Friday 6 September 2013

Sheikh Azzan atakiwa kutibiwa nje

                      
                                               Sheikh Azzan Khalid Hamadan 

Na Mwinyi Sadallah

Posted  Alhamisi,Septemba5  2013  saa 20:13 PM
Kwa ufupi
Kamishna wa Chuo cha Mafunzo (Magereza) Zanzibar, Khalifa Hassan alisema wamelazimika kuomba mwongozo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) ambaye kwa niaba ya Serikali ndiye aliyemfungulia mashtaka.


Zanzibar. Kiongozi Mwandamizi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumuki), Sheikh Azzan Khalid Hamadan, amebainika kuwa figo zake zina vijiwe na matibabu yake hayawezekani kufanyika Zanzibar, imefahamika.
Sheikh Azzan na wenzake tisa walifunguliwa mashtaka Oktoba mwaka jana, wakituhumiwa kufanya uharibifu wa mali na kusababisha hasara ya Sh500 milioni.
Pia wanatuhumiwa kuhatarisha usalama wa taifa kinyume na kifungu cha 3(4) sura ya 47 ya Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 2002.
Akizungumza na Mwananchi jana, daktari mmoja bingwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, alisema mawe yaliomo katika figo za Sheikh Azzan yamekuwa yakimsababishia maumivu na hakuna njia ya kuokoa maisha yake zaidi ya kusafirishwa nje ya nchi.
Hata hivyo daktari huyo hakutaka jina lake litajwe. Alisema vifaa kwa ajili ya tiba ya Sheikh huyo havipatikani Zanzibar wala Tanzania Bara na kwamba ni vya kisasa.
Kwa mujibu wa daktari huyo, tiba yake hufanyika kwa mgonjwa kuwekewa kifaa maalumu mgongoni kinachopitisha mawimbi yanayosaga mawe kwenye figo yaani Extracorporeal shock wave Lithrotripsy (ESWL).
Alisema baada ya mawe hayo kusagwa kwa kutumia mawimbi, chembechembe za vijiwe huhamia katika kibofu na baadaye kutoka kupitia njia ya mkojo.
Katibu wa Hospitali ya Mnazi Mmoja, Omar Abdallah Ali, alithibitisha mgonjwa kukabiliwa na matatizo ya figo na kwamba daktari anayemtibu atalazimika kuwasilisha ripoti yake kwa bodi.
Kamishna wa Chuo cha Mafunzo (Magereza) Zanzibar, Khalifa Hassan alisema wamelazimika kuomba mwongozo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP) ambaye kwa niaba ya Serikali ndiye aliyemfungulia mashtaka.
“Hatutaki kufanya mambo kinyume na utaratibu, kinachotakiwa ni kupata mwongozo kwanza ili kusitokee utata...taarifa ya Jamhuri ambayo ndiyo iliyomshtaki,” alisema.
“Kesi kama hii ni ya kwanza kutokea huku mahabusu wakiwa chini ya dhamana yetu, tumelazimika kuomba mwongozo kwa DPP kujua kama anaweza kutibiwa nje au la,” alisema Kamishna huyo.
Hata hivyo, DPP Ibrahim Mzee Ibrahim mara kadhaa alipopigiwa simu yake ilikuwa ikiita bila majibu hata baada ya kutumiwa ujumbe wa maneno, hakujibu hadi tunakwenda mitamboni.
Kwa muda mrefu tangu kukamatwa kama kiongozi huyo wa kikundi cha Uamsho, afya ya yake imekuwa ikizorota siku hata siku kutokana na kukabiliwa na matatizo hiyo ambayo sasa inaelezwa anatakiwa kusafirishwa nje kwa matibabu.

source: Mwananchi