Monday 23 September 2013

Wanaacha shule ili kufanya ukahaba


Pichani ni baadhi ya majengo ambayo yanadaiwa kutumika kwa ajili ya biashara ya ukahaba, katika eneo la Buguruni Madenge, jijini Dar es Salaam. 
Na Pamela Chilongola, Mwananchi

Posted  Jumatatu,Septemba23  2013  saa 11:19 AM
Kwa ufupi
Wananchi hawajui kwa nini viongozi wa Serikali wakiwemo  polisi wanashindwa kupiga marufuku biashara hiyo.

Dar es Salaam. Tatizo la ukahaba linaonekana kukua nchini, likiwemo Jiji la Dar es Salaam, kwa watu kufanya vitendo hivyo kwa staili tofauti.
Huku baadhi ya watu wakidaiwa kufanya ukahaba ofisini kwa kuvaa mavazi yasiyo na staha, kwa lengo la kuwawinda wanaume, baadhi yao wanajiuza waziwazi mitaani hasa nyakati za usiku, achilia mbali wale wanaojiuza mchana kwa kusimamisha watu na kujifanya wanaomba msaada au lifti za magari kisha anaomba namba ya simu.
Ahadi nyingi zimetolewa na Serikali kuhusiana na kukomesha biashara hii chafu, bila mafanikio, huku swali kuu likiwa ni nani hasa wananunua makahaba?
Utafiti unaonyesha kuwa wanunuzi wakuu wa makahaba ni watu wenye hali ya wastani kimaisha, wakiwemo waume za watu, huku baadhi ya wale wanaojiuza ni wake za watu. Sababu kubwa ni migogoro katika ndoa, tabia tu za mtu mwenyewe kupenda ngono na matatizo mengine ya kiafya na kiuchumi.
Biashara haramu hadharani
Ni jambo la kushangaza, lakini ndicho kinachozungumzwa kwamba kuna madanguro yameanzishwa katika baadhi ya  mitaa ya jiji la Dar es Salaam, watu wazima pia wakiwemo watoto wanajiuza.
Madanguro hayo yaliyopo eneo la Buguruni Madenge imedaiwa kuwa ni chanzo cha watoto hasa wa kike kuacha shule na kujiingiza kwenye ukahaba.
Jumla ya madanguro 15 yenye vyumba 170 yapo eneo hilo la Buguruni Madenge, huku yakitishia kuharibu mwelekeo wa watoto wanaoishi jirani na madanguro hayo hasa baada ya kuonekana baadhi yao kujiingiza kwenye ukahaba. Wakazi wa eneo hilo sasa wameonya kwamba watachukua hatua za kuyafunga madanguro hayo, baada ya kile wanachosema kwamba Serikali ni kama haitaki kufanya hivyo.
Wametangaza kuwa kabla ya mwisho wa mwezi huu, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala ayafunge madanguro hayo,  asipofanya hivyo wataandamana kuelekea kwenye ofisi ya Kamanda huyo, huku wengine wakisisitiza kwamba watayafunga kwa nguvu.
Wananchi waandamana
Hivi karibuni baadhi ya wakazi wa eneo hilo waliandamana hadi kwenye ofisi ya Serikali ya mtaa wao huo,  wakiushutumu uongozi wa Serikali hiyo  kwa kushirikiana na baadhi ya Polisi, kwa kile walichodai  kwamba kuna mazingira kama vile wanapokea rushwa kutoka kwa wamiliki wa madanguro hayo ili yasifungwe.
“Sitaki kuamini kama  kweli Serikali au polisi hawajui kinachoendelea kwenye madanguro haya. Hata kama hawajui, kwanini tunapolalamika kwenye vyombo vya habari kama hivi hakuna hatua za maana zinazochukuliwa,” anahoji Thadei Hamdani.  

ITAENDELEA KESHO

SOURCE: MWANANCHI