Monday 23 September 2013

Rais JK amempa pole rais Uhuru Kenyatta kufuatia shambulio la kigaidi.

 Rais  Jakaya  Kikwete amezungumza kwa simu na rais Uhuru Kenyatta wa Kenya na kumpa pole na kutaka kujua jinsi gani Tanzania inaweza kusaidia kufuatia shambulio la kigaidi kwenye kituo cha biashara cha Westgate katika eneo la Westlands, Nairobi, ambako watu 62 wameuawa na wengine 175 wamejeruhiwa.
 
Rais Kikwete alimpigia simu rais Kenyatta  jioni ya Jumamosi  kutokea mjini New York, marekani, mara baada ya kuwasili mjini humo akitokea Toronto, canada, ambako alifanya ziara ya kikazi ya siku tatu. Katika mazungumzo kati ya viongozi hao, rais Kikwete amemweleza rais Kenyatta mshtuko na hasira yake kutokana na taarifa za kusikitisha za shambulio hilo la kigaidi .
 
Rais Kikwete amefuatilia mazungumzo hayo kwa salamu rasmi za rambirambi ambazo rais Kikwete amemtumia rais Kenyatta akielezea masikitiko na hasira yake kufuatia mauaji hayo ya watu wasiokuwa na hatia akitaka kujua jinsi Tanzania inaweza kusaidia juhudi za serikali ya Kenya katika kukabiliana na madhara ya tukio hilo na balaa la ugaidi kwa jumla.
 
Katika salamu zake rais Kikwete amesema shambulio hili linalenga kuitisha serikali na wananchi hodari wa Kenya na kudhoofisha nia yao ya kutimiza wajibu wao wa kihistoria wa kuunga mkono jitihada za kuleta amani katika nchi jirani na yenye matatizo ya Somalia. Rais amesema kwa maana hiyo, shambulio hilo la woga na lisilo na huruma kabisa dhidi ya watu wasiokuwa na hatia, lazima lilaaniwe na kushutumiwa vikali na wapenda amani wote.
 
Amesema serikali na wananchi wa jamhuri ya muungano wa Tanzania wanasimama bega kwa bega na kaka na dada zao wa Kenya katika kipindi hiki kigumu. Aidha, serikali ya Tanzania inapenda kuihakikishia serikali ya Kenya itaendelea kuiunga mkono na kushirikiana nayo katika kupambana na balaa la ugaidi katika sura zake zote.
 
SOURCE: ITV-DAIMA