Posted Septemba14 2013 saa 6:46 AM
Kwa ufupi
Samaki hao kutoka Yemen, Dubai, China na Japan,
wanaoingizwa nchini wakiwa wameganda kwenye barafu, wengi huharibika
muda mfupi baada ya barafu kuyeyuka au baada ya kununuliwa.
Dar es Salaam. Afya za Watanzania ziko shakani
kutokana na kuwapo kwa biashara ya kuingiza samaki kutoka nje ya nchi,
wanaodaiwa kuharibika na kuuzwa katika la Soko la Feri jijini Dar es
Salaam.
Samaki hao kutoka Yemen, Dubai, China na Japan,
wanaoingizwa nchini wakiwa wameganda kwenye barafu, wengi huharibika
muda mfupi baada ya barafu kuyeyuka au baada ya kununuliwa.
Uchunguzi wa gazeti hili umegundua kuwa samaki hao
huletwa nchini kutafutiwa soko baada ya kukaa kwenye majokofu kwa muda
mrefu huko wanakotoka, kiasi cha kuelekea kuharibika.
Ili wasiharibike, samaki hao aina ya Marckerel
hukaangwa hadi wakauke. Uchunguzi zaidi umebaini kuwa wanunuzi wake
wakuu ni wafanyabiashara wa chakula wakiwamo wamiliki wa migahawa na
Mama Lishe wanaofanya shughuli zao katika miji ya Dar es Salaam, Pwani,
Morogoro na Dodoma.
Samaki hao wanauzwa kwa bei ya chini ambayo ni
Sh38,000 kwa boksi lenye uzito wa kilo 15, ikilinganishwa na wanaovuliwa
hapa nchini ambao bei yake ni Sh60,000, kwa uzito huohuo.
Inaelezwa kuwa samaki hao baadhi yake ni wale
ambao wamekwisha muda wake wa kutumika katika nchi hizo, hivyo kuingizwa
nchini kutafutiwa soko.
Gazeti hili lilifika katika soko hilo kwa siku
mbili na kushuhudia samaki hao wakiuzwa kwa wingi, huku wauzaji
wakihimizwa wateja wao kuwahi kuwakaanga au kuwaweka kwenye jokofu.
Gazeti hili pia lilinunua boksi moja la samaki hao
lenye uzito wa kilo 15 kwa Sh38,000, lakini lilipodai kupewa stakabadhi
wauzaji walisema: “Hatuna stakabadhi ya kukupa ndugu yangu,” alisema
muuzaji.
Baada ya kuwasafirisha kutoka Soko la Feri hadi
ofisi za gazeti hili zilizopo Tabata Reli, Barabara ya Mandela kwa muda
wa saa moja, tayari walikuwa wameharibika.
Baadhi ya samaki hao walianza kuoza huku wengine
wakiwa wamelegea tofauti na samaki wa kawaida. Baada ya saa nne kupita,
samaki hao waliharibika na kuanza kutoa harufu mbaya.
Dk Raymond Mwenekano wa Hospitali ya Taifa ya
Muhimbili, anayataja madhara ya ulaji wa samaki wa aina hiyo kuwa ni
kupata magonjwa kama vile kansa ya utumbo, mwili kuwasha, kubabuka na
vidonda mwilini.
“Madhara yake ni makubwa, ndiyo maana siku zote
tunasisitiza kula vyakula visivyokaa sana kwani vingine vimehifadhiwa
kwa dawa na wanaofanya hivi ni wafanyabiashara kwa faida yao,” alisema
Dk Mwenekano.
Daktari huyo alisema pia yapo madhara ya muda mfupi ambayo ni
mtu aliyekula samaki wa aina hiyo kuharisha na kutapika muda mfupi baada
ya kula.
Mamlaka husika
Ofisa Afya katika Soko la Feri, Barnabas Hanje
alithibitisha kuwepo katika soko hilo, samaki wabovu wanaotoka nje ya
nchi na kwamba ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko mengi kuhusu suala
hilo.
Hanje ambaye pia alitajwa kuwa ni Mwakilishi wa
Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) katika soko hilo, alisema
kesi zinawahusu wanunuzi wanaodai warejeshewe fedha au kubadilishiwa
samaki, baada ya wale waliowanunua kuharibika haraka hata kabla
hawajatoka sokoni hapo.
Alifafanua kuwa baadhi ya kesi hupata ufumbuzi
baada ya waliouza samaki wabovu kukubali kurejesha fedha kwa wahusika na
kwamba kwa pale mwagizaji wa jumla anapokataa kurejesha fedha kesi hizo
hupelekwa mahakamani.
“Sina idadi kamili ya kesi, lakini kesi kama hizo
ni nyingi na baadhi yake tuliposhindwa kuwapatanisha watu wawili mnunuzi
na muuzaji tuliwaambia waende mahakamani, lakini nakiri ni kweli jambo
kama hilo lipo,” alisema Hanje.
