Friday, 13 September 2013

Lulu; Watu wengi hawajui thamani yake, haibadiliki

 “Iwapo chaza wangekuwa wanakuzwa na kuvunwa lulu kama ilivyo katika nchi nyingine ni wazi mapambo ya plastiki kutoka China yasingekuwa na nafasi na  wananchi wangetengeneza ajira na mapato ya serikali yangeongezeka.” 

Na Joseph Zablon, Mwananchi

Posted  Alhamisi,Septemba12  2013  saa 10:38 AM
Kwa ufupi
Kito hicho ni tofauti na madini ya almasi, dhahabu, Tanzanite, Ruby na madini mengine ambayo yanachimbwa, lakini Lulu inatokana na wanyama jambo ambalo watu wengi hawalifahamu.


Lulu imekuwa kito cha kufikirika nchini kwani watu wachache wanaitambua na Serikali haina mipango ya kufanya chaza kwa ajili ya biashara.
Inaitwa Lulu kwa lugha ya Kiswahili. Kwa lugha ya Kiingereza ni ‘Pearl’.Hicho ni kito cha thamani ambacho mara nyingi kinakatwa, kusuguliwa na kung’arishwa kwa namna mbalimbali na kutumiwa pamoja na madini mengine kama dhahabu au fedha na kutengenezwa mapambo kama pete, hereni, mikufu au vikuku.
Lulu inatajwa siku nyingi kuanzia katika misahafu ambavyo ni vitabu vitakatifu kwa waumini wa dini ya Kiislamu hadi katika Bibilia na hadithi nyingine za kale. Nchini kuna utajiri mkubwa wa Lulu, lakini hakuna  jitihada zozote za kuvuna kito hicho cha thamani ambacho moja ya sifa yake kuu ni kutobadilika rangi yake kwa namna yoyote katika kipindi chote cha kudumu kwake labda iharibiwe kwa tindikali.
Lulu ni nini?
Kito hicho ni tofauti na madini ya almasi, dhahabu, Tanzanite, Ruby na madini mengine ambayo yanachimbwa, lakini Lulu inatokana na wanyama jambo ambalo watu wengi hawalifahamu.
Kwa jicho la pili ni eneo lingine ambalo vijana wanaweza kujiajiri kwa wingi, lakini endapo Serikali itakuwa nyuma ya vijana.
Kulingana na takwimu mbalimbali, Lulu hupatikana katika viumbe hai aina ya chaza ambao wanafanana na konokono wadogo na mara nyingi wanyama hao hupatikana chini ya bahari na kwa kawaida wanaliwa.
Tafiti mbalimbali zinabainisha kwamba watu wengi huwakusanya chaza hao na kuwachemsha kabla ya kubomoa gamba lao na kuitoa nyama ambayo inaliwa zaidi na watu wa makabila ya mwambao wa Pwani na kuna ambao wanahusisha na masuala ya tiba.
Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Shaaban Kikoti anasema chaza wanavuliwa sana Ufukwe wa Kigamboni na wanachemshwa wakiwa katika makopo au magaloni mbele ya jengo la Ikulu na kinamama ambao baadaye huuza.
Anasema ingawa hakuna takwimu sahihi, lakini nyama hiyo inahusishwa na kuongeza virutubisho mwilini na kuchochea ongezeko la homoni ambazo zinaongeza nguvu za kiume kwa wanaume na upande mwingine gamba la mnyama huyo hutumika kama mapambo majumbani na kwingineko.
Mhadhiri Mwandamizi wa Kemia ya Mazingira Bahari katika Chuo Kikuu Dar es Salaam, Idara ya Sayansi Bahari, Aviti Mmochi anasema Lulu ni moja kati ya mazao ya bahari ambayo kama yangetumika vizuri yangewanufaisha wakazi wa Pwani na Taifa kwa ujumla kuliko sasa.
Mtalaamu na mtafiti huyo anasema kwa kawaida chaza ana magamba na chakula chake hukipata baada ya kuyachuja maji ambayo kwa kawaida anayavuta baada ya kufungua na kufunga magamba yake na wakati wa tendo hilo kuna mabaki ambayo ni chakula kwake hubakia.

Wakati mwingine mchanga unabaki ndani ya jumba lake na kumkera na kuutengeza aina fulani ya ute na kukifungia kitu hicho ili kisiendelee kuzunguka ndani ya mwili wake na bahati mbaya au nzuri anasema malighafi hiyo huwa inang’aa sana.
Mmochi anasema nchini wanyama hao wanaharibiwa kwa kuliwa na baadhi ya watu mapema kabla hawajapevuka vya kutosha na mbaya zaidi hakuna ufugaji wa chaza uliolenga uzalishaji wa lulu tofauti na inavyofanyika katika nchi  nyingine.
 “Iwapo chaza wangekuwa wanakuzwa na kuvunwa lulu kama ilivyo katika nchi nyingine ni wazi mapambo ya plastiki kutoka China yasingekuwa na nafasi na  wananchi wangetengeneza ajira na mapato ya Serikali yangeongezeka,” anasema mhadhiri huyo.
Serikali haina mpango
Hivi sasa Lulu imekuwa kito cha kufikirika nchini kwa kuwa ni watu wachache ambao wanaitambua na Serikali na taasisi zake hazina mipango ya kufanya ufugaji wa chaza kwa ajili ya biashara.
Mmochi anasema Lulu inapatikana kwa kuwafuga chaza katika maeneo maalumu ambayo yanakuwa yamepangwa na kabla ya kufanya uzalishaji wa lulu ni lazima uchonge kitu kulingana na mahitaji yako.
“Mtu unaweza ukakata kipande cha chupa, plastiki kwa umbo la moyo, chozi au msalaba kisha unakipaka gundi Super Glue,” anabainisha.
Anasema mfugaji wa chaza atamwangalia jinsi rangi zake zilivyojipanga na kusogeza nyama zake kidogo na ukipachika kitu hicho katika rangi anazozipenda mnyama huyo anarudishwa katika maji kuendelea na maisha yake na kitu hicho kinamkera hivyo anazalisha ute mwingi zaidi kukikabili.
“Ute huo hubadilika na kuwa mgumu mithili ya mfupa katika umbo tarajiwa,” anasema. Anaeleza kwamba hatua hiyo hupitia katika kipindi cha miezi tisa hadi mwaka mmoja kabla ya chaza kutolewa nje  ya maji.
Anasema akitolewa unavuna lulu kwa kutoa nyama yake na jumba lake kusafishwa na kulisugua ili kupata lulu safi ambayo inakuwa imejitengeneza kulingana na ulivyotaka  na anabainisha kwamba chaza huyo unaweza kumtoa walau mara moja kila mwezi na kuangalia jinsi anavyoendelea.
Mmochi anasema baada ya kuisugua lulu unakata kipande kulingana na mahitaji yako na kipande cha vipande vinavyobaki vinatengenezwa heleni au kitu kingine cha namna hiyo.
Bei ya lulu ni kati ya Sh30,000 hadi Sh50,000 na ubora wake hubaki kama ulivyo bila kuathiriwa na kitu kingine.
Mmochi anasema wengi hawaelewi, lakini Lulu ina mwonekano na mvuto usio wa kawaida tofauti na madini mengine.

SOURCE: MWANANCHI