13th October 2013
Mvurugano
kwenye Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki (EAC) unazidi kushika kasi,
baada ya muungano wa kimsimamo wa nchi za Tanzania na Burundi kuanza
kuleta tishio kwa nchi tatu wanachama wa jumuiya hiyo zinazodaiwa
kuanzisha mchakato wa siri wa kijitenga.
Hofu hiyo imetokana na tamko la hivi
karibuni lililotolewa na nchi ya Burundi kwamba inaunga mkono msimamo wa
Tanzania kwa kutotambua `utatu' ulioanzishwa na nchi za Uganda, Kenya
na Rwanda.
Habari kutoka vyanzo vya kuaminika,
vinasema tayari viongozi wa nchi ya Rwanda wameanza kuwatuhumu viongozi
wa Burundi kwa kitendo hicho, wakieleza kinavunja udugu uliokuwapo kati
ya wananchi wa nchi hizo mbili.
Wiki iliyopita Waziri wa Afrika Mashariki
wa Burundi, Leontine Nzeyimana, wakati akizungumza na NIPASHE alisema
wazi nchi yake haitambui mikutano yote iliyofanywa na viongozi wa nchi
hizo kwa sababu imefanyika kinyume na makubaliano ya EAC.
Waziri Nzeyimana aliweka wazi kwamba hata
miradi iliyokubaliwa kuanzishwa wakati wa mikutano hiyo ni batili na
kamwe haitaingizwa kwenye jumuiya kutokana na kutoshirikishwa kwa nchi
zote tano wanachama.
Kutolewa kwa kauli hiyo ilionekana kuwa
mwiba mkali kwa nchi hizo, ambapo haraka viongozi wa Rwanda
waliwasiliana na Burundi na kuwataka wasiegemee upande wa Tanzania kwa
sababu nchi hiyo ina nia mbaya ya kuwagombanisha.
Taarifa hizo zinasema kwenye mawasiliano
hayo ya siri, viongozi wa Rwanda walionyesha msimamo mkali wa kuitenga
Tanzania na kuwaomba wabadili msimamo wao na wajiunge kwenye umoja wao.
"Rwanda iliilalamikia Burundi kwa nini
imeungana na Tanzania, wakisema nchi hiyo inataka kuwatenganisha udugu
wao wa damu, hivyo kuwaunga mkono ni kama kuwasaliti," kilisema chanzo
hicho.
Hata hivyo, uongozi wa Burundi ulionyesha
msimamo wa kutokubaliana na malalamiko hayo kwa kueleza wanachoamini
nchi hizo tatu hazikufuata utaratibu wa EAC, kamwe haitakuwa tayari
kuingia kwenye makosa hayo.
Akizungumzia suala hilo kwa njia ya simu
kutoka Bujumbura, Waziri Nzeyimana alisema alichofanya ni kuondoa
sintofahamu iliyokuwapo baada ya nchi hizo kuihusisha Burundi katika
'utatu' walioanzisha.
Alisema hakuna jambo la kuwasaliti
lililofanyika, badala yake amewakumbusha nchi wanachama kufuata
makubaliano na itifaki zilizowekwa katika kusimamisha jumuiya.
"Hatujawatosa (Rwanda) kama wanavyodai
kilichofanywa na nchi hizo ni makosa makubwa na sisi kama nchi
inayopenda sheria tunapinga na kuieleza dunia kwamba hatukushiriki na
hatutashiriki katika umoja wao," alisema Nzeyimana.
Alisema katika vikao vilivyofanywa na nchi
tano wanachama waliweka njia ya kufikia masuala mbalimbali ikiwamo
Shirikisho la kisiasa, ambalo kwa sasa viongozi hao wamekubaliana
kuanzisha kwa haraka.
"Tulikubaliana wote kwamba tuanze hatua
kwa hatua hadi kufikia shirikisho, lakini tunasikia wenzetu wameanza na
kuandaa rasimu ya katiba, hili ni jambo la kushangaza," aliongeza
kusema.
Katika makubaliano hayo, nchi hizo
zilikubaliana kuanza kushirikiana kwanza kwenye umoja wa soko la pamoja,
umoja wa forodha, umoja wa fedha na sarafu na hatimaye kuja kwenye
Shirikisho la kisiasa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Nzeyimana, bado
hali haijatengemaa katika masuala hayo ya mwanzo, hivyo kuna haja ya
kuimarishwa kabla ya kukimbilia kuwa na shirikisho moja la kisiasa.
Akizungumzia suala hilo, Naibu Waziri wa
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Abdullah Juma Sadallah alisema bado
anaunga mkono kauli ya Burundi kwa kuonyesha msimamo imara wa
kuimarisha EAC.
Alisema kinachofanywa na nchi hizo ni
kutaka kurudisha nyuma juhudi zilizochukuliwa na viongozi waliotangulia
za kuziunganisha nchi hizo kwa maslahi ya wananchi wa kila nchi husika.
"Hatutaki kurudi kama huko nyuma, lakini
ieleweke msimamo wa Burundi unataka kuimarisha jumuiya, tunawaunga mkono
na wanaolalamika watakuwa na mambo mengine," alisema Dk. Sadallah.
Bado alisisitiza nchi hizo mbili
hazitakubaliana na namna yoyote ya kutumia nguvu kuwashurutisha
kukubaliana na mambo yaliyoundwa nje ya EAC.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI