Na Mwinyi Sadallah
Posted Alhamisi,Septemba26 2013 saa 24:0 AM
Posted Alhamisi,Septemba26 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Ni kauli iliyotolewa wakati wa mkutano wa hadhara uliovishirikisha vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi
Waziri wa Sheria na Katiba Mathias Chikawe
ametakiwa ajiuzulu kwa kutoa taarifa za uongo kwamba Zanzibar
ilishirikishwa kabla ya Muswada wa Mabadiliko ya Katiba kuwasilishwa
bungeni na kupitishwa na Bunge Septemba mwaka huu.
Msimamo huo ulitolewa na Waziri wa Sheria na
Katiba Zanzibar, Aboubakary Khamis Bakari wakati akihutubia mkutano wa
hadhara uliovishirikishwa vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi
uliofanyika Uwanja wa Kibandamaiti mjini Unguja jana.
Aboubakari alisema kwamba Zanzibar ilipokea
taarifa ya awali ya mabadiliko kuhusu vifungu vinne vya Muswada wa
Mabadiliko ya Katiba na kutakiwa Zanzibar itoe maoni na mapendekezo
yake, jambo ambalo alisema lilifanyika kupitia Ofisi ya Makamu wa Pili
wa Rais Zanzibar na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Hata hivyo, alisema vifungu vya mabadiliko ghafla
viliongezwa kutoka vinne hadi 12 bila ya Zanzibar kupewa nafasi ya
kujadili vifungu vinane ambavyo vina umuhimu mkubwa katika kupata katiba
bora.
“Waziri nimesoma naye Chuo Kikuu mwaka 1972, Chikawe kwa hili amesema uongo vinginevyo ajiuzulu, hafai,” alisema Aboubakari.
Alisema kabla ya kufanyika Waziri akifuatana na
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Bunge, William
Lukuvi walifika Zanzibar na kutaka wajadili vifungu hivyo kwa siku moja
jambo ambalo alipinga kulitekeleza.
“Baada ya kuanza kupiga kelele, wenzetu walikuja
Zanzibar wakitaka tujadili mabadiliko ya mswada,nikawaambia siwezi
kujadili masilahi ya nchi kijuujuu, huko ni kuiuza nchi, siko tayari
kufanya hilo,” alisema.
Aboubakari alisema marekebisho yaliyofanyika
katika muswada huo na kutoa nafasi kujadili na kupitisha mabadiliko ya
Katiba kwa kutumia wingi wa kura ni sawa na wazimu.
Alisema mabadiliko yoyote ya Katiba yanapaswa
kutumia theluthi mbili toka pande mbili za Muungano, utaratibu ambao
ndiyo umekuwa ukitumika na nchi mbalimbali zenye mfumo kama wa Tanzania.
Mwananchi ilipomtafuta Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe
kujibu tuhuma hizo alisema Aboubakari ameudanganya umma mchana kweupe
kwa vile yeye na Waziri Lukuvi walifika Zanzibar kupeleka rasimu ya
muswada na si kujadili na kupokea mapendekezo papo kwa hapo.
Chikawe alisema kwamba walipokabidhi muswada pia
walimtaarifu siku ya kuwasilishwa muswada huo katika kikao cha Bunge na
kuwataka kutoa maoni na mapendekezo kwa wakati mwafaka kabla ya
kujadiliwa na kamati ya Katiba ya Sheria ya Bunge.
Alisema kwamba nyongeza ya marekebisho ya vifungu
vinane yalitokana na mapendekezo ya wabunge katika kamati na michango ya
wabunge ndani ya Bunge katika utaratibu unaoruhusiwa kisheria.
“Baada ya kamati ya Bunge kukaa, Mbunge Halima
Mdee wa Chadema ndiye aliyependekeza kutumika kwa utaratibu wa wingi wa
kura katika kupitisha mabadiliko hayo ya Katiba kama hatua ya theluthi
mbili itashindwa kufikia mwafaka,” alisema Chikawe.
SOURCE: MWANANCHI
Pia alisema mbunge kupitia Baraza la Wawakilishi, Jaku Hashim
Jaku yeye alitetea kwa nguvu ya hoja kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
imalize kazi yake baada ya kuwasilisha ripoti yake kwa Rais na kwamba
haikuwa ni uamuzi na matakwa ya Serikali kama inavyodaiwa na vyama vya
upinzani kuhusu nyongeza hiyo.
“Nyongeza ya vifungu ilitokana na wabunge katika
kamati na ndani ya Bunge lenyewe, Serikali haiwezi kupuuzia ushauri wa
wawakilishi wa wananchi na wabunge ambao wanaisimamia Serikali,” alisema
Waziri Chikawe.
Aidha, Aboubakari alimshutumu Naibu Spika wa
Bunge,Job Ndugai kwa kulidanganya Bunge kwa kitendo chake cha kutoa
barua ikithibitisha Zanzibar imeshiriki wakati kuna vifungu vya ziada
vimefanyiwa marekebisho bila ya kupata baraka ya Zanzibar.
Alisema kwa msingi huo amevunja na kukiuka kanuni
za Bunge na wabunge wana haki ya kumshtaki kwa kutumia kanuni zao kwa
kupotosha Bunge na umma.
Hata hivyo, taarifa hizo za Aboubakari kutokana na
maelezo aliyotoa awali Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad
kwenye mkutano wa hadhara, alisema Zanzibar ilishirikishwa katika
kuvifanyia vifungu sita na SMZ ilitoa mapendekezo katika vifungu vitatu
na baadae vikaongezwa vinane kinyemela bila ya Zanzibar kushirikishwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia alisema kwa muda mrefu viongozi wa Zanzibar walikuwa wakijitolea
kupigania mabadiliko ya taifa lao na kukutwa na vizingiti ikiwemo
kuwekwa vizuizini na kupewa hongo ya madaraka.
Mbatia alisema miongoni mwa viongozi waliojitoa
muhanga kutaka mabadiliko ya mfumo wa Muungano ni pamoja na Rais wa
Awamu ya Pili Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi ambaye aliondolewa kibabe
madarakani chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere.
Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alimtaka
Rais Jakaya Kikwete kumfuta kazi Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Frederick Werema na Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe kwa
madai kuwa hawana nia njema wakikusudia kuharibu nia njema ya Rais ya
kupata Katiba mpya.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba alisema
Katiba iliyopo sasa nchini haifai kwa kuwa imejaa upungufu unaokwenda
kinyume na misingi ya haki za raia.
SOURCE: MWANANCHI