Friday, 18 October 2013

Nikioa tena sifanyi sherehe, asema mume wa marehemu


Na Daria Erasto, Mwananchi

Posted  Ijumaa,Oktoba18  2013  saa 11:40 AM
Kwa ufupi
Hassan alisema anahofia kufanya tena sherehe kubwa wakati wa harusi, kwa sababu   tukio la kufiwa na mkewe katika sherehe bado liko katika akili yake na anadhani halitafutika.


Kauli hiyo inatokana na kifo cha mkewe kilichotokea wakati wakijianda kwa sherehe
Dar es Salaam. Mkazi wa Ilala  Amani Hassan(44) aliyefiwa na mkewe siku ya sherehe ya kwenda kumchukua, amesema kama ataoa tena, hatafanya sherehe .
Akizungumza na gazeti hili Hassani alisema bado yuko kwenye majonzi ya kumpoteza mkewe mpendwa Mwanahamis Said.
Alisema kama binadamu anaweza kuamua tena kumtafuta mwenza katika  maisha kwa sababu  bado anahitaji kuwa na familia.
“Mimi ni muumini wa dini ya kiislamu, siwezi kujitoa kwenye ndoa, nasubiri arobaini, ikiisha ntajua cha kufanya,” alisema.
Hassan alisema anahofia kufanya tena sherehe kubwa wakati wa harusi, kwa sababu   tukio la kufiwa na mkewe katika sherehe bado liko katika akili yake na anadhani halitafutika.
Mwanahamisi Saidi alifariki dunia saa  kadhaa kabla ya kupelekwa kwa mumewe baada ya kufunga ndoa,  hali iliyolazimu shughuli nzima ya sherehe ya harusi kugeuka msiba.
Tukio hilo la kuhuzunisha  na lililoacha gumzo katika maeneo ya Ilala na hasa Mtaa wa Arusha na ile ya jirani, lilitokea Jumapili iliyopita.
Bibi harusi  alipaswa  kuchukuliwa na mumewe kwenda nyumbani kwake baada ya kufunga ndoa Ijumaa iliyopita.
Mwanahamis aliaga dunia katika Hospitali ya Amana, baada ya kuugua ghafla na habari zilisema katika hospitali hiyo, wataalamu  walibaini kuwa alikuwa amepungukiwa na damu.
Hassani alisema alikuta na Mwanahamisi  mwaka 2012, wakati binti huyo akiwa  katika hatua  za kuachana na mwanaume aliyekuwa akiishi naye kwa takribani miaka minane.
Alisema baada ya kuachana na mwanaume huyo, alimshawishi waishi wote na baadaye maisha yao yakaanza.

“Baada ya kuishi bila ndoa kwa takribani mwaka, tukaamua tufunge ndoa, nakumbuka ilikuwa mwezi wa tatu mwaka huu  niliamu kwenda kwa kaka yake Bagamoyo kutoa barua ya  posa, kaka yake akaikubali,” alisema.
Alisema katika kipindi chote cha maandalizi hali ya mkewe ilikuwa nzuri, isipokuwa wiki mbili kabla ya harusi.


SOURCE: MWANACHI