Thursday 12 September 2013

UN yakosoa TZ kwa kuwafukuza wakimbizi

 
Imebadilishwa: 12 Septemba, 2013 - Saa 13:07 GMT
Baadhi ya wahamiaji haramu waliolazimishwa kurejea makwao na Tanzania
Umoja wa Mataifa umesema kuwa takriban wakimbizi elfu 25 kutoka Burundi wameondoshwa Tanzania kwa nguvu katika mwezi mmoja uliopita.
Afisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi amesema malori yanayowasafirisha warundi yamekuwa yakivuka mpaka kila siku , huku wakimbizi wengi wakikosa mahitaji muhimu kama vile maji na chakula .
 
Katika wiki za hivi karibuni, Tanzania imekuwa ikiwafukuza wakimbizi kutoka Burundi, Rwanda na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo .
Kwa miaka mingi Tanzania iliwahifadhi mamilioni ya wakimbizi waliokuwa wakiyakimbia mapigano katika nchi jirani .
Takriban watu milioni moja walitoroka kutoka Burundi na kuingia Tanzania wakati wa mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe wakati vita vilipozuka mwaka 1993. Wengi walirejea kwa hiari wakati amani ilipopatikana mwaka 2006.
Lakini inaonekana Tanzania haina tena uvumilivu kwa swala hilo. Nchi hiyo imekuwa makao kwa mamilioni ya wakimbizi katika kipindi ya zaidi ya miaka kumi iliyopita kutokana na migogoro katika eneo la maziwa makuu.
Maafisa sasa wameanza kupiga jeki juhudi za kuwaondoa wakimbizi hao kutoka Burundi, Rwanda, na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo kwa nguvu wakiwataka kurejea makwao.
Tanzania inasema kuwa wakimbizi hao ni wahamiaji haramu.
Shughuli hii imetokea wakati mmoja na mgogoro wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Rwanda ambayo imekuwa ikikanusha madai ya kuchochea vurugu katika Jumuhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Mgogoro ndani ya Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo nao unaendelea kuchochea idadi ya wakimbizi wanaotoroka vita na kuingia katika nchi jirani.

SOURCE: BBC