Posted
Jumanne,Septemba10
2013
saa
22:8 PM
Kwa ufupi
Nikirejea walichosimama kidete kutetea, Mbunge
wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema ni lazima tutunge sheria
zinazolinda wazawa badala ya kuweka vipengele vinavyowapendelea
wawekezaji.
Wiki iliyopita tumeshuhudia mjadala mzito kuhusu
Muswada wa Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji wa mwaka 2013 uliowafanya
wabunge kuungana bila kujali tofauti za kisiasa, kutetea maslahi ya
nchi.
Matukio ya aina hii ni nadra kushuhudiwa katika Bunge letu katika miaka ya karibuni.
Mara nyingi tumeshuhudia baadhi ya wabunge wakiponda jambo fulani kwa sababu tu wakiliunga mkono litakipa chati chama fulani.
Nimetumia mfano wa mjadala wa muswada huo kwa siku
za usoni wabunge watapata fursa ya kujadili miswada miwili muhimu
katika mustakabali wa taifa letu ikiwamo wa Katiba Mpya.
Mmoja wa miswada hiyo ni ule wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2013 ambao
umepita licha ya kususiwa na wabunge wa upinzani. Ule wa Kura ya Maoni
uliondolewa.
Je, wabunge wetu wataweka kando tofauti zao za
kisiasa na misimamo ya kichama na kujadili muswada huo kwa maslahi ya
nchi kama walivyofanya katika ule wa Sheria ya Taifa ya Umwagiliaji?
Sababu ya kuhoji nitazieleza baadaye baada ya
kwanza kueleza walichokifanya wabunge wakati wa kujadili muswada
nilioutaja hapo juu. Hakika walionyesha uzalendo wa hali ya juu.
Kikubwa katika mjadala huo ni kwamba Bunge
lilipoketi kama kamati ya Bunge zima, walioongoza kuibana serikali
walikuwa ni wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Huu ni uzalendo.
Nasema walichoonyesha wabunge ambao waliungwa mkono na upinzani hakika
kilionyesha uzalendo na namna walivyojitoa kutetea maslahi ya
Watanzania.
Nikirejea muswada huo, baadhi ya vifungu
vilipendekeza pale ambapo eneo fulani limetamkwa ni la umwagiliaji, mtu
au watu wanaomiliki eneo hilo watalipwa fidia na kuondoka.
Nikirejea walichosimama kidete kutetea, Mbunge wa
Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema ni lazima tutunge sheria
zinazolinda wazawa badala ya kuweka vipengele vinavyowapendelea
wawekezaji.
Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM), “Huu msimamo wa kuwakumbatia wageni halafu wazawa hawanufaiki tunasema sasa basi.”
Bulaya ambaye mimi ni muumini wake mkubwa alienda
mbali na kudai, “Watanzania wameshindwa kunufaika na rasilimali nyingine
na wamebakia na ardhi…hatukubali tena.”
Kwa maneno mengine, Bulaya alitaka kufikisha ujumbe kuwa katika
maeneo ambayo kulikuwa na madini, wananchi waliondolewa ama kwa kulipwa
fidia kidogo ama kutolipwa kabisa.
Hata hivyo, kubwa zaidi wananchi wa maeneo hayo
hawanufaiki na uwekezaji katika migodi hiyo zaidi ya wageni kuwa ndio
wanufaika wakubwa huku wananchi wanaoishi jirani wakiwa mafukara.
Ndiyo maana Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM)na
yule wa Peramiho, Jenister Mhagama (CCM), wakasimama kidete wakitaka
sheria hiyo itamke wananchi watakaokutwa katika eneo linalotangazwa kuwa
la umwagiliaji kwanza wapewe hisa na kama hataki ndipo apewe fidia ama
vyote viwili.
Serikali ilikubali mapendekezo hayo na kwa mara ya
kwanza katika nchi yetu, hakuna mwekezaji atakayepewa eneo la
umwagiliaji ama kwa kuingia ubia na wenyeji ama kuwalipa fidia lakini na
hapo hapo kuingia nao ubia.
Hakika ndiyo maana kule mwanzo nilihoji kama
katika muswada huu, wabunge waliweka tofauti zao za kisiasa. Je, katika
miswada hii miwili muhimu inayohusu katika mpya wataonyesha uzalendo
huo?
0754 432243
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI