Posted Jumanne,Septemba3 2013 saa 21:4 PM
Kwa ufupi
Wazo hilo la Mbunge Peter Mathuki kutoka Kenya
aliungwa mkono na wabunge wote kutoka Rwanda na baadhi kutoka Kenya,
Uganda na Burundi.
Katika siku za hivi karibuni, kumetokea mambo
kadhaa yanayoonekana kama tishio kwa uhai na mustakabali ya Jumuiya ya
Afrika Mashariki, EAC.
Kwanza, ulikuwa ni mikinzano kimawazo kati ya Rais
Jakaya Kikwete na Paul Kagame wa Rwanda kuhusu njia ya sahihi ya
kukabiliana na makundi ya waasi.
Wakati Kikwete akipendekeza njia ya mazungumzo ya
amani kama njia ya kupatikana kwa mwafaka bila madhara makubwa kwa pande
zote mbili, Kagame kwa upande wake anaona makundi ya waasi yanastahili
kupigwa hadi yatokomezwe.
Kagame amekaririwa akisema kujadiliana na makundi
hayo ambayo baadhi yanatuhumiwa kuhusika kwenye tukio la kihistoria ya
mauaji ya kimbari nchini mwake ni kuwakosea marehemu waliopoteza maisha.
Kwa msimamo na mtazamo wa Rais Kagame, majadiliano
na makundi ya waasi ni sawa na kucheza ngoma juu ya makaburi ya
waliokufa kwenye mauaji hayo ya watu zaidi ya 800,000.
Msigano wa kimawazo na mtizamo baina ya Kikwete na
Kagame ‘yamehanikizwa’ na kikao cha Kagame na wenzake, Uhuru Kenyatta
wa Kenya na Yoweri Mseveni wa Uganda jijini Kampala na kujadili
ushirikiano mpya kati ya nchi hizo katika sekta ya usafirishaji, hasa
reli na Bandari ya Mombasa.
Wakati vumbi hilo kati ya wakuu hao wawili
likiendelea, jambo lingine limeibuka wiki iliyopita wakati wa vikao vya
Bunge la Afrika Mashariki, EALA.
Wabunge wake tisa kutoka kila nchi mwanachama
waliingia kwenye mvutano mkubwa miongoni mwao baada ya hoja ya kutaka
vikao vya Bunge hilo kufanyika kwa kupokezana kutoka nchi moja hadi
nyingine.
Wazo hilo la Mbunge Peter Mathuki kutoka Kenya
aliungwa mkono na wabunge wote kutoka Rwanda na baadhi kutoka Kenya,
Uganda na Burundi.
Mathuki aliwasilisha hoja ambayo ilipata upinzani
kutoka kwa wajumbe wengine waliodai haikuzingatia kanuni na taratibu
zinazoelekeza hoja zote kuwasilishwa mezani kwa spika na kuwekwa kwenye
orodha ya mambo yanayostahili kujadiliwa.
Baada ya hoja yao kupingwa, wabunge wote kutoka
Rwanda hawakuhudhuria kikao kilichofuata na hivyo spika wa Bunge hilo,
Magreth Zziwa kutoka Uganda kuahirisha kikao hadi siku iliyofuata.
Kama mchezo wa kuigiza, siku ya pili, wabunge
kutoka Tanzania, wakiongozwa na Abdulah Mwinyi nao wakawasilisha hoja ya
kuelezea kusikitishwa na kitendo cha wenzao kukwamisha kikao na ili
kuonyesha ‘hasira’ zao, nao wakatoka nje ya ukumbi wa kikao.
Uamuzi wa wabunge wa Tanzania nao kususia kikao kikasababisha
bunge kushindwa kuendelea kwa siku ya pili kutokana na kanuni ya Bunge
hilo linaloelekeza vikao kufanyika baada ya kuwepo uwakilishi wa wajumbe
kutoka nchi zote tano wanachama ambazo ni Rwanda, Burundi, Uganda,
Kenya na Tanzania, kila kimoja kina uwakilishiwa wabunge tisa.
Kila mmoja anaweza kuwa na tafsiri yake kuhusu
matukio hayo mawili, kwanza tofauti ya kimtazamo kati ya Kikwete na
Kagame kwa upande mmoja na mvutano kati ya wabunge wa EAC.
Kwa upande wangu, matukio haya mawili yana dalili
mbaya kwa EAC kwa sababu yametupa picha na fursa ya kuweka kujua nyufa
zinazoikabili jumuiya hiyo ili tutafute mbinu ya kuyakabili na kuyaepuka
madhara mengine makubwa siku zijazo.
EAC imejengwa upya baada ya ile ya awali iliyohusisha Tanzania, Kenya na Uganda kuvunjika mwaka 1977.
Tunahitaji kuwa na EAC imara isiyoyumbishwa na
tofauti ka ya viongozi tunaowapa dhamana ya uongozi. Tunataka tujenge
EAC iliyozama na kuota mizizi miongoni mwa wananchi wake watakaosimama
kidete kuilinda dhidi ya viongozi wabinafsi wanaoweza kujaribu kulivunja
kwa maslahi au utashi wao binafsi.
Nikitumia mfano wa Mwalimu Julius Nyerere
(marehemu), EAC ni sawa na nyumba ambayo uimara wake hujulikana pale
tufani inapovuma na kutikiswa.
Jumuiya yetu imetikiswa na matukio hayo mawili,
Tayari tumeshuhudia penye udhaifu. Sasa turekebishe ili kuepuka madhara
zaidi sasa na baadaye.
Nasema matukio haya ni fursa ya kipekee kwetu sote
kujua maeneo ya kurekebisha wakati tukiendelea na juhudi za kufikia
hatua ya juu ya ushirikiano wa kisiasa, Shirikisho.
Katibu Mkuu wa EAC, Dk Richard Sezibera anasema
mivutano hayo haina madhara kwa jumuiya kwa sababu imejengwa katika
msingi imara usioyumbishwa na tofauti na mivutano midogo midogo miongoni
mwa viongozi au taasisi zinazohusiana na jumuiya.
psaramba@gmail.com, +255 766 434 354.
source; Mwananchi
source; Mwananchi