Thursday, 12 September 2013

Wakazi wa Mwasekagi Shinyanga wafunga barabara wakidai maji na umeme


 Wakazi wa kijiji cha Mwasekagi  wilaya ya shinyanga vijijini wamefunga barabara huku wakiwa wameshikilia mabango yenye ujumbe wa mahitaji ya maji  na umeme kwa lengo la kufikisha kilio chao cha  ukosefu wa huduma hizo kwa katibu mkuu wa chama cha mapinduzi(CCM) Bw. Abdulrhaman Kinana hali iliyomlazimu kusimama na kusikiliza kero zao.
Kero hizo ni miongoni mwa kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Shinyanga vijijini ambapo mara baada ya kusikiliza kilio chao katibu mkuu huyo wa CCM  ambaye  ameambatana na mkuu wa mkoa wa Shinyanga Bw Ally Rufunga alimtaka kuwaeleza mipango ya mkoa juu ya upatikanaji wa huduma hiyo ambapo baada ya maelezo ya mkuu huyo wa mkoa bw kinana amewahakikishia wananchi hao kuwa atafuatilia kwa karibu.
Katika ziara yake mkoani Shinyanga katibu mkuu huyo mbali na kuhutubia mikutano ya hadhara pia amekagua miradi mbalimbali ya maendeleo na kujionea hali halisi ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambapo amesema tanzania siyo masikini tatizo kubwa ni urasimu unaofanywa na watendaji wa serikali ambao wanafanya kazi kwa mazoea na kuwataka viongozi wote wa serikali kuanzia mawaziri kuacha tabia ya umangi meza na kwenda kuwahudumia wananchi.
Katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho Bw Nape Nnauye ambaye ameongozana na katibu mkuu huyo akiwahutubia wananchi wa kata ya Salawe, amewataka wananchi hao kuendelea kuiamini CCM kwani ndio chama pekee chenye uwezo wa kuendelea kudumisha amani.
SOURCE: ITV-DAIMA