Na Sharon Sauwa, Mwananchi
Posted Oktoba26 2013 saa 10:28 AM
Posted Oktoba26 2013 saa 10:28 AM
Kwa ufupi
Kauli hiyo ilitolewa jana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba.
Dodoma. Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara,
Mwigulu Nchemba, amesema makundi yaliyotokana na uchaguzi katika jumuiya
za chama hicho, yanawapa shida.
Nchemba aliyasema hayo jana alipokuwa akifungua
mafunzo ya siku tatu kwa viongozi na watendaji wa Umoja wa Wanawake wa
Tanzania (UWT), mjini Dodoma.
Hata hivyo, Nchemba ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati
Kuu ya CCM, alisema UWT imetulia tofauti na jumuiya nyingine za chama
hicho kikongwe cha siasa nchini.
Jumuiya nyingine za chama hicho ni Wazazi na Umoja wa Vijana (UVCCM).
“Jumuiya nyingine tunapata shida, wanaadhibiana lakini kwenu UWT, kumetulia,”alisema Nchemba.
Aliwataka UWT kuvunja makundi na kushirikiana katikia kuiendesha.
“Tangu zamani wanawake wanatabia ya kusameheana,
mshirikiane na wale waliowachagua na wasiowachagua. Msiruhusu makundi,”
alisema.
Alitoa mfano wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya
Kikwete ambaye amekuwa akitoa nafasi za uongozi kwa watu wote wakiwemo
waliomtukana wakati uchaguzi mkuu.
Hata hivyo, alisema makundi yanayomuunga mkono
mgombea katika chaguzi si dhambi, lakini yanatakiwa kuvunjwa baada ya
kumalizika kwa chaguzi.
Pia aliwataka kuhakikisha kuwa wanawake
wanaandikishwa katika daftari la kudumu la kupiga kura na kujitokeza
kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.
Naibu katibu mkuu huyo, alisema daftari hilo ni la
muhimu katika maisha ya Watanzania na kwamba ni vema watu wakijitokeza
kila linapofanyiwa marekebisho.
Aliwataka wajumbe kujadili kwa kina mambo yote muhimu.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI