Dar es Salaam. Siku moja baada ya Serikali 
kuweka msimamo wake baada ya nchi za Kenya, Uganda na Rwanda 
kutoihusisha Tanzania katika mambo yanayohusu Jumuiya ya Afrika 
Mashariki (EAC), wasomi nchini wamesema Jumuiya hiyo inaendeshwa kwa 
uamuzi wa wanasiasa, wananchi hawashirikishwi katika uamuzi.
Wamesema mara nyingi nchi zilizopo katika umoja zinatupiana maneno baada ya kutofautiana kwa viongozi wake wa kisiasa.
Walisema sababu za kujitoa zilizotolewa na 
Tanzania hazina mantiki. Juzi Serikali kupitia kwa Waziri wake wa 
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ilieleza msimamo wake 
ikiwa ni pamoja na kutohudhuria mikutano ya jumuiya hiyo yenye ajenda 
ambazo nchi hizo tatu zimekwishaweka msimamo wa peke yao.
Nchi za Rwanda, Uganda na Kenya zimeanzisha 
ushirikiano wa pamoja katika maeneo ya miundombinu, biashara na viza ya 
pamoja na mara nyingi viongozi wakuu wa nchi hizo wamekuwa wakifanya 
mikutano bila kuzihusisha Tanzania na Burundi
.
.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti 
jana, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bashiru Ally, alihoji, 
“Uamuzi wa Tanzania kujitoa katika EAC unafanywa kwa niaba ya wananchi 
au wanasiasa?”
Alisema mkataba wa jumuiya hiyo unaeleza kuwa 
jumuiya ni mali ya watu wa Afrika Mashariki. Mhadhiri mwingine wa chuo 
hicho, Dk Kitila Mkumbo alisema sababu zinazoelezwa na Serikali hazina 
mantiki.
“Binafsi naona jumuiya hii ni ya wanasiasa. 
Sidhani kama Serikali yetu imewahi kuwaeleza wananchi kuwa Tanzania 
inafaidika vipi na jumuiya hii.”
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria, Emmanuel Mallya 
alisema kuwa, msingi wa jumuiya hiyo ni kushirikiana kwa mambo yenye 
masilahi kwa nchi husika.
“Kama Tanzania inaona nchi nyingine zinataka 
kushirikiana nayo katika mambo ambayo yenyewe haijayaafiki sidhani kama 
litakuwa jambo baya kujitoa,” alisemaSOURCE: MWANANCHI