Monday 23 September 2013

Kurudi nyumbani



Tido Mhando 


Posted  Jumapili,Septemba22  2013  saa 13:16 PM
Kwa ufupi
Tido Mhando amefanya kazi ya utangazaji kwa zaidi ya miaka 40. N i kipindi kilichomwezesha kufanya na kuona mengi kwenye kazi yake hiyo. Kwa hiyo, katika makala zake hizi za kila wiki, anadokeza tu baadhi ya mambo hayo. Sasa endelea…

Niliamka asubuhi ya Jumapili, Februari 3 mwaka ule wa 1974 nimechokachoka. Nilikuwa na ile aina ya uchovu ambayo kule kwetu Bonde tunaiita “mavune”, unaosababishwa na shughuli kubwa. Naam, nilikuwa na shughuli kubwa usiku uliotangulia, au niseme siku yote ya jana yake, ambayo ilikuwa ya heka heka nyingi.
Jumamosi ile ndiyo siku ambayo sisi tuliokuwepo kule Christchurch, New Zealand, tulimshuhudia Mtanzania Filbert Bayi akiweka rekodi mpya ya dunia kwenye mbio za mita 1,500, tukashangilia kupindukia.
Halafu ikawa ndiyo siku yangu ya mwisho ya kutuma ripoti za michezo ile ya Nchi za Jumuiya ya Madola. Nikawa nimeamua kuchapa kazi ya nguvu ya kweli kweli, maana nilikuwa nautua mzigo.
Hatimaye, usiku kukafanyika tafrija ya kuagana ambayo ilikuwa ya kukata na shoka. Waliokula wakala, waliokunywa wakanywa na wapenzi wa muziki na wao wakaselebuka kefu yao; ili mradi ilikuwa usiku wa kujimwaga. Usiku wa furaha.
Ndiyo maana siku hiyo ya pili ikawa ya mavune. Pamoja na hali hiyo, nilikuwa na mambo kadhaa muhimu ya kukamilisha kabla ya kuanza safari ya kurejea nyumbani keshoye.
Kwanza nilikuwa niende kwenye ofisi za Shirika la Ndege la Qantas kuulizia sanduku langu ambalo nilikuwa sijalipata hadi wakati huo, sanduku ambalo lilipotea njiani wakati nikija.
Hawa jamaa waliniambia nisiwe na shaka hata kidogo, lingepatikana tu kabla hata ya siku za michezo kumalizika. Lakini sasa kukiwa kumesalia saa chache tu nisanzue, hali bado ilikuwa ya utata mtupu.
Tayari walikuwa wamenipatia fedha ya kuridhisha, ili niweze kujinunulia mahitaji muhimu na hasa mavazi, na hii ilinisaidia sana. Nilijinua mavazi, si ya kunipamba tu vyema wakati wote wa michezo, lakini pia nikihakikisha ni nguo za uhakika ambazo zingenifanya nilibabaishe jiji nirejeapo Dar.
Kwa kuwa hii pia ilikuwa siku ya Jumapili, siku ya mapumziko, nilitaka nifike ofisi za Qantas mapema, maana sikuwa hata na uhakika kama ningekuta mtu yeyote wa kunisaidia. Nilikuwa na wasiwasi, maana kama nisingefanikiwa kupata msaada unaofaa siku hiyo, basi kila kitu kingesambaratika.
Niliondoka hotelini kwangu mapema asubuhi ile na kwenda kwenye ofisi za Qantas. Nilikuwa nimepewa maelekezo ya jinsi ya kuzipata na hivyo nikawasili hapo kwa rahisi.
Nilifurahi sana kukuta ofisi zikiwa wazi na kwa hakika, nilipokewa vizuri sana, hasa baada ya wenyeji wangu kutambua ya kwamba nilikuwa natoka Tanzania. Walikuwa bado na shauku ya kujua zaidi juu ya ushindi wa Filbert Bayi.
Kwa muda walijisahau kuhusu kile nilochokifuata mapema asubuhi ile, badala yake wakawa wanajadili tu kuhusu pata-shika hasa baina ya mwanaraidha wao John Walker na Filbert Bayi.


Hapana shaka gumzo kuhusu mchuano ule ndilo lililokuwa likitawala mazungumzo mengi nchini mle, hasa kwa kuwa magazeti yote ya Jumapili hiyo yalikuwa vilevile yametawaliwa na stori hiyo, ikiwa ni pamoja na picha kadhaa za kusisimua.
Hatimaye walirejea kwenye shughuli za kazi, wakaniuliza shida yangu. Niliwafahamisha kwa kifupi tu, na palepale wakaelewa shida yangu, kisha wakanifahamisha ni nini cha kufanya.
Kwa jumla tayari shida yangu ya kupotea kwa sanduku ilikuwa imeshapatiwa ufumbuzi. Ilishakubalika kwamba kulikuwepo na uwezekano mdogo sana wa sanduku hilo kupatikana, kwa hiyo lilichobakia, kwa kuzingatia sheria za safari za Shirika la Ndege la Qantas, lilikuwa ni kunilipa fidia ipasavyo.
Kutokana na hali hii, waliniambia kuwa mipango ilikwisha kukamilishwa kwa mimi kulipwa fidia keshoye nitakapofika jijini Melbourne, Australia, wakati nikiwa njiani kurejea nyumbani.
Walinieleza kuwa nitakapofika hapo, ambako ndipo yaliko makao makuu ya shirika hilo la ndege, nitamkuta ofisa wa shirika hilo atakayekuwa ananisubiri na ambaye atanipeleka kwenye ofisi husika za malipo. Kwa hiyo niliondoka ofisini hapo nikiwa na matumaini makubwa ya kupata malipo yangu.
Niliondoka haraka haraka na nikiwa mwenye furaha tele, nikaamua kukamilisha jukumu langu jingine kubwa ambalo nilikuwa nimejipangia kulikamilisha kabla ya kuondoka jijini humo.
Kwa kuwa nilikuwa nafahamu kwamba ningefanya harusi siku chache tu baada ya kurejea nyumbani, nilikuwa nimejitayarisha kununua pete zote za harusi huko huko New Zealand.
Wazee walikuwa wameniarifu mapema kuwa ilikuwa ni wajibu wangu kununua pete, hivyo nilikuwa nimejitayarisha kwa hilo, tatizo likawa kukosa muda wa mapema wa kutimiza jukumu hilo.
Haraka nilisimamisha teksi na kumfahamisha dereva nilikotaka kwenda. Nilifika mahali ambako kulikuwa na maduka chekwa ya vito. Nilihangaika kidogo na mara nikafanikiwa kupata duka lililokuwa na aina ya pete nilizokuwa nikizitafuta.
Nilichagua mbili zilizonipendeza na kuzilipia kama ilivyotakiwa na wauzaji wakaniambia kwamba, ili kuweka kumbukumbu, ingefaa kuziandika kwa ndani, tarehe iliyokuwa imepangwa kufanyika harusi: 24.02.74.
Niliondoka dukani hapo nikiwa nimefarijika kwamba nilikuwa nimekamilisha jukumu langu jingine muhimu. Ila ghafla nikakumbuka kwamba nilikuwa nawajibika kujinunulia sanduku jingine la kusafiria. Nikafanya hivyo haraka haraka na nilihakikisha kuwa na nina sanduku bora kuliko lile lililopotea.
Nilirejea hotelini kwangu na kujipumzisha kwa kuangalia televisheni ambayo nilikuwa nimeanza kuizoea na kuikubali kama chombo kizuri mno kwa kutangazia habari. Nikawa nawaza na kujiuliza ni lini Tanzania nayo itakuwa na kituo chake cha televisheni.

Jambo la kupendeza zaidi ni kwamba siku nzima ile vipindi pekee vilivyokuwa vikionyeshwa mara kwa mara vikuwa vinahusu michezo iliyomalizika, na hasa mbio zile za mita 1,500.
Sijui hata ilikuwakuwaje, lakini nilipitiwa na usingizi na niliposhtuka kulikuwa kumekaribia saa saba usiku, huku bado televisheni ikiwa bado inaendelea na matangazo. Niliizima haraka haraka na kulala vizuri kwa kuwa nilifahamu siku inayofuata ningewajibika kuamka asubuhi na mapema kwenda uwanja wa ndege kwa ajili ya safari kurejea nyumbani.
Ilikuwa ni siku ya Jumatatu; nikaamka mapema nikitilia maanani kuwa nilibaki na muda mfupi sana wa kuendelea kuwepo New Zealand na kwamba baada ya muda mfupi tu ningeanza safari ya kuelekea uwanja wa ndege, tayari kwa kuondoka.
Ilikuwa mnamo saa moja asubuhi tulipofika uwanja wa ndege uliokuwa umefurika watu, hasa wanamichezo mbalimbali waliokuwa wanarejea makwao baada ya kukamilisha wajibu wao, nami nikaenda kuungana na wanariadha wa timu ya Tanzania waliokuwa wamechangamka kweli kweli. Tulikamilisha haraka taratibu zote za uhamiaji na punde tukawa tayari kwa safari yetu ndefu ya kurejea nyumbani kupitia Australia.
Nilipokuwa ndani ya ndege, wakati huo inapaa taratibu, nilichungulia kupitia dirishani na kwa chini, nikauona uwanja wa QEII Park, mahali ambapo Filbert Bayi wetu aliipatia heshima kubwa Tanzania. Nikawa nawaza: Sijui tutapokewa vipi wakati tutakapotua jijini Dar es Salaam!
INAENDELEA JUMAPILI IJAYO

SOURCE: MWANANCHI