Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Septemba14 2013 saa 6:59 AM
Posted Septemba14 2013 saa 6:59 AM
Kwa ufupi
Katika majaribio ya chanjo hiyo, wanasayansi hao
wameelezea kuwa imeonyesha mafanikio kwa kuangamiza kabisa virusi
wanaofanana na VVU kwa nyani.
Washington. Wanasayansi nchini Marekani
wamegundua chanjo ambayo wanaamini itaweza kuangamiza Virusi Vya Ukimwi
(VVU) kwa binadamu.
Katika majaribio ya chanjo hiyo, wanasayansi hao
wameelezea kuwa imeonyesha mafanikio kwa kuangamiza kabisa virusi
wanaofanana na VVU kwa nyani.
Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC)
limechapisha kwenye tovuti yake kuwa baada ya kubaini hilo sasa
wamekusudia kufanya majaribio ya chanjo hiyo kwa binadamu.
Likinukuu taarifa iliyochapishwa kwenye jarida la
kisayansi linaloitwa; Nature, lilimnukuu Mwanasayansi wa Chuo Kikuu cha
Sayansi ya Tiba cha Oregon, nchini Marekani akisema walijiridhisha kuwa
chanjo hiyo iliangamiza virusi vyote kwenye mwili wa nyani.
Virusi hao jamii yake inafanana sana na VVU
wanajulikana kama Simian Immunodeficiency Virus (SIV) ikiwa na maana ni
virusi vinavyosababisha upungufu wa kinga ya kujikinga na maradhi kwa
nyani.
Taarifa za kisayansi zinaonyesha kwamba SIV ni
virusi ambao wamekuwa wakienea kwa njia ya kujamiiana miongoni mwa
vizazi vya nyani na vilibadilika baada ya kuambukizwa kwa binadamu
vikawa vimezaa VVU.
Wanasayansi hao wanasema kati ya nyani 16
waliopewa chanjo hiyo, waliyoipa jina la Cytomegalovirus (CMV),tisa
walipona kabisa maradhi ya SIV.
Mtaalamu wa Taasisi ya Chanjo na Jeni katika Chuo
Kikuu cha Oregoni, ambaye alihusika kwenye utafiti huo, Profesa Louis
Picker aliielezea chanjo hiyo kuwa ni ya kutia moyo ukilinganisha na
nyingine ambazo zimewahi kufanyika.
“Katika chanjo nyingi ambazo ziliwahi kuonyesha
mafanikio ya kuangamiza virusi ni kwamba kuna baadhi ya seli virusi
walibakia,” alisema Profesa Picker, akifafanua:
“Lakini kwa chanjo hii tulichunguza sehemu nyingi nyeti katika mwili wa nyani tukagundua kwamba hakuna kirusi aliyebakia.”
Alisema chanjo yao wameiamini kutokana na uwezo
wake wa kupenya maeneo mbalimbali ya mwili kiasi kwamba siyo rahisi
kirusi kubakia.
Wanasayansi hao walisema kwa kawaida nyani ambaye ameambukizwa SIV hufa ndani ya kipindi cha miaka miwili.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI