Kwa ufupi
Upande wa barabara nako kuna matatizo yake
lukuki, imaelezwa kuwa barabara za Tanzania zina vizuizi vingi kiasi cha
kuwakwaza wasafirishaji wa mizigo wa ndani na nje ya nchi.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa takwimu
za hali ya uchumi katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu
inayohusisha mwezi Januari na Machi.
Kwa mujibu wa takwimu hizo pato la taifa(GDP)
limepanda kwa asilimia 7.5 kiwango ambacho ni kikubwa kuliko viwango
vingine vya kipindi kama hicho tangu mwaka 2009.
NBS inasema sekta zote za uzalishaji zimefanya
vizuri kiuchumi katika kipindi hicho cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka
huu na pato hilo limefikia Sh4.5 trilioni.
Miongoni mwa sekta hizo ni sekta ya uchukuzi na
mawasiliano ambayo kasi ya ukuaji wake ilifikia asilimia 22.2.
Mkurugenzi wa uchumi wa NBS, Morrice Oyuke anasema huduma ya usafiri wa
treni jijini Dar es Salaam, maarufu kama treni ya Mwakyembe imechangia
kupanda kwa pato katika sekta ya uchukuzi.
Pamoja na habari hizo kwa sekta hiyo ambayo mbali
na reli pia inahusisha anga, barabara na maji upande wa pili wa sarafu
kwa sasa umegubikwa na hali ya shaka.
Pamoja na sekta ya reli kufanya vizuri, lakini
hivi karibuni mgomo wa wafanyakazi wa Shirika la Reli la Tanzania na
Zambia (Tazara), umeleta athari kwani matatizo ya Tazara yamekuwa ya
muda mrefu na jitihada zinazochukuliwa hazionekani kutoa tiba ya kudumu.
Matatizo haya yanapoendelea yanazorotesha hali ya uchumi.
Kwa upande wa anga, siku za hivi karibuni Uwanja
wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) umekuwa njia ya kusafirishia dawa za
kulevya kiasi cha kutia aibu kwani vitendo hivyo havifanani kabisa na
jina lenyewe.
‘Unga’ unapitishwa uwanjani hapo huku wahusika
wakiwa ‘wamelala’ mpaka Waziri wa Uchukuzi Dk Harrison Mwakyembe
alipoingilia kati na kuanza kusafisha.
Nakumbuka Waziri Mwakyembe alisema katika moja ya
mikutano yake kuwa aibu hiyo inasababisha Watanzania wasiaminiwe
wanaposafiri kwenda mataifa mengine kwa kuhisiwa watakuwa wamebeba unga.
Naunga mkono hatua alizoanza kuchukua dhidi wote wanaohusika na uchafu
huo.
Upande wa barabara nako kuna matatizo yake lukuki,
imaelezwa kuwa barabara za Tanzania zina vizuizi vingi kiasi cha
kuwakwaza wasafirishaji wa mizigo wa ndani na nje ya nchi. Kwa mfano,
kuna mizani nane kutoka Dar es Salaam hadi Rusumo ulipo mpaka kati ya
Tanzania na Rwanda.
Si mizani tu bali na vizuizi vingine vingi vya
ukaguzi wa magari yanapokuwa safarini, hali hii inasababisha nchi za
Uganda na Rwanda kutaka kujitoa kutumia Bandari ya Dar es Salaam kwa
sababau ya vizuizi vingi vinavyochelewesha mizigo yao. Madereva
wanaofanya safari hizo wanasema kuna wakati wanakaa kwenye foleni kwa
saa tatu katika mzani mmoja, mpaka amalize mizani zote atakuwa amepoteza
muda kiasi gani?
Bandari ya Dar es Salaam inalalmikiwa kwa ucheleweshaji wa
mizigo huku pia ufanisi wake ukiwa mdogo. Utafiti uliofanywa na mtandao
unaojihusisha na ukaguzi wa hesabu KMPG na Benki ya Dunia (WB)
unaonyesha kwamba mwezi Mei na Juni 2012, meli za kontena zilikuwa
zinapanga foleni kwa wastani wa siku 10 zikisubiri gati katika Bandari
ya Dar es Salaam, wakati muda wa kusubiri ulikuwa chini ya siku moja
katika Bandari ya Mombasa. Msafirishaji gani anaweza kuvumilia hali hii?
Kwa nini tusifanye mambo kisasa? Tunapoteza fursa
kwa sababu ya uzembe. Foleni bandarini, foleni barabarani ukienda uwanja
wa ndege unakutana na unga yote haya Tanzania. Kwa nini?
0715 221918.
source: Mwananchi
source: Mwananchi