Ofisa Uvuvi wa Manispaa ya Ilala, Msongo Songoro
alisema wamekuwa wakipata changamoto nyingi kuhusiana na suala hilo
ndiyo maana wameanza mchakato wa kutambua kampuni zote zinazoingiza
katika Soko la Feri samaki kutoka nje ya nchi.
Alisema hadi sasa wamebaini kuwapo kwa kampuni 20
na kati ya hizo ni sita pekee ambazo zimewasilisha uthibitisho wa
kufuata sheria pale wanapoingiza shehena ya samaki nchini. Songoro
aliongeza kuwa karibu tani moja na nusu ya samaki hao kutoka nje
wanauzwa kila siku katika Soko la Feri.
“Niliwahi kupata kesi kama hizo ambapo
nilichukulia kama changamoto na kuanza kufanya hiki ninachokifanya sasa
na hadi sasa ni kampuni sita pekee ambazo wameniletea vibali vyao
vinavyoonyesha uhalali wa kuagiza shehena ya samaki kutoka nje kati ya
kampuni 20 ambazo zinaagiza,”alisema Songoro.
Songoro alivitaja vitu ambavyo kila kampuni
inatakiwa kuviwasilisha kwao kuwa ni pamoja na Cheti cha Shirika la
Viwango Tanzania (TBS), Cheti cha Usajili wa kampuni, Cheti cha TFDA,
leseni ya biashara na vibali vyote vinavyoruhusu kuingiza samaki nchini.
Ofisa Maliasili wa Manispaa ya Ilala, Charles
Seche, alisema hatua walizochukua ni mwanzo lakini lengo ni kuondosha
bidhaa zote zisizo na ubora katika soko hilo.
Ofisa Uhusiano wa TFDA, Gaudencia Simwanza
alipoulizwa alisema hafahamu kuhusu uwepo wa samaki wabovu na kuahidi
kwamba angekwenda kulijadili na wahusika.
Alimtaka mwandishi wa habari amwambie samaki hao wameanza
kuingia lini nchini, wanatoka nchini gani na wanaitwaje, ili aweze
kuwasiliana na wahusika wa idara ya chakula.
“Wewe ndiyo unaniambia nitaiwasilisha kwenye idara
ya wahusika wa chakula moja kwa moja waifanyie kazi na baada ya
kukamilisha uchunguzi nitakupa taarifa,” alisema Simwanza.
Alipohojiwa baada siku moja, Simwanza alisema
jukumu la TFDA ni kuangalia mzigo ambao unaingizwa kwa wingi na hii ni
baada ya kupokea sampuli na kuridhishwa nao, kisha hutoa kibali kwa
ajili ya kuruhusu uingizwe.
“Kazi yetu sisi ni hiyo kwa mzigo uliopo sokoni
hasa wa vyakula muhusika mkuu ambaye tunafanya naye kazi kwa karibu ni
ofisa afya wa soko ambaye ndiye ana wajibu wa kukagua mzigo na kuangalia
una tatizo gani,”alisema Simwanza.
Simwanza alifafanua kuwa hata wanapotoa kibali cha
kuingiza mzigo siyo mwisho, kwani unapowasili huwa unafanyiwa ukaguzi
mwingine uwapo bandarini na ukigundulika una matatizo unazuiliwa.
Samaki bado wapo
Hata hivyo, uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa
pamoja na kufanya ukaguzi, samaki wasiofaa wanaendelea kuingizwa katika
soko hilo.
Mmoja wa wachuuzi wa samaki katika soko hilo
(ambaye hakupenda kutaja jina lake gazetini), aliliambia gazeti hili
kuwa samaki hao huuzwa kwa bei ya chini ikilinganishwa na wanaovuliwa
nchini.
“Siyo bure, huwezi kusafirisha samaki kutoka
Uarabuni kuja kuuza nchini kwa bei ya chini, je wewe unanunua kwa bei
gani?” alihoji na kusema ndiyo maana wengi wa samaki hawa wameharibika.
Alisema kama Serikali haitakuwa makini basi
Watanzania wanaweza kujikuta wanapata magonjwa mengi kutokana na
kugeuzwa dampo la vyakula visivyofaa.
Uchunguzi unaonyesha kuwa baada ya kuingizwa
nchini shehena ya samaki hao wakiwa katika makontena ya barafu,
hupelekwa kuuzwa katika soko hilo wakiwa wamehifadhiwa kwenye chumba cha
barafu.
Baadhi ya wateja wanapowatoa katika makasha
waliyofungiwa na kuwaosha, huharibika kabla hawajafika nyumbani. Baadhi
ya wachuuzi wanasema samaki hao hukosa soko kipindi ambacho samaki
wanakuwa wakipatikana kwa wingi wa nchini.
Mmoja wa wachuuzi hao, Hamisi Ally alisema,
“Niliwahi kupata taabu niliponunua samaki hao ili nikauze, maana wakati
nagawana na mwenzangu walikuwa wanatoa harufu kali na tulipowachunguza
walikuwa wameharibika kabisa.”
Mwingine ni Mwajuma Jumbe ambaye alisema, aliwahi
kupata bahati mbaya ya kununua samaki hao bila kujua na alipowauza
alipata malalamiko kutoka kwa wateja wake ambao walisema amewauzia
makapi kwa maana ya samaki kukosa ladha.
“Mm! bora nisote ninunue kidogokidogo hadi nijaze
ndoo kuliko kununua hao ‘kamongo’, waliwahi kukata msingi (mtaji) wangu
maana nilinunua na baada ya muda wakaharibika. Hao samaki wanataka
uwaandae wakiwa na barafu. Naona shida kununua kitu halafu kinipeleke
puta,” alisema Jumbe.
Mmoja wa wavuvi wa soko la Feri, Juma Abdul (siyo
jina lake halisi) alisema samaki hao hununuliwa na wachuuzi kutoka
maeneo mbalimbali ya jiji kwa kuwa bei yake ni ya chini, ikilinganishwa
na samaki wengine.
“Ukitaka kutambua hilo njoo asubuhi utashuhudia
kila kitu, samaki hawa si salama na wapo wavuvi ambao wamefikisha
malalamiko yao kwa uongozi wa soko,” alisema.
Alisema kuwa samaki hao mbali na kuharibika ndani
ya muda mfupi, ukiwala wanakuwa hawana ladha halisi ya samaki na kwamba
ili uwauze kiurahisi ni lazima uwakaange wakauke sana.
Waagizaji wa samaki
Kampuni moja ambayo inaingiza samaki hao kutoka
nje ya nchi ni Alpha Crust, ambayo Ofisa wake wa Rasilimaliwatu, Elton
Kachele alisema hawajawahi kupata malalamiko ya samaki kuharibika muda
mfupi baada ya kununuliwa.
Kachele alisema kuna uwezekano samaki huharibika
kutokana na jinsi wanavyohifadhiwa baada ya kutoka mikononi mwao, kwani
wao huwahifadhi vizuri na kwamba hata samaki wa kawaida kama hakutunzwa
vizuri huharibika.
Kachele aliongeza kuwa samaki wao kabla ya kuingia
sokoni hupita katika Mamlaka husika ikiwamo TFDA na TBS, ili
kuthibitisha kama wanaweza kuingia sokoni na kuliwa.
“Hata mwaka jana tulipata msukosuko baada ya
kuwepo kwa shutuma kama hizo na Wizara ya Afya pamoja na TFDA, walikuja
hapa kukagua na wakaona hakuna tatizo sasa kama bado linaendelea ni huko
nje lakini hapa kwetu kila kitu kipo safi,” alisema Kachele.
Alisema samaki wao wanaagizwa kutoka Yemen na
Japan, na baada ya kupata malalamiko hayo aliwahi kwenda hadi kwenye
Soko la Feri kuangalia kwenye vyumba vya kuhifadhia na kukuta kila kitu
kipo sawa.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo aliyejitambulisha kwa jina la
Vedagiri, alisema anachojua kabla ya kuuza samaki wanapitia kwenye
taratibu zote za Serikali ikiwemo ukaguzi wa kina kutoka kwa mamlaka
husika.
“Hao ambao wamepata samaki wabovu na wanaamini
wametoka kwangu walete ushahidi, lakini mimi ninachojua mamlaka husika
zimethibitisha kuwa wapo safi na ndiyo maana nauza na watu wanakula,”
alisema Vedagiri.
Juni, 2009 uongozi wa Soko la Feri ulikamata tani
moja ya samaki waliovuliwa kwa kutumia baruti ambao hawafai kwa matumizi
ya binadamu wakiwa wanauzwa sokoni hapo.
Agosti 2011,
Jeshi la polisi lilikamata tani 123.908 za samaki
aina ya Marckerel kutoka Japan zikituhumiwa kuwa zilikuwa na mionzi ya
nyuklia kutokana na nchi hiyo kupata ajali ya kinu cha nyuklia kuvuja.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliiagiza
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kufanya ukaguzi na kuhakikisha kuwa
samaki hao wanazuiliwa ili wasitumiwe.
Hata hivyo, baadaye TFDA ilitoa taarifa kuwa samaki hao hakuwa wamechafuliwa na mionzi ya nyuklia kutoka Japan.
Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk David
Mathayo David alipoulizwa kuhusu samaki hao wabovu alijibu kwa kifupi:
“Nipo njiani naendesha hivyo siwezi kulitolea ufafanuzi suala hilo.”
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Wizara hiyo,
Benedict Ngalama Ole-Nangoro, yeye alipoulizwa alimtaka mwandishi
ampelekee maswali kwa maandishi wayafanyie kazi na kuyatolea ufafanuzi.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI