Saturday 14 September 2013

UTENDAJI BORA: CAG amkagua wakala wa meli Z’bar


Mkurugenzi wa Mamalaka ya usafiri Zanzibar (ZMA) Abdi Omar Maalim akionyesha fomu za mashariti ya usajili wa meli kufuatia kukamatwa kwa meli ya MV Gold Star ikiwa na tani 30 za bangi meli hiyo imesajiliwa Zanzibar mwaka 2011.Picha na Mwinyi Sadallah 
Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi

Posted  Ijumaa,Septemba13  2013  saa 10:50 AM
Kwa ufupi
Mkurugenzi wa ZMA,Mhandisi Abdi Omar Maalim alithibitisha kuwa CAG wa Zanzibar tayari ameanza kufanya kazi ya ukaguzi ikiwamo kutuma watendaji wake katika ofisi za kampuni hiyo huko Dubai kwa minajili ya kuangalia mapato na SMZ jinsi ilivyoweza kunufaika kutokana na mgao wake wa asilimia 65.


Zanzibar. Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali Zanzibar (CAG),ameanza kuzifanyia ukaguzi wa hesabu Kampuni ya Philtex inayosajili meli kama wakala nchini Dubai,pamoja na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini(ZMA) kuanzia Agosti mwaka huu.
Mwananchi imebaini kuwa ukaguzi huo wa mapato na matumizi ya meli za kigeni zinazosajiliwa nje umekuja baada ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Julai mwaka huu kulalamika kuwa ZMA imekuwa hainufaiki na mapato hayo tangu Philtex ianze kusajili meli mwaka 2007.
Mkurugenzi wa ZMA,Mhandisi Abdi Omar Maalim alithibitisha kuwa CAG wa Zanzibar tayari ameanza kufanya kazi ya ukaguzi ikiwamo kutuma watendaji wake katika ofisi za kampuni hiyo huko Dubai kwa minajili ya kuangalia mapato na SMZ jinsi ilivyoweza kunufaika kutokana na mgao wake wa asilimia 65.
 Alisema kuna watendaji wa Philtex ambao walikuwa wakileta fedha hizo kwenye vikapu na kumkabidhi aliyekuwa mrajisi wa meli na mhasibu wake ambao baadaye walikuwa wakiziingiza katika akiba maalumu ya Hazina Zanzibar.
“Aprili mwaka huu kwa mara ya kwanza ndiyo Mamlaka yetu  imeanza kupokea fedha za mapato ya usajili wa meli,huko nyuma  zilikuwa zikiingizwa moja kwa moja hazina,”alisema Mhandisi Abdi.
Alisema utaratibu huo wa uwasilishaji wa fedha kwa njia zisizo za kawaida uliweza kuibua wasiwasi na kupendekezwa na Kamati ya Hesabu za Serikali na Mashirika ya Umma ya Baraza la Wawakilishi(PAC), kupendekeza Mkaguzi wa Hesabu afanye uchunguzi wa mapato na matumizi.
 ”CAG amefanya ukaguzi wa hesabu wa awali huko Dubai,atarudi  kukamilisha kazi hiyo,kwa upande wetu wametukagua  kwa siku tatu na kukamilisha kazi yao juzi,walikuwa wakifuatiliana na kuhakiki mapato na matumizi,”alisema Mhandisi Abdi.
SOURCE: MWANANCHI