Kwa ufupi
Dar es Salaam. Siku moja baada ya jopo la
madaktari bingwa wa upasuaji kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi)
kwa kushirikiana na wale wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kuokoa
maisha ya mtoto aliyekuwa ameungana na kiwiliwili cha pacha mwenzake,
mama wa mtoto huyo, Pili Hija (24), amesema hakutegemea kama mtoto wake
angepona.
Hija alitoa kauli hiyo jana alipozungumza na
Mwananchi Jumamosi na kudai kuwa, kabla alikata tamaa akidhani
atampoteza mtoto wake, lakini kwa nguvu za Mungu madaktari wamemwokoa na
ameanza kunyonya.
“Sina cha kuwalipa madaktari zaidi nawaombea kwa
Mwenyezi Mungu, sikutegemea kama leo hii ningekuwa na mwanangu
namnyonyesha, nilishakata tamaa na kumkabidhi Mungu, yeye ndiyo amenipa,
basi atende atakavyo. Nashukuru mwanangu anaendelea vizuri,” alisema
Hija na kuongeza huku akitabasamu:
“Bibi yake mzaa baba na shangazi yake walikuja
jana usiku (juzi), wamempa jina la Kudra, kwa vile ni Kudra za Mwenyezi
Mungu pekee ndiyo zimemweka hai mpaka leo.”
Alisema anashukuru mtoto wake ameshaanza kunyonya
vizuri, pia jana asubuhi alipata choo kikubwa na kuwaasa wazazi wenye
watoto walemavu kuacha kuwanyanyapaa kwa kuwaficha.
Daktari Bingwa wa Ubongo na Uti wa Mgongo ambaye
aliongoza jopo la madaktari saba katika upasuaji huo, Dk Hamis Shaaban,
alisema kiwiliwili cha mtoto ambaye hakukamilika licha ya kutokuwa na
kichwa na macho, hakikuwa na moyo, figo, tumbo na maini.
Dk Shaaban alisema kilikuwa na uti wa mgongo na
kwamba, huenda tatizo hilo limesababishwa na upungufu wa madini ya Folic
Acid ambayo mama alitakiwa kupata kipindi cha ujauzito.
Hata hivyo, Pili alipoulizwa kuhusu kutumia madini
hayo kipindi cha ujauzito alisema: “Nilipokuwa na mimba nilikuwa naumwa
umwa sana, nikaanza klinic ikiwa na miezi mitatu, nilikutwa sina damu
kuna dawa nilipewa za kuongeza damu nikazitumia zilipoisha nikarudi
tena, ikawa imeongezeka nikambiwa nisitumie tena.”
Msemaji wa Moi, Jumaa Almas, alisema mtoto
anaendelea na ananyonya vizuri, bado yupo chini ya uangalizi maalum
(ICU) hadi afya yake itakapoimarika.
source:Mwananchi
source:Mwananchi