Kwa ufupi
Inadaiwa kuwa siku ya tukio askari huyo
alisimamisha gari la bosi huyo wa polisi ambaye alitii sheria na kabla
ya maelezo zaidi kutoka kwa askari huyo feki wa usalama barabarani, mkuu
huyo alijitambulisha kwa askari huyo.
Dar es Salaam. Siri imefichuka
ya jinsi gani mtu ambaye aliyejifanya askari wa Kikosi cha Usalama
Barabarani, James Juma Hussein (45), alivyokamatwa wakati akiwa
‘kazini’ eneo la Kinyerezi Mnara, Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa
wiki.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi na kuthibitishwa
na mmoja kati ya askari walioshiriki katika kumkamata zinabainisha kuwa
mtuhumiwa huyo ambaye anatarajiwa kupandishwa kizimbani leo (Jumatatu),
alitiwa mbaroni baada ya kulisimamisha gari binafsi la mmoja kati ya
makamishna wa polisi.
Inadaiwa kuwa siku ya tukio askari huyo
alisimamisha gari la bosi huyo wa polisi ambaye alitii sheria na kabla
ya maelezo zaidi kutoka kwa askari huyo feki wa usalama barabarani, mkuu
huyo alijitambulisha kwa askari huyo.
Askari huyo wa Kituo cha Stakishari alisema:
“Inapotokea askari mwenye cheo cha juu anapojitambulisha pengine kwa
kuwa hukumfahamu kabla, kinachofuata ni saluti kabla ya kumruhusu
kuendelea na safari lakini kitu hicho hakikufanyika hali ambayo
ilimfanya bosi huyo akasirike.
Kinaeleza chanzo hicho kuwa askari waliotumwa
kumfuatilia walipofika eneo hilo kwa ajili ya kumtambua na kumchukulia
hatua za kinidhamu kwa kosa alilofanya, waliposimamisha gari na kumuita
alitimua mbio kabla ya kutiwa mbaroni na kujifanya amepoteza fahamu mara
baada ya kumdaka.
Askari hao walimbeba na kumpandisha katika gari
‘defender’ hadi Kituo cha Polisi Stakishari ambako amefunguliwa jalada
la kujifanya askari wa usalama barabarani akijua kuwa si kweli na
atafikishwa mahakamani leo kujibu mashtaka yanayomkabili.
Maelezo yake Polisi
Askari huyo bandia ambaye amefunguliwa jalada
namba STK/RB/15305/2013, amedai katika maelezo yake kuwa kamba ya
filimbi na kizibao ni vya polisi isipokuwa vifungo cha kung’ara
havikuwa vya polisi .
Askari huyo alidai kuwa nguo nyeupe juu ya kofia
aliitengeneza kienyeji, wakati krauni, tepe za usajenti na mkanda ni vya
shemeji yake ambaye alikuwa polisi mkoani Tabora ambaye alimtaja kwa
jina moja la Shaaban. Mtuhumiwa huyo anasema katika maelezo yake hayo
kuwa alijiunga na Chuo cha Polisi Moshi mwaka 1990 kabla ya kutimuliwa
mwaka uliofuata kutokana na vitendo vya utovu wa nidhamu na alikuja
mjini hivi karibuni baada ya kufiwa na mtoto na mkewe na maisha kuwa
magumu huko Tabora.
Habari zaidi zinaeleza kuwa katika sare za trafiki
alizokutwa , ndani alivaa na nguo nyingine za kiraia ndani na
inadhaniwa kuwa huwa anaziweka nguo hizo katika mfuko na kuzivaa akifika
eneo la jirani na hapo alipoamua kuwa kituo chake cha kazi kuzivua hizo
za trafiki baada ya kukamilisha siku.
Polisi Kimara Matangini
Askari mmoja wa kituo kidogo cha Polisi Kimara
Matangini, ambako ndiko yaliko maskani yake alisema jana kuwa mtuhumiwa
aliletwa kituoni hapo juzi akiwa katika gari la polisi na hata askari wa
usalama barabarani waliokuwa kituoni hapo walishindwa kumtambua.
source: Mwananchi
source: Mwananchi