Na Waandishi Wetu
Posted Alhamisi,Septemba26 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Septemba26 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Gazeti limebainisha jinsi mpango mzima wa kupanga shambulizi hilo ulivyoratibiwa.
Dar es Salaam. Maandalizi ya kushambulia jengo la maduka la eneo la Westgate, Nairobi yalifanyika kwa miezi mingi.
Gazeti la New York Times la Marekani lilikariri
vyanzo vyake ndani ya vyombo vya usalama vya nchi hiyo jana vilivyosema
kuwa mipango na mazoezi kwa ajili ya shambulizi hilo vilifanyika
Somalia.
Magaidi kati ya 10 hadi 15 wa Al-Shabaab walivamia
kwa silaha kwenye jengo la ghorofa nne la maduka na kusababisha vifo
vya watu 67 kwa mujibu wa taarifa za Serikali ya Kenya na majeruhi 175.
Magaidi watano walipoteza maisha kwenye tukio hilo.
Kitengo cha Mambo ya Nje cha Kundi la Al-Shabaab ndicho kilichokuwa na kazi ya kupanga shambulizi hilo.
Imeelezwa kuwa watekelezaji wa tukio la kigaidi
walipitia mafunzo maalumu huko Somalia yaliyowawezesha kubaini michoro
ya jengo pamoja na mbinu za kusafirisha silaha.
Utekelezaji
Gazeti hilo lilidai kuwa uratibu wa operesheni
hiyo ulifanywa kwa uangalifu kwani wafuasi wa Al-Shabaab waliochaguliwa
ni wale ambao walikuwa wanafahamu vyema Kiingereza na wenye uzoefu wa
masuala ya kimataifa.
“Hawa jamaa pia waliandaa mchoro wa jengo hilo.
Wakaandaa mkakati wa kupenyeza silaha ambazo walikuwa wamezileta kutoka
Somalia,” kilisema chanzo cha gazeti hilo.
Gazeti la New York Times, lilisema silaha
zilizotumika kwenye uvamizi huo zilipenyezwa kupitia maeneo yalikuwa
yakilindwa na askari wa kampuni binafsi za ulinzi.
Duru za usalama za Marekani zimeeleza kuwa kuna
uwezekano mkubwa kuwa baadhi ya askari walihongwa kutokana na kukabiliwa
na ukata wa kutolipwa kwa wakati na waajiri wao.
Taarifa zinasema kuwa siku moja au mbili kabla ya
uvamizi huo, inasemekana magaidi hao walipitisha kwa siri mikanda ya
risasi kwa ajili ya kutumika kwenye bunduki zao aina ya `Short Machine
Gun’ (SMG).
Baadhi ya wafanyakazi wa jengo hilo wanadaiwa kula
njama na magaidi hao ili kufanikisha mpango wa kuingizwa kwa silaha
hizo zilizotumika kwenye ugaidi.
Taarifa zaidi zinasema kuwa mmoja wa magaidi hao alikuwa amebeba
nguo za kubadilisha ambazo angezitumia na wenzake kwa ajili ya kutoka
nje ya jengo hilo pamoja na raia wakati wa kukimbia baada ya kufanya
mauaji. Serikali ya Kenya imetoa orodha ya washukiwa wa shambulizi hilo
wanaotoka Marekani na Uingereza.
Rais Uhuru Kenyatta alisema taarifa za kiusalama
zimedokeza kuwa mashambulizi hayo yalitekelezwa na raia watatu kutoka
Marekani na mwanamke mmoja wa Uingereza.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani imesema imepokea
taarifa za kuhusika kwa raia wake, lakini imesisitiza kuwa bado haiwezi
kudhibitisha moja kwa moja mpaka pale itakapopata uhakika kwa njia ya
vipimo vya kinasaba (DNA).
“Tunafahamu yaliyotokea Kenya, lakini hatuwezi
kuthibitisha moja kwa moja kuhusika kwa raia wa Marekani, tunasubiri
vipimo vya DNA pamoja na baadhi ya picha za kwenye mitambo ya CCTV...
lakini tendo lililofanyika nchini Kenya ni la kinyama,” alisema ofisa
mmoja wa usalama wa Marekani ambaye hakutaka jina lake kutajwa
alipohojiwa na New York Times.
Serikali ya Kenya imesema imedhibiti eneo zima la
jengo na kuwaua baadhi ya magaidi hao ingawa nchi za Ulaya na Marekani
zinaona kwamba kuna uwezekano baadhi ya wavamizi walifanikiwa kutoroka
wakati wa kurushiana risasi.
SOURCE: MWANANCHI