Na Goodluck Eliona na Ibrahim Yamola, Mwananchi
Posted Jumapili,Septemba22 2013 saa 1:0 AM
Posted Jumapili,Septemba22 2013 saa 1:0 AM
Kwa ufupi
- Upinzani watangaza Oktoba 10 kuwa siku ya Watanzania wote kushiriki katika maandamano kushinikiza wapewe haki ya kuandaa Katiba yao.
- Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF, kuendelea kupinga mchakato wa Katiba, wasema hawako tayari kuridhia Kikwete asaini Muswada wa Marekebisho ya Katiba.
Dar es Saalam. Vyama vya
upinzani jana vilifanya mkutano mkubwa kuwashawishi wananchi kupinga
kile walichokiita kuhujumiwa kwa mchakato wa Katiba Mpya, wakitangaza
Oktoba 10 kuwa siku ya Watanzania wote kushiriki katika maandamano
kushinikiza wapewe haki ya kuandaa Katiba yao.
Wakizungumza kwa kupokezana katika Viwanja vya
Jangwani, jijini Dar es Salaam jana, wenyeviti wa vyama vya Chadema,
NCCR-Mageuzi na CUF, walieleza kuwa wataendelea kushirikisha taasisi za
kiraia kupinga hujuma dhidi ya mchakato wa Katiba Mpya na kwamba
hawatakubali endapo Rais Jakaya Kikwete atasaini Muswada wa Marekebisho
ya Mabadiliko ya Katiba Mpya.
Akizungmza katika mkutano huo Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Lipumba alisema chama chake hakitakubali endapo Rais Kikwete
atasaini muswada huo kwa kuwa una lengo la kupata Katiba Mpya isiyokuwa
na tija kwa taifa. Alisema kuwa Katiba inayoandaliwa ni kwa ajili ya
Watanzania wote na siyo kundi la watu, hasa CCM na kwamba mchakato wa
kuwapata wajumbe 166 wa Bunge la Katiba kutoka makundi mbalimbali siyo
sahihi.
“Haiwezekani kila taasisi ikateuwa wajumbe tisa
ambao majina yao yatakwenda kuchakachuliwa na usalama wa taifa, kisha
kupata majina ya watu wanaowataka wao, kitu hiki kama CUF hatutakubali,”
alisema Profesa Lipumba na kuongeza:
“Hatutarudi nyuma na kukubali kuendelea na
mchakato huu endapo Rais atasaini muswada huu. Tutaendeleza harakati za
kupinga kwani bila hivyo tutapata Katiba Mpya isiyokuwa na tija.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia alisema kuwa ni wakati wa kukaa meza moja ya mazungumzo kuondoa
tofauti zilizopo ili kulinusuru taifa kuingia katika machafuko.
Alisema kama taifa, linatakiwa kujifunza kutoka
mataifa mengine yalivyotokea maafa katika michakato ya kuandikwa kwa
Katiba Mpya.
“Ni wakati wa kukaa meza moja, kwa kushirikisha
wadau mbalimbali kwani Katiba inayotafutwa ni ya Watanzania wote na siyo
ya CCM,” alisema Mbatia na kuongeza:
“Lazima tupate Katiba Mpya kwa gharama yoyote ile,
iwe ndani au nje ya Bunge ili kuhakikisha tunapata Katiba ya Watanzania
wote.”
Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe alisema kosa
kubwa katika kudai haki ni woga na hatutapata Katiba Mpya kama
tutaendelea kuwa taifa la watu wenye hofu. Tunataka kukutana na makundi
mbalimbali katika jamii ambayo ni viongozi wa dini, wasomi na watu wa
makundi mengine kuwaeleza kinachoendelea sasa hivi.
Hata migogoro ya kiimani baina ya Wakristo
iliyotokea nchini imesababishwa na katiba iliyopo sasa, kama Rais
atasaini wao hawatashiriki Bunge la Katiba na watatumia kila mbinu
iliyopo duniani kuueleza umma nini kimetokea na hawataendelea
kunyenyekea vitisho vya Jeshi la Polisi.
Tunalaani mchakato wa katiba kuhodhiwa na chama
kimoja na tunatangaza Oktoba 10, mwaka huu kuwa ni siku maalumu ya kudai
katiba na sasa hawataenda tena Ikulu kwani inaaminika huko ni kwenda
kunywa chai na watatangaza maandamano nchi nzima.
