Saturday 14 September 2013

TUWAOMBEE: Wabunge Cheyo, Max walazwa



Mbunge wa Bariadi Magharibi, John Momose Cheyo (UDP) 
Na Kalunde Jamal, Mwananchi

Posted  Septemba14  2013  saa 6:54 AM
Kwa ufupi
Wabunge hao ni Donald Maxi wa Jimbo la Geita (CCM) aliyelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili (MOI), alikofanyiwa upasuaji ambao hata hivyo bado haujawekwa wazi.


Dar es Salaam. Wabunge wawili wakongwe kwenye Bunge la Tanzania wanaendelea na matibabu, kutokana na maradhi yanayowasumbua.
Wabunge hao ni Donald Maxi wa Jimbo la Geita (CCM) aliyelazwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Hospitali ya Muhimbili (MOI), alikofanyiwa upasuaji ambao hata hivyo bado haujawekwa wazi.
Mwingine ni Mbunge wa Bariadi Magharibi, John Momose Cheyo (UDP), aliyeelezwa yuko India kwa matibabu.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema jana kwamba wanatambua kuwa mbunge Max amefanyiwa upasuaji na amelazwa MOI, ambako anaendelea kuwa chini ya uangalizi wa madaktari.
Japokuwa hakutaka kutaja ugonjwa unaomsumbua mbunge Max, Dk Kashililah alisema kwamba ofisi yake inaendelea kufuatilia kwa karibu taarifa za maendeleao yake, na taarifa zaidi zinaweza kupatikana kwa wanafamilia na madaktari wanaomtibu.
Akizungumzia maendeleo ya hali ya afya ya mbunge Cheyo ambaye pia kuna taarifa kwamba bado anasumbuliwa na ugonjwa wa kiharusi, alisema kwamba ofisi yake inaendelea kufuatilia taarifa za kitabibu na maendeleo yake kutoka hospitali anayotibiwa India.
“Bado tunaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo yake tangu tulipoidhinisha apelekwe India, mwanzoni mwa mwezi uliopita. Hata hivyo madaktari wamesema anaendelea vizuri,” alisema Kashililah.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa MOI, Jumaa Almas alisema Mbunge Max, amelazwa hospitalini hapo akiwa kwenye chumba cha uangalizi maalumu.
SOURCE: MWANANCHI