Sunday 22 September 2013

VITA YA MADAWA YA KULEVYA: Polisi kufuatilia nyendo za Masogange, Melissa

Agnes Gerald, maarufu Masogange katika pozi 

Na Florence Majani, Mwananchi

Posted  Jumapili,Septemba22  2013  saa 1:1 AM
Kwa ufupi
Hatua hiyo iliyotangazwa na Kamishna Mkuu wa kitengo hicho, Geofrey Nzowa, imekuja siku moja baada ya Watanzania hao, Masogange na Melissa kuachiwa huru na Mahakama ya Kempton Park ya Afrika Kusini.

Johannesburg. Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini, kimewataja Agnes Gerald, maarufu Masogange, na Melissa Edward kuwa watafuatiliwa nyendo zao kwa umakini.
Hatua hiyo iliyotangazwa na Kamishna Mkuu wa kitengo hicho, Geofrey Nzowa, imekuja siku moja baada ya Watanzania hao, Masogange na Melissa kuachiwa huru na Mahakama ya Kempton Park ya Afrika Kusini.
Nzowa alizungumza jana na mwandishi wa habari hii kwa njia ya simu, kuwa watu hao wataangaliwa kwa umakini watakapokuwa wakisafiri nje ya nchi.
Vilevile, alisema wataimarisha ukaguzi kwa Watanzania wengine, wenye historia ya kubeba dawa za kulevya wanaposafiri kwenda nje ya nchi.
“Masogange na Melissa tutawaangalia kwa jicho la umakini zaidi watu hawa,lakini siyo hao tu hata Watanzania wengine kwa sababu umdhaniaye siye kumbe ndiye,” alisema Nzowa.
Nzowa alisema Watanzania watakaokamatwa na dawa za kulevya nchini au nje na wataadhibiwa kulingana na sheria kama Masogange alivyoadhibiwa.
Hata hivyo, juzi Nzowa alionyesha kushangazwa na hukumu waliyopewa Masogange na Melissa akisema kuwa ni ndogo ukilinganisha na kiasi kikubwa cha kemikali walizobeba.
Hapa jijini Johannesburg, Masogange na Melissa jana walionekana wakitembelea maeneo mbalimbali ya jiji hilo ikiwamo madukani wakifanya ununuzi na katika saluni za urembo.
Mtu wa karibu na watu hao alisema, Watanzania hao hawana hofu ya kufanya chochote kwa sababu mahakama imegundua kuwa hawana hatia.
“Waogope kutembea barabarani kwa sababu gani wakati wameachiwa huru? Mahakama imefanya kazi yake na wao wana haki,” alisema mtu huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Julai 5 mwaka huu, Masogange na Melissa walikamatwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Oliver Tambo Afrika Kusini wakiwa wamebeba kilo 150 za dawa za kulevya aina ya crystal methamphetamine (Tik).
Hata hivyo, baada ya kukaa mahubusu kwa takriban miezi mitatu, mahakama ya Kempton inayoshughulikia makosa ya jinai, ilibaini kuwa Watanzania hao hawakubeba dawa za kulevya bali kemikali zinazotumika kutengeneza dawa za kulevya aina ya ephedrine.

 Masogange alihukumiwa kwenda jela miezi 30 au kulipa faini ya fedha za Afrika Kusini R30,000 (Sh4.8 milioni), ambapo alilipa faini hiyo. Melissa aliachiwa huru baada ya kukosekana ushahidi wa kumuhusisha na dawa hizo.

SOURCE: MWANANCHI