Kwa ufupi
Weruweru ilijizolea umaarufu kutokana na kutoa
elimu bora kwa wasichana ambao wameweza kuendelea hadi kufikia kuwa
viongozi, kama Dk Asharose Migiro ambaye alikuwa ni mwanamke wa kwanza
kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Dar es Salaam. Waliosoma katika Shule ya
Sekondari ya Weruweru wametamba kuwa wanaamini rais wa kwanza mwanamke
nchini anaweza kutoka miongoni wao, kutokana na kiwango cha elimu bora
inayotolewa katika shule hiyo.
Hayo ameyabainisha jana Dar es Salaam, Mwenyekiti
wa Umoja wa Wanafunzi waliosoma katika sekondani hiyo, Balozi Mwanaidi
Maajar akijibu maswali ya waandishi alipokuwa akizungumzia kuhusu
Maadhimisho ya Miaka 50 ya Sekondari ya Weruweru ambapo Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
“Weruweru ilijizolea umaarufu kutokana na kutoa
elimu bora kwa wasichana ambao wameweza kuendelea hadi kufikia kuwa
viongozi, kama Dk Asharose Migiro ambaye alikuwa ni mwanamke wa kwanza
kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, tunaamini itakuwa ya kwanza pia
kutoa rais mwanamke kwa sababu elimu tuliyoipata inatupa nafasi ya
kuweza kufanya lolote,” alisema.
Alifafanua kuwa kuna wanawake wengine waliosoma
kwenye sekondari hiyo ambao ni viongozi katika nyanja za
wafanyabiashara,madaktari, wanasiasa wanadiplomasia, waandishi, walimu,
wahadhiri na wajasiliamali. Alisema wanalenga kukusanya Sh500 milioni
katika maadhimisho hayo ya miaka 50.
source: Mwananchi
source: Mwananchi