Na Mwandishi Wetu, AFP
Posted Jumanne,Oktoba1 2013 saa 10:39 AM
Posted Jumanne,Oktoba1 2013 saa 10:39 AM
Kwa ufupi
Wafanyakazi katika vitengo mbalimbali vya
serikali nchini humo waliodamkia maofisini leo alfajiri wamejikuta
wakirudishwa majumbani, huku karibu 800,000 kati yao wakiambiwa wachukue
likizo bila malipo mpaka muafaka utakapopatikana.
Washington. Kwa mara ya kwanza
ndani ya miaka 17, utawala wa Rais Barack Obama umeidhinisha baadhi ya
shughuli za kiserikali zisimamishwe kuanzia mapema leo baada ya Bunge
la nchi hiyo kuikataa bajeti yake, wakipinga mabadiliko ya kisheria ya
sekta ya afya yaliyofanyika hivi karibuni.
Huku matumaini ya suluhisho la mtafaruku huo wa
bajeti unaopambanisha wabunge wa chama tawala cha Democrat dhidi ya
Republicans yakizidi kufifia, wachumi na wataalamu wa uongozi wameonya
kuwa uamuzi wa kusitisha huduma ‘zisizo muhimu’ utaathiri uchumi wa
Marekani kwa kiwango kikubwa.
Wafanyakazi katika vitengo mbalimbali vya serikali
nchini humo waliodamkia maofisini leo alfajiri wamejikuta wakirudishwa
majumbani, huku karibu 800,000 kati yao wakiambiwa wachukue likizo bila
malipo mpaka muafaka utakapopatikana.
Wafanyakazi pekee watakaobakizwa ni wale ambao
shughuli zao haziwezi simama, kama vile madaktari na manesi, waongoza
ndege na wafanyakazi wa shirika la posta la Marekani.
Katika baadhi ya vitengo kama NASA – inayofanya
tathmini za usafiri wa kwenda sayari nyingine na anga za mbali – zaidi
ya asilimia 95 ya wafanyakazi wote wamewekwa benchi katika kipindi hiki
cha mtafaruku wa bajeti.
Vilevile huduma za utoaji hati za kusafiri na viza
zinatarajiwa kusimama kwa kiwango kikubwa, na wasafiri toka nchi
nyingine wanaambiwa watarajie foleni ndefu kidogo katika vituo vya
uhamiaji kwa sababu wafanyakazi wengi wa kitengo hicho wamepumzishwa. (AFP)
SOURCE: MWANANCHI