Monday, 2 September 2013

Serikali ihakikishe benki zinapewa ulinzi

                       
                                                                      Benki Kuu 



Posted  Agosti31  2013  saa 23:20 PM
Kwa ufupi
Pamoja na Benki Kuu (BoT) kuweka sera za kuiongoza sekta nzima ya benki nchini, Serikali bado haijaonyesha kusimamia kikamilifu suala zima la usalama katika benki hizo.


Habari za Benki ya Habib, Tawi la Kariakoo jijini Dar es Salaam kuporwa Sh1 bilioni na majambazi mchana kweupe mwishoni mwa wiki zinathibitisha kwamba Serikali bado ina safari ndefu katika kuhakikisha benki zinazofanya kazi nchini zinafanya biashara katika mazingira salama.
Pamoja na Benki Kuu (BoT) kuweka sera za kuiongoza sekta nzima ya benki nchini, Serikali bado haijaonyesha kusimamia kikamilifu suala zima la usalama katika benki hizo.
Matokeo yake sote tumekuwa tukiyashuhudia kwa muda mrefu. Benki nyingi zimekuwa zikiporwa fedha kwa njia mbalimbali, lakini nyingi zinaamua kutotangaza matukio hayo hadharani kwa kuhofia kuwafaidisha washindani wake na kukimbiza wateja. Benki zinazoweka matukio hayo hadharani ni zile zinazoporwa mchana kweupe, huku kadamnasi ya watu ikishuhudia na kuvifahamisha vyombo vya habari, kama ilivyokuwa katika tukio la Benki ya Habib.
Ulinzi na usalama katika benki hapa nchini unahitaji mbinu za kisasa kutokana na mbinu za zamani kama kutumia askari wenye virungu kupitwa na wakati, kwani majambazi na wezi wanaozivamia na kupora mamilioni ya fedha wanatumia teknolojia na silaha za kisasa kama ilivyokuwa katika tukio hilo la mwishoni mwa wiki. Ndio maana sekta ya benki duniani kote imewekeza sana katika ulinzi wa teknolojia ya kisasa kutokana na majambazi kubadili mbinu mara kwa mara.
Kama Jeshi la Polisi lilivyothibitisha, majambazi waliovamia benki hiyo ya Habib hawakutumia nguvu nyingi. Waliingia katika benki hiyo kiulaini na kujifanya wateja, huku wakiwaita baadhi ya wafanyakazi kwa majina. Waliwaamuru kutoa funguo za chumba cha kuhifadhi fedha, wakawaweka chini ya ulinzi pamoja na wateja wachache waliokuwamo, huku dereva wa teksi aliyewaleta akiwa nje akiweka ulinzi na kuwasiliana nao kwa ‘radio call’. Baada ya muda mfupi walitokomea kusikojulikana, huku wakiwa wamebeba kitita hicho pasipo kutoka jasho.
Tukio hilo pamoja na matukio mengine yaliyotangulia yanapaswa kuwa somo tosha kwa Serikali na sekta ya benki hapa nchini. Kwamba pande hizo mbili hazina budi kushirikiana katika kuhakikisha unakuwapo ulinzi stahiki katika benki hizo. Ni aibu kubwa kwa sekta hiyo kukubali kufanywa ‘shamba la bibi’, kwa majambazi kuachwa kupora fedha katika benki hizo na kuondoka nazo kiulaini. Hakuna jinsi sekta hiyo inavyoweza kujivua jukumu la kuwekeza katika ulinzi wake yenyewe kama ambavyo Serikali haiwezi kukwepa dhima ya kuhakikisha yanakuwapo mazingira mazuri kwa wawekezaji katika sekta hiyo, kutokana na mchango wake mkubwa katika kukuza pato la taifa.
Kinachotakiwa sasa ni Serikali na BoT kuzileta pamoja benki zote zilizo hapa nchini na kutoa vigezo vya ulinzi ambavyo kila benki lazima ivifikie. Hii ni pamoja na kufunga kamera za usalama kila kona ndani na nje ya benki; kufunga vyombo vya mawasiliano; kutoa mafunzo maalumu kwa wafanyakazi kuhusu usalama; kuweka kampuni za ulinzi zenye rekodi za ufanisi na uaminifu; na kuweka milango ya kufunga na kufungua kwa ‘rimoti’, kitufe au namba maalumu ili majambazi wakiingia wasiwe na mahali pa kutokea.
Lakini pia benki zenyewe zisitoe ajira kiholela bila kuchunguza vizuri rekodi za waajiriwa, kwani imedhihirika katika matukio mengi baadhi ya wafanyakazi wanahusika. Ni matumaini yetu kwamba hatua hizo zikichukuliwa uporaji katika benki utapungua kama siyo kutoweka kabisa.

source: BBC