“Tumemwambia IGP (Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali
Said Mwema) kuwa hatutaomba ruhusa bali tutampa taarifa.Tunaomba walio
makanisani na misikitini kutafuta katiba mpya na jambo la mwisho
Jumatato tutaenda kufanya mkutano kama huo Zanzibar,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti wa Chama cha NLD, Dk Emmanuel Makaidi
alisema chama chake kinapinga namna mchakato wa Katiba ulivyoendeshwa
kwasababu kilichopelekwa bungeni kilikuwa Muswada wa Katiba Mpya, lakini
kilichopo mitaani ni Mchakato wa Rasimu ya Katiba Mpya.
“Tunawaambia CCM hawatengenezi Katiba Mpya,
wanachofanya ni danganya toto kwa kuwa wanatakiwa kuirudisha Katiba ile
ile ya awali.
Naye Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible
Fellowship (FGBF), Zacharia Kakobe aliyefika katika viwanja hivyo
alisema kuwa Rais Kikwete akisaini muswada huo, Watanzania watajua kuwa
hana nia njema na taifa kwa kuwa wengi wanaipinga.
“Mimi natega masikio kusikia kama utasaini au la
ili kujua kama unawatega na kuwahadaa Watanzania. Tunakuomba usikubali
mtego huo,” alisema Kakobe akimwambia Rais Kikwete.
Alisema tangu awali CCM ilikuwa ikipinga
kuandaliwa kwa Katiba Mpya, ingawa Rais Jakaya Kiwete alijitosa na
kukubali mchakato huo kuanza nchini.
“CCM ilikataa katakata Katiba isianzishwe. Jakaya
Kikwete pekee yake alijipiga kifua akakubali ingawa alishambuliwa kuwa
amefanya makosa,” alisema Kakobe.
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kukuu cha Dar es
Salaam(Udsm), Dk Azaveli Lwaitama alisema kuwa duniani kote shinikizo la
kuundwa kwa Katiba Mpya hutoka nje ya Bunge na Serikali iliyopo
madarakani.
“Tangu mwaka 1992 vyama vya upinzani vilikuwa
vikitaka Katiba Mpya... Katiba Mpya huzaliwa na wanamapinduzi waliopo
nje ya Bunge,” alisema Dk Lwaitama.
Akizungumzia ushirikiano wa vyama kumzuia Rais
asisaini Sheria ya Rasimu ya Katiba, alisema: “ Ukifanya jeuri kwa
sababu upo madarakani, watu uliodhani wamegombana watashirikiana.”
Mbunge wa Ubungo John Mnyika, alisema Mahakama ya wananchi ndiyo itakayotoa uamuzi wa mwisho.
“Ninyi ndiyo Mahakama yenye uamuzi wa mwisho, tunasubiri mwongozo wenu, mtakachosema tutafanya,” alisema Mnyika.
Kabla kuwasili kwa viongozi wakuu wa vyama hivyo vya siasa
kwenye Viwanja vya Jangwani, jana wafuasi wao walikuwa kwenye makundi
wakichambua baadhi ya mambo yaliyoonekana kuleta utata kwenye mchakato
wa Katiba Mpya.
Rangi za bluu, nyekundu na nyeupe zinazotumiwa na
vyama vilivyoshiriki kumtaka Rais Jakaya Kikwete kutosaini Muswada wa
Marekebisho ya Mabadiliko ya Katiba Mpya zilionekana kuzagaa katika
viwanja hivyo.
Magari ya Polisi yalionekana kuzunguka maeneo ya viwanja hivyo kuhakikisha ulinzi unaimarika wakati wote wa mkutano.
Nao wafuasi wa vyama hivyo waliokuwa wamevaa suti
nyeusi, miwani na mashati meupe waliimarisha ulinzi katika eneo la
mkutano, wengine wakiingia Viwanja vya Jangwani kutoka eneo la Barabara
ya Morogoro, huku wakibeba mabango, bendera za vyama hivyo na picha za
viongozi wao wakiimba nyimbo mbalimbali.
Wengi wa wafuasi hao walifika uwanjani hapo kwa
kuletwa na mabasi madogo aina ya Coaster na wengine wakija kwa makundi
kutokana Jeshi la Polisi kuzuia kufanyika kwa maandamano.
SOURCE: MWANANCHI