Kwa ufupi
Nani aliyepoteza au kunufaika katika Muungano wa sasa– Tanganyika au Zanzibar? Kwa haraka naweza kusema ni Zanzibar.
Zanzibar. Kwa muundo wa
Muungano wa Serikali mbili Zanzibar haipiki wala haipakui, yenyewe
inasubiri ukumbuni kitakachopikwa ndicho itakachokula.
Hii ndio falsafa ya baadhi ya wanasiasa Zanzibar
ambao kwa hofu tu ya kupoteza ulwa wanajiweka katika nafasi ya ‘mgeni
mwalikwa’ wakati yenyewe ndio mwenye shughuli.
Zanzibar kwa asili yake, kwa maumbile yake
haistahiki kuwa ilivyo, haifurahishi kuona inapoteza mila, silka,
utamaduni wala historia yake iliyotukuka.
Cha ajabu leo miaka 49 ya Muungano, kuelekea
jubilee ya miaka hamsini mwakani, umaarufu wa Zanzibar unazikwa na
wanasiasa wa kambi ya kihafidhina kwa kisingizio cha kupambana na
wapinga mapinduzi!
Ni ukweli uliowazi kwamba Wazanzibari wengi
wanauona mfumo wa serikali mbili kama ni jakamoyo, wanajiuliza kwani wao
wana nafasi gani katika Muungano huu?
Je wamenufaika vipi na ushirikiano huu wa kisiasa
kwa miaka 49 au ndio maneno yale yale ya udugu na historia ambayo
hayawezi kufutika.
Nani aliyepoteza au kunufaika katika maumbile ya
sasa ya Muungano – Tanganyika au Zanzibar? Kwa haraka haraka naweza
kusema ni Zanzibar iliyopoteza kila kitu. Imepoteza nguvu za nchi,
imepoteza mamlaka yake sio tu ya kimataifa bali hata ya ndani maana kuna
mambo mpaka ‘kaka mkubwa’ atake, apendezwe na jambo fulani.
Kiti kinachokaliwa na Balozi wa Kudumu wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Umoja wa Mataifa ni cha Tanganyika iliyojiunga
na UN Desemba 14 mwaka 1961, kilichohaulishwa kwa Muungano na si cha
Zanzibar iliyojiunga na UN Desemba 16, mwaka 1963.
Kumbukumbu za maandishi ya Umoja wa Mataifa
zinaonesha kwamba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilijiunga na UN siku
ambayo Tanganyika ilijiunga na umoja huo, jawabu unayo mwenyewe.
Tukiwa na mfumo wa muundo wa Muungano ambao
utaifanya Zanzibar na Tanganyika kujiunga na mashirika na taasisi za
kimataifa kama UN, ICC, WTO, IMF, WB na mengine bila shaka utatuondoshea
jakamoyo walilonalo wananchi.
Mara baada ya mapinduzi ya Januari 12 mwaka 1964,
Zanzibar ilianza kazi ya kujenga uchumi madhubuti, wakoloni wakibezwa,
ari ya kujitawala ilikuwa kubwa, maadui watatu wakatangazwa – umaskini,
ujinga na maradhi.
Tumekuwa tukijiuliza Zanzibar ina nafasi gani,
ubavu gani wa kupambana na maadui hao ambao kwa maumbile, hulka zao
wanahitaji kushughulikiwa kwa kiasi kikubwa na mashirika kama Benki ya
Dunia, Umoja wa Mataifa, Shirika la Fedha Duniani, Shirika la Sayansi,
elimu na utamaduni na Shirika la Afya ulimwenguni.
SOURCE: MWANANCHI
Waziri wa Afya wa Zanzibar pamoja na ukakamavu, uhodari wake
hawezi kutia saini mkataba wa kimataifa bila ya kuomba ruhusa wala
kupata kibali cha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe.
Kibali chenyewe inategemea na siku yenyewe,
akiamka na mazonge ya Jimbo la Mtama, itabidi usubiri maana hakuna nguvu
za kisheria za kumshurutisha kutekeleza suala hilo, huku wananchi wako
wa Mtende, Kitope, Pongwe wakisubiri kuona utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi uliyoinadi.
Kwa sababu ya umaskini uliokothiri, wananchi wengi
hawapati chakula bora na kwa hivyo, utapiamlo nao ni tatizo kubwa hapa
Zanzibar, hasa kwa shamba nyingi za hapa Zanzibar ambapo kikawaida
chakula chao ni cha aina moja tu kila uchao kwa sababu ya kutokuwa na
kipato cha fedha cha kutosha.
Tatizo la ajira ni maumivu mengine hasa kwa
vijana ambao licha ya kupata elimu kwa mazabe mazabe, mashaka, lakini
wamalizapo mafunzo yao wanaselelea vijiweni kuhesabu ndege zituazo na
zinazo paa pale Kisauni.
Maisha ya Wazanzibari wengi ni magumu, lakini kwa
sehemu za mashamba maisha yanakuwa magumu zaidi na kwa hivyo idadi kubwa
ya watoto wanaomaliza masomo darasa la kumi hulazimika kukimbilia mjini
Unguja ambako nako pia hakuna ajira na kusababisha ongezeko la idadi ya
watoto wa mitaani na wazururaji katika Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja.
Tunaambiwa takwimu za sense ya watu na makazi
iliyofanyika mwaka 2012 Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja una watu
593,678 sawa na asilimia 46 ya watu wote wa Zanzibar.
Idadi ya watu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
imeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka watu milioni 12.3 mwaka 1967 hadi
watu milioni 44.9 mwaka 2012. Kati yao 43,625,354 wapo Tanzania Bara na
1,303,569 wapo Tanzania Zanzibar.
Tunaambiwa kuwa taarifa za Sensa ya mwaka 2012
zitatumika kutathmini Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 kwa Tanzania Bara
na Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2020 ya Zanzibar.
Pia, itatumika kutathmini Mpango wa Maendeleo wa
Miaka Mitano 2011/12 – 2015/16, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza
Umaskini (Mkukuta) kwa Tanzania Bara (Tanganyika) na Mkakati wa Kukuza
Uchumi na Kupunguza Umaskini Zanzibar (Mkuza) pamoja na Malengo ya
Milenia ya Mwaka 2015.
Je, Zanzibar imetimiza vipi vigezo vya malengo ya
milenia 2015 ilhali ikiwa ni ‘mgeni mwalikwa’ kwenye ukumbi unaopanga
masuala hayo?
Kwanini hatufikiri kwa makini zaidi kutanguliza
maslahi ya umma mbele, hasa tukitazama ongezeko la watu mwaka 1967 na
mwaka 2012 kuwa kunahitajika mabadiliko ya mfumo wa muundo wa Muungano
kwa kuwa mahitaji ya watu yameongezeka?
Ongezeko la vibaka, wezi na kukithiri kwa vitendo
vya baadhi ya wanawake kujiuza mijini ni ushahidi wa kuporomoka kwa
maadili, lakini kwa kiwango kikubwa hali hiyo inasababishwa pia na
umaskini uliokithiri katika jamii.
Na jambo hili ni hatari kwa amani na utulivu wa nchi yetu. Bado
Wazanzibari wanaishi chini ya mstari mwekundu wa umaskini huku
wakitegemea pato la chini ya dola moja.
Jamani, wakati umefika kuchagua historia nzuri ya
nchi yetu, tuacheni ubabaishaji, undumilakuwili na upopo wa leo kuwa
ndege, kesho mnyama. Tuchague historia bora kwa maisha yetu.
SOURCE: MWANANCHI