Na Dinna Maningo, Mwananchi
Posted Jumatano,Septemba11 2013 saa 15:30 PM
Posted Jumatano,Septemba11 2013 saa 15:30 PM
Kwa ufupi
Mume anapohisi mtoto aliyezaliwa hafanani nae,
jambo kuu linalofanywa ni kuua mtoto ili kuifanya ndoa iendelee kuwepo
au la mke atarajie mateso au hata talaka.
Tarime. Waswahili husema, mapenzi matamu pale yanapokolea, lakini hugeuka shubiri pale yanapochacha.
Ukweli wa mambo hayo unadhihirika katika maeneo
mbalimbali ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara ambako imebainika kuwa idadi
kubwa ya wanawake, wasichana wanaotoa mimba au kuua watoto wanaowazaa ni
kwa sababu ya mapenzi au kukubaliana na wenzi wao.
Wengine huwanyonga, kuwatupa vichanga au watoto
wadogo kwa sababu ya kuchuja mapenzi au kwa sababu wamekubaliana na
wenza wao wawaue watoto labda kwa sababu hawafanani na mume.
Ukosefu wa uaminifu kwa wapendanao, hususan
waliomo kwenye ndoa imekuwa ni sababu ya wahusika kukata tamaa, jambo
ambalo limesababisha watoto wanaozaliwa kufanyiwa ukatili na hata
kuuawa.
Utafiti uliofanywa katika wilaya hiyo umebaini
kuwa watoto wengi wanaozaliwa na kutupwa ni wale ambao wazazi wao ama
wapo kwenye ndoa au uchumba, ambao watu wake hawaelewani.
Kwa upande wa wanawake, yule aliyekuwa na uhusiano
na mwanamume mwingine na kwa bahati mbaya akapata ujauzito nje ya ndoa
hujikuta akilazimika kutoa mimba au kutupa mtoto pindi anapojifungua ili
kunusuru ndoa au uchumba.
Kadhalika, mwanamume anapomuhisi mkewe kuwa
alikuwa na uhusiano ya kimapenzi na mwanamume mwingine, ajifunguapo
mtoto, humshawishi mke au au yeye huwadhuru wote kwa pamoja.
Pia, mama akishajifungua na baba akaona mtoto
hafanani naye, humshawishi mama kumuua mtoto. Matendo haya jambo
yanaonekana kupigiwa kelele mno na vyombo vya dola, bado yanaendelea kwa
siri kubwa katika baadhi ya maeneo.
Ushuhuda na hali halisi
Ipo mifano kadhaa ya matukio kama hayo kwani
wilayani Musoma mwaka 2011, aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara,
Robert Boazi ambaye kwa sasa yuko Kilimanjaro aliwahi kuwakamata wazazi
ambao walishirikiana kuua mtoto na kisha kumtupa.
Kisa ni nini ?
Ni baada ya baba kudai kuwa mtoto yule aliyezaliwa si wake, bali mwanamke alipewa uja uzito na mwanamume mwingine.
Sufiani Mageta, ambaye ni Katibu wa Afya katika Hospitali ya
Wilaya ya Tarime anasema kuwa wao hupokea watoto wachanga wanaotupwa
baada ya kuzaliwa, baadhi yao hukutwa wakiwa hai na wengine wakiwa
tayari wamekufa.
Anasema kwa mwaka jana pekee, watoto watatu hai
waliokotwa wakiwa wametupwa na sasa wanalelewa katika kituo cha kulelea
watoto yatima kilichopo mjini Musoma.
Askofu Isaac Kitongo wa Kanisa la Jeshi la Wokovu,
Divisheni ya Tarime anasema kuzaa mtoto nje ya ndoa husababisha baadhi
yao kutelekezwa.
Ofisa Habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime,
Magreth Segu anasema: ”Wanaume wa siku hizi wengi, wao wanakataa kuishi
na mtoto wa kambo, hata wakiishi nao wanawanyanyapaa na wengine
wamefikia hatua ya kuwaua kwani anaona ni aibu kwa rafiki zake kuwa
ameoa mwanamke mwenye mtoto”.
Abel Gicheina, Ofisa wa Ustawi wa Jamii katika
Hospitali ya Wilaya ya Tarime anasema: “Siku hizi wengi wanaonekana
wanaingia kwenye uhusiano kwa kuwa na tamaa zaidi ya upendo wa kweli”.
Ofisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Tarime, Mwasiti
Itumbo anasema kuwa zaidi ya kesi 20 zimeripotiwa mwaka jana ofisini
kwake na zote zinazohusu wanandoa kutoka nje ya ndoa na tatizo la
wanaume kutokutoa huduma ya matunzo kwa watoto wanaowazaa.
Itumbo anasema kuwa wanaume hudai kuwa hawatoi matunzo kwa watoto wanaozaliwa kwani wanakuwa si damu yao.
Wanawake kwa upande wao, wanajitetea kuwa wanatoka
nje ya ndoa kutokana na baadhi ya wanaume kutotoa matumizi ya kutosha
kwa familia zao, badala yake wengi wao huwajali zaidi wanawake wa nje
ya ndoa.
Ingawa si wote wenye tabia hii ya kutoka nje ya
ndoa, jambo hilo, ofisa huyo anasema ndilo linalowafanya wanawake nao
watoke nje ya ndoa kutafuta watu wa kuwapa mahitaji, baadhi yao
hujikuta wamepachikwa uja uzito nje ya ndoa.
Lucy John, mkazi wa Tarime (si jina lake halisi)
anasema kuwa baadhi ya wasichana ambao hawajaolewa wakiwamo wanafunzi
wanasema kuwa wataacha kutoa mimba iwapo wanaume wanaowabebesha mimba
watakuwa tayari kulea watoto kwani wengi wao wamekuwa wakikataa ujauzito
na wanaposhtaki polisi hawaoni hatua za kisheria zikichukuliwa dhidi ya
wanaume.
Kauli ya RPC
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa
Tarime/Rorya, Justus Kamugisha anasema kuwa kwa mwaka 2011-2012, zaidi
ya watoto wanane wachanga walikutwa wametupwa wamekufa na wengine wakiwa
hai na kuongeza kuwa watuhumiwa watano walifikishwa mahakamani.
Wengine wamehukumiwa kifungo na kesi nyingine zimefutwa kwa kukosekana ushahidi na sababu mojawapo kubwa ni kutokana na jamii kutokusaidia kutoa ushirikiano Polisi wakati wa upelelezi.
Wengine wamehukumiwa kifungo na kesi nyingine zimefutwa kwa kukosekana ushahidi na sababu mojawapo kubwa ni kutokana na jamii kutokusaidia kutoa ushirikiano Polisi wakati wa upelelezi.
Kamanda Kamugisha anaitaka jamii kushirikiana na
polisi kuwafichua wale wanaobeba mimba na kisha kutoa mimba au kuua
watoto wao ili wachukuliwe hatua zi kisheria.
Anaeleza kuwa jamii ndiyo ipo karibu na wahusika
wa tukio, wamekuwa hawako wazi kuwafichua waovu, jambo ambalo linawapa
ugumu polisi wakati wa upelelezi wao, kiasi kwamba wengine huficha
watuhumiwa.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI