Na Beatrice Moses, Mwananchi,
Posted Ijumaa,Septemba13 2013 saa 10:59 AM
Posted Ijumaa,Septemba13 2013 saa 10:59 AM
Kwa ufupi
Wahusika hao ni pamoja na wamiliki wa viwanda
mbalimbali vyenye maabara, shule zinazotumia kemikali katika masomo ya
vitendo na hospitali.
Huweza kusababisha madhara makubwa kwa viumbehai hususan binadamu, hasa zile zilizoisha muda wa matumizi.
Dar es Salaam. Mkemia Mkuu wa
Serikali, Profesa Samwel Manyere, amewataka waliohifadhi kemikali
zilizochakaa kujisalimisha na kutoa maelezo kwenye ofisi yake, ili
kunusuru maisha ya watu na mazingira kwa jumla.
Akizungumza na gazeti hili jana, Profesa Manyere
alisisitiza kuwa, kuna kemikali ambazo ni hatari kuendelea kuhifadhiwa
kwa muda mrefu kwa kuwa licha ya kuharibu mazingira zinaweza kulipuka na
kusababisha moto unaoweza kuchangia hasara ya mali na maisha pamoja na
kuleta maafa.
Wahusika hao ni pamoja na wamiliki wa viwanda
mbalimbali vyenye maabara, shule zinazotumia kemikali katika masomo ya
vitendo na hospitali.
“Kemikali zilizochakaa, zimetunzwa kwa muda mrefu
ni hatari(sumu) kwa ardhi na maji ambayo yakitumiwa pia yanaweza
kusababisha madhara kwa viumbe hai ikiwamo mimea na binadamu, hivyo
tumewatumia barua wahusika ili watujulishe wamezitunza kwa muda gani,”
alisema na kuongeza:
“Kwa kuwa tunaamini zipo ambazo hazina lebo
pengine hata hazijulikani majina yake,tutazichunguza kwa umakini ili
zinazotakiwa kuharibiwa ziharibiwe na zitakazofaa kwa somo la kemia
tuweze kuzipeleka kwenye shule za sekondari zisaidie katika masomo ya
vitendo,” alisema Profesa Manyere.
Wakati huo huo Mkemia Mkuu huyo alizungumzia
kuhusu vibali vya uingizaji na usafirishaji wa tindikali kuwa mwisho
wake ni Novemba 30,mwaka huu,hivyo wote wenye uhitaji wajisajili upya
ili Serikali iweze kuwafuatilia kwa karibu baada ya matumizi yake
kugeuzwa silaha .
Alisema mwitikio wa kujisajili umepokewa vyema
katika ofisi za kanda ikiwamo Arusha, Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam
tangu wito huo ulitolewa mapema Agosti mwaka huu.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI