Saturday 14 September 2013

VIJANA NA SANAA. Soko limemrejesha GK



GK 
Na Herieth Makwetta, Mwananchi


Posted  Septemba14  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Alitamba na vibao kama Hii Leo na Sister Sister, hajabadilika sana lakini anasema kuwa ana mtazamo mpana na mawazo chanya yanayoweza kuubadilisha muziki wa sasa na kuwabadilisha wasanii kwa kiasi kikubwa.


King Crayz Gk. Ukitaja jina hili kwa wapenzi wa muziki nchini bila shaka watakwambia neno moja tu; Huyo ni mwanamapinduzi wa muziki wa kizazi kipya kwa miaka saba nyuma.
Ukikaa naye kwa muda, utagundua kwamba mkongwe huyo wa muziki wa kizazi kipya, ana matumaini makubwa ya kuufanya muziki huo kuwa ajira itakayokuza kipato cha wasanii miaka miwili ijayo.
Gwamaka Kaihula jina lalisi la ‘GK’ akiwa na mwili wa wastani na sauti kama ilivyokuwa miaka saba iliyopita wakati huo akitamba na kundi lake la East Coast Team. Alitamba na vibao kama Hii Leo na Sister Sister, hajabadilika sana lakini anasema kuwa ana mtazamo mpana na mawazo chanya yanayoweza kuubadilisha muziki wa sasa na kuwabadilisha wasanii kwa kiasi kikubwa.
Yafuatayo ni mahojiano kati ya msanii huyo na Starehe.
Starehe: Ulikuwa wapi kwa kipindi cha miaka saba?
GK: Kwanza kabisa ieleweke, muziki upo kwenye damu yangu, pili nilikuwa nasomea shahada ya kwanza kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini, Dar es Salaam Campus (TUDARCO), masomo yalibana sana, nilikuwa natafuta shahada, sasa nimepata na nimerudi kufanya muziki, pia kusaidia chipukizi.
Starehe: Kipindi chote hicho ulikuwa shule, elimu yako imeishia hapo kwa sasa au unadhani inafaa kuendeshea shughuli zako za muziki?
GK: Siyo kwa kipindi chote hicho ila naomba nieleweke kwamba nilikuwa bize na mambo kadhaa. Elimu yangu ndiyo kwanza nimeianza kwani natarajia kujiunga na shahada ya pili ‘Masters’ mwezi Novemba mwaka huu Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Starehe: Una mikakati ya kuajiriwa siku za usoni baada ya kumaliza elimu yako?
GK: Upeo wangu umekuwa mpana mno, kwa sasa nafikiria kufanya makubwa katika sekta ya muziki. Sifikirii kuajiriwa, lakini tayari nimeshajiajiri. Nimeanza kwa kufungua Kampuni ya East Coast Team itakayokuwa ikiuza milio ya simu ya wasanii, sanjari na kuibua vipaji vya wasanii. Siyo hivyo tu, nimerudi katika muziki kuleta chachu zaidi.
Starehe: Kwa nini umeamua kurudi?
GK: Sikuamua kuacha muziki maisha yangu yote, ila nilikaa nikatafakari, nilipanga kuwa nitaacha muziki niende kupata elimu, nashukuru Mungu kwani elimu imenifungua sana. Kazi niliyokuwa naifanya zamani kwa sasa naona kama ni takataka, nimekua sasa, najua nini kinahitajika na ninaimba kwa ajili ya nani. Zamani niliimba mambo ya ugomvi na mabifu, lakini leo hii naimba kwa ajili ya Watanzania na Waafrika.
 tarehe: Wasanii wengi waliopotea hutumia nguvu kubwa kurudi katika muziki, unadhani unaweza kurudi na kuwa GK yule wa zamani na utatumia mbinu zipi?
GK: Nadhani kila Mtanzania ameona kazi yangu mpya ‘Baraka au Laana’ niliyoiachia katika redio mbalimbali na video yake katika vituo vya televisheni. Kazi hiyo pekee imefanikiwa kunirudisha kwenye muziki, lakini siyo hivyo, tu bali wameipenda kazi yangu.
Mimi ni GK na nina kipaji kikubwa hasa kwani nia yangu ni kuona tasnia hii inasonga mbele ya kuwekeza nguvu zangu nyingi kuinua chipukizi na kuusimamia muziki ipasavyo. Pia kuhakikisha wasanii wananufaika na jasho lao kupitia Kampuni ya East Coast Team.
Starehe: Ni nini wazo la wimbo wa ‘Baraka au Laana’, kundi lenu inakuwaje?
GK: Nimerudi kwenye gemu baada ya kuona kuwa bado nahitajika na nimeamua kuja na ngoma ambayo ni swali kubwa kwa Waafrika kama kuzaliwa Afrika ni Baraka au Laana. Kazi hii ni mwanzo wa ujio mpya wa kishindo katika game ya muziki Tanzania kuleta ladha na ushindani mpya. Wiki tatu zijazo nitatoa kazi mpya na kali ambazo ni kolabo, zitakazoturudisha tena pamoja East Coast Team akiwamo AY pamoja na Mwana FA ndani yake.
Starehe: Muziki kwa sasa umebadilika, staili yako ya muziki nayo imebadilika?
GK: Crayz GK wa leo anaimba na kurap tofauti kabisa na zamani ambako nilirap tu. Najua soko lipo vipi na ninaujua muziki. Kwa sasa kila kitu nafanya, natunga mashairi, naimba  na natayarisha muziki. Upeo wa kimuziki umekuwa mkubwa, natafiti muziki nipite njia gani ili niweze kufika kule niendapo, muziki unahitaji utulie, ujue watu fulani wanataka nini na unamwimbia nani na kwa wakati gani.
Starehe: Kitu gani huwezi kukiacha ambacho zamani ulikifanya na sasa utaendelea kukifanya?
GK: Kwa sasa nimebadilika sana kimuziki, zamani nilikuwa naimba kwa kujibu mapigo, maneno kadhaa kurushiana vijembe, lakini kwa sasa ninakuja tofauti ila siwezi kuacha vita ya maneno kwani ni nzuri katika kuleta ushindani.
Starehe: GK umeoa au una mchumba?
GK: Ha ha ha ha, kama ninapata maziwa, kuna haja ya kufuga ng’ombe.
Starehe: Ni mtu gani unayempenda zaidi katika maisha yako?
 GK: Mama yangu mzazi Naomi Kaihula, nampenda sana. Hata hivyo, nakiri upendo wake kwangu kwani kwa kipindi chote amekuwa akinihimiza katika mambo mengi mazuri yakiwemo masomo na vitu vilivyo vya msingi katika maendeleo ya maisha yangu.
SOURCE: MWANANCHI