12 Septemba, 2013 - Saa 13:47 GMT
Mahakama moja nchini Ufaransa
imeamuru kuachiliwa kwa aliyekuwa Kanali wa jeshi la Rwanda , anayesakwa
na taifa hilo kwa kuhusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994
nchini humo.
Rwanda iliwasilisha ombi la kutaka Kanali huyo
Laurent Serubuga, wa kabila la Hutu, na ambaye alihudumu kama naibu mkuu
wa majeshi kurejeshwa nchini humo.Takriban watu 800,000 wengi wao wakiwa wa kabila la Tutsi, waliuawa na wahutu ambao ni wengi kwa idadi nchini Rwanda mnamo mwaka 1994.
Mwanawe Serubuga alikuwa mahakamani kushuhudia kesi hiyo. Wakati jaji akitoa uamuzi wake, alisema kuwa wameridhishwa na uamuzi wa kumwachilia huru babake.
"tulirajaria kesi ya kisiasa. Uongo wa Rwanda haujasikika mbele ya mahakama hii," alinukuliwa akisema na shirika la habari la AFP .
Mahakama iligundua kuwa wakati wa mauaji ya kimbari, uhalifu wa mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu haungeweza kuadhibiwa chini ya sheria ya Rwanda, kwa hivyo, bwana Serubuga hangeweza kuchukuliwa hatua zozote kwa makosa ambayo hayakuwa na adhabu.
Sheria za Ufaransa, haziruhusu mshukiwa au mhalifu kurejeshwa kwao hasa ambapo mshukiwa ana wasiwasi ikiwa haki zake zinaweza kulindwa, alisema wakili wa Bwana Serubuga.
Wakili aliyekuwa anatetea maslahi ya Rwanda alisema kuwa hakushangazwa na uamuzi huo kwani Ufaransa mara kwa mara imekataa kuwarejesha washukiwa wa mauaji hayo nchini Rwanda ili wakabiliwe na sheria.
SOURCE BBC SWAHILI