Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Ijumaa,Oktoba18 2013 saa 24:0 AM
Posted Ijumaa,Oktoba18 2013 saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Lengo lilikuwa ni kuwahabarisha Watanzania kwa misingi ya taaluma na weledi.
Dar es Salaam. Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa
,ndiye aliyeialika Kampuni ya Nation Media Group (NMG) ya Kenya, kuja
kuwekeza katika sekta ya habari hapa nchini, imeelezwa.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NMG, Wilfred
Kiboro alisema juzi usiku jijini Dar es Salaam kuwa, baada ya kupata
wito huo, NMG iliamua kuja kuwekeza Tanzania kwa kununua hisa katika
Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL).
“Nakumbuka wakati huo nikiwa Ofisa Mtendaji Mkuu
wa NMG, niliambatana na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi na tulikwenda
kumwona Rais Mkapa kule Arusha na katika mazungumzo yetu, alitualika
tuje kuwekeza nchini,” alisema Kiboro alipokuwa akizungumza kwenye hafla
ya MCL na wadau wake juzi.
Alisema: “Rais Mkapa alituambia angependa
Watanzania wahabarishwe katika misingi ya taaluma na weledi kwa kupewa
taarifa zisizoegemea upande mmoja na za kweli, tumefanya kazi hii kwa
ufanisi katika safari ndefu ambayo tumekuwa nayo”.
Kiboro alisema uwekezaji kupitia MCL umechangia
kwa kiasi kikubwa katika uchumi wa nchi kupitia kodi mbalimbali
zinazolipwa na kwamba mchango huo, hauna maana kwamba kampuni hiyo
inabeba ajenda yoyote kutoka Kenya.
“Hatuna ajenda yoyote ya Kenya hapa Tanzania, na
pengine ajenda tuliyonayo ni moja tu nayo ni kuimarisha ushirikiano
katika Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema Kiboro.
“Kwa hiyo, kama alivyosema Mwenyekiti wa Bodi ya
MCL, hakuna kumbukumbu zozote zinazoonyesha kwamba MCL inaendeshwa kwa
maelekezo au maagizo kutoka Kenya, hatujawahi kufanya hivyo na wala
hatuna mpango wa kufanya hivyo,” alisisitiza.
Kiboro pia alizungumzia kufungiwa kwa Gazeti la
Mwananchi kwa muda wa wiki mbili na kuweka bayana kwamba, hatua hiyo
ilikuwa na athari kubwa kwa watu ambao kwa namna moja au nyingine wana
uhusiano na gazeti hili.
“Pengine ni wito wetu kwa Serikali kwamba
kunapokuwa na tatizo kwenye vyombo vya habari ifuate mkondo wa
kimahakama kuliko utaratibu unaofanya Serikali iwe mlalamikaji,
mwendesha mashtaka, shahidi na hata mtoa hukumu,” alisisitiza.
Mwenyekiti wa MCL:
Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya MCL, Zuhura Muro,
alisema Serikali ni kama ilifanya kuvizia wakati ikichukua hatua za
kulifungia Mwananchi kutokana na vitendo vilivyoambatana na kufungiwa
huko
“Ni kama walituvizia, wale mliopita jeshini mtakuwa mnafahamu
vizuri uviziaji, maana hata katika mkutano wa waandishi wa habari
ulioitishwa ili kutangaza Mwananchi limefungiwa, waandishi wa habari wa
Mwananchi hawakualikwa wala wa Gazeti la The Citizen hawakualikwa,”
alisema Muro.
Alisema alipigiwa simu na watu waliomweleza kuwa
gazeti limefungiwa baada ya kuona taarifa kwenye mitandao ya kijamii na
alipokwenda kwenye Mtandao wa Jamii Forums, alikuta taarifa ya Gazeti la
Serikali (GN) inayoeleza kufungiwa kwa Mwananchi.
“Baada ya kuthibitisha kweli ni taarifa ya
Serikali, nilitoa maelekezo gazeti lisichapishwe, pamoja na hatua hiyo
bado usiku ule unamwona Ofisa wa Serikali akizungumza kwenye televisheni
Mwananchi ni wakaidi, unajiuliza huu ni ukaidi upi,” alisema.
“Taarifa ya kufungiwa ilitolewa kwenye Gazeti la
Serikali la Septemba 27, lakini mkutano wa waandishi wa habari
uliitishwa Septemba 28 wakati gazeti letu lipo mitaani, lakini sisi
tuliletewa taarifa rasmi ya kufungiwa kwa maandishi, Jumatatu Septemba
30, saa 8:00 mchana, ndiyo maana nasema sikuelewa lugha kwamba Mwananchi
ni wakaidi,” alisisitiza Muro.
Alisema pamoja na maumivu yaliyotokana na
kufungiwa huko, MCL itaendelea kutimiza wajibu wake kwa umma kama
ambavyo imekuwa ikifanya.
“Tumefanya mengi, tumekuwa na mfululizo wa makala
kuhusu miaka 50 ya uhuru wa nchi yetu, tumeanza kufanya hivyo kwa ajili
ya miaka 50 ya Muungano, tunaandika kitabu kwa ajili ya kutunza
kumbukumbu, sasa hapo pengine mtu atuambie ni uzalendo wa aina gani
tunaopaswa kuwa nao,”alihoji Muro.
Mmoja wa waliohudhuria hafla hiyo, Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, alisema mchakato
wa Katiba Mpya unaoendelea nchini unaweza kusaidia kuondoa kile
kinachoonekana kuwa ni sheria kandamizi.
SOURCE: MWANANCHI