Na Mwandishi Wetu
Posted Alhamisi,Septemba26 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Septemba26 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Wakati Kundi la Al-Shabaab likidai kuwa watu
137 wamekufa jana, Serikali ya Kenya imeeleza kuwa watu waliokufa ni 67
tangu shambulizi hilo lilipotokea Jumamosi iliyopita.
Nairobi. Hatua ya Kundi la Al-Shabaab la Somalia
kudai kwamba watu 137 lililokuwa limewateka waliuawa kwa silaha za sumu
juzi, imezidisha utata wa idadi ya vifo vilivyotokea baada ya
shambulizi la kigaidi lililofanyika Westgate, Nairobi, Jumamosi
iliyopita.
Taarifa iliyotolewa na kundi hilo kupitia kwenye
mtandao wa Twitter jana, ilidai kuwa mateka 137 waliokuwa wanashikiliwa
na wafuasi wao kwenye jengo la biashara la ghorofa nne, walifariki baada
ya kupuliziwa sumu na vikosi vya usalama vya Serikali ya Kenya.
Hata hivyo, Msemaji wa Serikali ya Kenya, Manoah Esipisu alikanusha vikali madai ya kundi hilo.
Ghorofa tatu kati ya nne za jengo hilo zilianguka jana lakini kumekuwa na utata wa idadi ya waliokuwamo ndani.
Esipisu alisisitiza kuwa kuta za jengo hilo
zilianguka baada ya magaidi hao wa Al-Shabaab kuchoma moto bidhaa za
maduka hayo. “Hawa jamaa walikusanya vitu vingi kwenye ghorofa ya tatu
na kuvichoma moto. Wingi wa vitu ulisababisha kuta na sakafu za ghorofa
zile kuzidiwa uzito.
“Kuta za ghorofa ya tatu zikaangukia ghorofa ya
pili. Kuta za ghorofa ya pili zikaangukia ile ya tatu ndiyo sababu kuu
ya hali hiyo... Al-Shabaab wanajulikana kwa propaganda zao, hakuna
ukweli wowote kuhusu habari hizo,” alisema Esipisu.
Kundi hilo la Al-Shabaab lilidai kupitia mtandao wa Twitter kuwa Serikali ilipuliza sumu kabla ya kuanza kubomoa jengo hilo.
Utata wa idadi ya waliokufa
Wakati Kundi la Al-Shabaab likidai kuwa watu 137
wamekufa jana, Serikali ya Kenya imeeleza kuwa watu waliokufa ni 67
tangu shambulizi hilo lilipotokea Jumamosi iliyopita.
Idadi kubwa ya waliofariki ni raia wa Kenya na
wageni 18 kutoka Ufaransa, Canada, Uholanzi, Australia, Peru, India,
Ghana, Afrika Kusini na China. Raia watano wa Marekani nao wamethibitika
kufariki dunia.
Kwa mujibu wa taarifa ya Serikali, watu 175 walijeruhiwa katika shambulizi hilo huku watu 60 wakiwa wamelazwa hospitalini.
Pamoja na watu hao, pia kuna magaidi watano waliouawa wakati wa operesheni hiyo.
Askari wanaendelea na operesheni ya kupekua eneo hilo ili kuona kama kuna uwezekano wa magaidi wengine kujificha.
Marekani, Israel na Uingereza zaongeza nguvu
Marekani, Uingereza na Israel zimeongeza mashushushu ili kusaidia uchunguzi wa tukio hilo.
Hiyo ni baada ya nchi hizo kuongeza maofisa wake
wa usalama ambao walishirikiana na vikosi vya usalama vya Kenya tangu,
Jumapili iliyopita.
Kazi ya kuondoa miili
Esipisu alisema pia kuwa vikosi vya usalama
vinajiandaa kuanza kazi ya kuondoa miili ya watu waliofariki dunia
kwenye jumba hilo.
“Kazi hii itaanza pale vikosi vyetu vitakapojiridhisha kuwa kuna hali ya usalama,” alisema Esipisu.
Kuna wasiwasi kuwa bado kuna magadi waliojificha
kwenye jumba hilo lililokuwa na maduka ya kampuni mbalimbali, migahawa
kadhaa, benki na jumba la michezo ya casino.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI