Saturday 14 September 2013

WFP yajitoa kufadhili ugawaji ujilishe shuleni



Na Sharon Sauwa
Kwa ufupi
Tangu mwaka 2001 WFP imekuwa ikifadhili utoaji ujilishe na chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule hizo ili kupunguza idadi ya watoto wanaoacha shule na kuongeza ufaulu.


Dodoma. Mpango wa Chakula Duniani (WFP), umejitoa katika ufadhili wa uji wa lishe kwenye shule za msingi 1,167 zilizopo Mikoa ya Dodoma, Shinyanga, Singida, Simiyu, Manyara na Arusha.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili juzi, Mkuu wa Ofisi ya WFP Mkoa wa Dodoma, Nima Sitta alisema utaratibu huo umeachwa kwa wazazi.
Alisema WFP hivi sasa imejikita katika kuwawezesha watoto waliopo katika shule hizo kupata chakula cha mchana.
Tangu mwaka 2001 WFP imekuwa ikifadhili utoaji ujilishe na chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule hizo ili kupunguza idadi ya watoto wanaoacha shule na kuongeza ufaulu.
“Juzi nilitembelea baadhi ya shule Singida kuangalia jinsi wazazi walivyoweza kuanza kuchangia chakula kwa watoto wao, nikakuta wamefanya vizuri. Kuna shule wazazi wamechangia nafaka za uji hadi Julai mwakani,” alisema.
Hata hivyo, alisema bado Serikali haijaandaa mwongozo wa kuwezesha shule kujitegemea kwa chakula na kwamba mpango mkakati unaotumika ni ule wa WFP.
Katika matembezi ya mshikamano yaliyoandaliwa na WFP kwa ajili ya kuchangia chakula shuleni mwaka juzi, Serikali iliahidi kuanza kutoa chakula shuleni lakini hadi sasa hakuna mwongozo ulioandaliwa.
SOURCE: MWANANCHI