tukio alipita mdogo wake na kumwomba amsindikize gengeni kununua bidhaa ambazo alitumwa na mama ambako ni karibu na anakoishi Mwanaidi.
“Baada ya kufika nyumbani kwa wazazi wangu nilijadiliana nao masuala kadhaa na kisha kuaga kurejea kwangu ambako nilifika na kumkuta shemeji Shaban Ali akiwa nje amekalia dumu akionekana mwenye hasira na amelewa,” alisema Mwanaidi na kuongeza kuwa hakumwuliza chochote akaingia ndani na kuuliza wapangaji kilichotokea.
Alisema wapangaji wakiwa wamejifungia ndani kwa hofu, walimwambia waume zake walitaka kuuana na baada ya kusikia hivyo, Mwanaidi aliingia ndani na kuendelea kuandaa chakula ndipo shemeji yake akiwa na dumu alimmwagia kitu kama maji ambayo alidai yalimwasha na kushindwa kuona vizuri.
Aliongeza kuwa kutokana na tukio hilo akiwa hajui alichomwagiwa ni tindikali au maji ya betri, alichukua wanawe wawili na kupigia simu wazazi wake waje kumsaidia, wakaja na kwenda kituo cha Polisi cha Sandali kuripoti na kupewa fomu ya matibabu PF3 namba, Sand/RB/474/2013.
Aidha, alisema kituoni hapo alikutana na mumewe aitwaye Likwatu Ali ambaye alikwenda kutoa taarifa za kushambuliwa na ndugu yake huyo, Shaban, akidai alikuwa na hasira dhidi ya mmoja wa wapangaji ambaye hakuwa amemalizia sehemu ya kodi ya pango.
Likwatu alidai ugomvi ulianza jioni baada ya kaka yake huyo kufika amelewa ambapo alimwita na kumwuliza juu ya mpangaji aliyelipa kodi nusu lakini yeye akamhakikishia kuwa asiwe na wasiwasi kwani fedha italipwa tatizo ni hali ya uchumi kwa sasa kuwa mbaya.
Katika hatua nyingine, Mwanaidi aliongeza kuwa shemeji yake huyo hajui ana visa gani naye, kwani mbali ya kuwa msaada mkubwa kwake akimpikia chakula mtoto wake anayesoma darasa la saba, lakini pia aliwahi kumtamkia kuwa ipo siku atamnyonga, na ugomvi huo kumalizwa na baba mzazi wa mumewe.
Kuhusu tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Temeke, Englibert Kiondo alisema taarifa hizo hazijafika ofisini kwake rasmi na kumtaka Mwanaidi aende haraka ofisini kwake, ili kuwezesha kupatikana kwa mtuhumiwa, kwani huenda akawa ni mmoja wa watuhumiwa wa tindikali wanaotafutwa na Jeshi hilo.
IMETOLEWA KATIKA MTANDAO WA BONGO NEWS