15th September 2013
Waziri
Mkuu Mstaafu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, amesema machifu,
watemi na wakuu wengine wa kimila wana nafasi kubwa katika kuzuia
mmomonyoko wa maadili kwenye jamii.
Akizungumza mjini Tabora jana wakati wa
sherehe ya kuadhimisha miaka 124 ya shujaa wa Unyanyembe, Chifu Isike
Mwana Kiyungi, Lowassa alisema wakuu hao wa kimila wakitumika wanaweza
kusaidia masuala mbalimbali katika jamii.
"Hawa machifu wanaweza kabisa kusaidia
tatizo hili, mimi kule kwetu Monduli ni Laigwanan mkuu...kuna wakati
hali ya maambukizi ya Ukimwi yalikuwa makubwa sana kwa wamasai, sasa
nikawaita malaigwanan wenzangu nikawaomba waondoe baadhi ya mila
zinazochangia hali ile, tukakubaliana na kupita kijiji kwa kijiji
kuelezea, na kweli ikaleta mafanikio makubwa sana maambukizi yale
yakapungua," alisema Lowassa.
Alipongeza hatua iliyofikiwa ya kuenzi
kumbukumbu hiyo na kusema kizazi cha sasa kina kila sababu ya kuiga
mfano wa Chifu Isike wa kutetea utu wake.
"Chifu Isike alisimama imara kutetea utu
wake dhidi ya wakoloni, alionesha ushupavu, sasa kizazi hiki ni lazima
kiige mfano huu wa kutetea utu wa Mtanzania dhidi ya wadhalilishaji,"
alisema Lowassa.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika kijiji
cha Itetemia ambako ndiko iliko Ikulu ya chifu huyo wa Unyanyembe,
aliyepigana dhidi ya majeshi ya Mjerumani Von Prince (Mwana sakaraga)
kuanzia mwaka 1889 hadi 1893.
Lowassa aliwataka wakazi wa Tabora kuwekeza mji wao kitalii kutokana na historia kubwa ya mkoa huo.
"Tabora ina historia kubwa sana katika
uhuru wa nchi yetu, viongozi wengi nikiwemo mimi tumesoma hapa, neno
ikulu asili yake ni hapa tulipo, ikulu ya chifu Isike, chama changu
wakati huo TANU kina historia na mjini huu, sasa hivi vitu ni utalii
tosha, kwa hivyo naunga sana mkono hatua ya kujenga mnara wa kumbukumbu
ya chifu Isike, muitangaze ili kupata watalii wa nje na ndani," alisema.
Mapema Lowassa ambaye alikuwa mgeni rasmi
katika maadhimisho hayo alitawazwa kuwa Chifu wa Nyanyembe na kuteuliwa
kuwa mlezi wa watemi wote wa Unyanyembe. Aliweka jike la msingi la
ujenzi wa mnara wa kumbukumbu ya shujaa huyo.
Sherehe hizo zilihudhuriwa na machifu na
watemi kutoka makabila mbalimbali, pamoja na watu wengine mashuhuri
katika kabila la kinyamwezi.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI