Na Daniel Mjema
Posted Ijumaa,Septemba27 2013 saa 24:0 AM
Posted Ijumaa,Septemba27 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
“Ni kweli kuna vurugu kati ya Wananchi wa hicho
kijiji na mwekezaji anayemiliki shamba kubwa la kahawa na migomba ndiyo
vijana wetu wa FFU wameelekea huko,”
Hai: Vurugu kubwa jana ziliibuka wilayani Hai
Kilimanjaro na kulilazimu Jeshi la Polisi kufyatua mabomu ya machozi
katika jitihada za kuzima vurugu hizo.
Hata hivyo, hali iliendelea kuwa tete ilipofika
saa 10:00 alasiri na kulazimu Jeshi la Polisi kuongeza nguvu kwa
kuwatuma askari zaidi wa kutuliza ghasia (FFU) kutoka Moshi Mjini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz
alilithibitishia gazeti hili kuibuka kwa vurugu hizo zilizoanza saa
6:00 mchana katika Kijiji cha Kwansera huko Masama.
“Ni kweli kuna vurugu kati ya Wananchi wa hicho
kijiji na mwekezaji anayemiliki shamba kubwa la kahawa na migomba ndiyo
vijana wetu wa FFU wameelekea huko,” alisema.
Taarifa zaidi kutoka eneo la tukio zilisema Polisi
wenye sare kutoka Kituo cha Bomang’ombe wilayani Hai ndio wa kwanza
kufika eneo la tukio na kujaribu kudhibiti vurugu bila mafanikio.
“Mabomu ya kutosha yameshafyatuliwa hapa tangu saa
6:00 mchana, lakini hali siyo nzuri wananchi wanataka kuchoma moto
majengo ya mwekezaji,” kilidokeza chanzo chetu.
Kiini cha mgogoro huo ni uhasama uliojengeka kati
ya wananchi hao na mwekezaji huyo Mtanzania kutokana na mwekezaji
kuhodhi eneo kubwa huku wananchi wakiwa hawana ardhi.
SOURCE: MWANANCHI