Tuesday 10 September 2013

Usajili wa meli za kigeni uangaliwe upya


Meli ya Gold Star iiliyosajiliwa Tanzania ikiwaka moto baada ya mabaharia wake kuichoma iliponaswa ikiwa imebeba dawa za kulevya aina ya bangi katika pwani ya Italia juzi. Picha ya Reuters  

Posted  Jumatatu,Septemba9  2013  saa 22:49 PM
Kwa ufupi
Tunashindwa kupata maneno stahiki ya kulaani kitendo cha kusajili meli za kigeni kiholela na kuziwezesha kufanya biashara au vitendo vya kihalifu, huku zikipeperusha Bendera ya Tanzania.


Ni jambo la kusikitisha kwamba jina la Tanzania limezidi kuchafuliwa mbele ya jumuiya ya kimataifa baada ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa Zanzibar kukamatwa Jumamosi iliyopita katika Bahari ya Mediterranean ikiwa na tani 30 za dawa za kulevya aina ya bangi yenye thamani ya Sh125 bilioni.
Meli hiyo iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Tanzania ilinaswa na askari wa doria wa Italia waliokuwa Pwani ya Sicily katika Bahari hiyo ya Mediterranean. Idara ya Ushuru ya nchi hiyo ilisema, meli hiyo ilikamatwa baada ya taarifa za kiintelijensia kwamba ilikuwa imebeba dawa hizo, lakini ikasema haikutarajia kama ingekuwa imebeba mzigo mkubwa kiasi hicho.
Tukio hilo la aibu kubwa kwa Tanzania limethibitishwa na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA), Abdi Omar ambaye alisema juzi kwamba ofisi yake iliwasiliana na Kampuni ya Philtex yenye ofisi zake Dubai ambayo ilithibitisha kuisajili meli hiyo mwaka 2011 kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar kwa kazi ya kubeba mizigo chini ya Kampuni ya Gold Star.
Alisema kutokana na tukio hilo, Kampuni ya Gold Star imekiuka masharti ya Sheria ya Usajili wa Meli na ile ya Umoja wa Mataifa (UN) zinazozuia meli kubeba dawa za kulevya, huku akisema ofisi yake itafanya uchunguzi na kuchukua hatua. Jeshi la Polisi nchini lilithibitisha kukamatwa kwa meli hiyo na kusema ilikuwa ikipeperusha bendera ya Tanzania na kwamba ilisajiliwa na Serikali ya Zanzibar.
Tunashindwa kupata maneno stahiki ya kulaani kitendo cha kusajili meli za kigeni kiholela na kuziwezesha kufanya biashara au vitendo vya kihalifu, huku zikipeperusha Bendera ya Tanzania. Hakuna ubishi kwamba usajili holela wa meli za kigeni ambao umekuwa ukifanywa na Serikali ya Zanzibar, sio tu umeharibu jina zuri la taifa letu mbele ya jumuiya ya kimataifa, bali pia umesababisha maafa makubwa ambapo watu wengi wamepoteza maisha kutokana na meli hizo kusajiliwa pasipo kukidhi vigezo vilivyowekwa kisheria.
Yafaa tujikumbushe hapa, angalao kwa muhtasari tu jinsi usajili huo holela ulivyosababisha maafa na kuharibu jina la taifa letu nchi za nje. Bila shaka sote tunakumbuka maafa yaliyotokea huko Zanzibar kutokana na kuzama kwa MV Spice Islander, Septemba 10, 2011 na MV Skaget, Julai 19, 2012 ambapo watu wengi walipoteza maisha kutokana na ubovu wa meli hizo.
Lakini matukio mabaya zaidi yalikuwa pale meli za Iran 36 ziliposajiliwa na Serikali ya Zanzibar wakati nchi hiyo ikiwa chini ya vikwazo vya UN, lakini zikakwepa vikwazo hivyo kwa kujisajili Zanzibar na kupeperusha Bendera ya Tanzania. Kwa hatua hiyo, Tanzania iliponea chupuchupu kuwekewa vikwazo na UN na mataifa mengine, ikiwamo Marekani. Hakuna anayejua hatua zitakazochukuliwa dhidi ya Tanzania kutokana na kukamatwa kwa meli hiyo ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa Zanzibar ikiwa na shehena kubwa ya dawa za kulevya, pia ikiwa inapeperusha Bendera ya Tanzania.
Tunadhani sasa umefika wakati wa suala la usajili wa meli za kigeni kuwa suala la Muungano. Ni hatari kubwa pale kila upande wa Muungano unapofanya kivyake mambo nyeti kama usajili wa meli za kigeni. Nani hajui kwamba kufanya hivyo tunahatarisha usalama wa taifa letu?

source: Mwananchi