Thursday, 24 October 2013

Ripoti: Watanzania waongoza kwa hofu ya uhalifu



Posted  Alhamisi,Oktoba24  2013  saa 24:0 AM
Kwa ufupi
Imebainika kuwa, asilimia 42 ya watu waliofanyiwa vitendo vya kihalifu kati ya mwaka 2011 na 2012, ndiyo waliotoa taarifa polisi huku ikielezwa kwamba wanaume ndiyo wanaoongoza kwa kutoa taarifa hizo polisi.

Dar es Salaam. Utafiti mpya umebaini kuwa, Watanzania wanaongoza katika Afrika kwa kuwa na hofu ya kutendewa matukio ya kihalifu katika nyumba zao kutokana na kupungua kwa usalama hapa nchini.
Hayo yalibainika kwenye majibu ya utafiti uliotolewa jijini Dar es Salaam jana na Taasisi ya Utafiti kuhusu Kuondoa Umaskini (Repoa), ambao unaonyesha kuwa asilimia 40 ya wananchi 2,400 waliohojiwa wana hofu ya kufanyiwa uhalifu na kuifanya Tanzania kuwa kinara kati ya nchi 34 zilizofanyiwa utafiti huo.
Nchi nyingine zilizopo katika tano bora ni; Afrika Kusini asilimia 38, Cameroon (37), Liberia (35) na Swaziland asilimia 34.
Ripoti hiyo iliyoandaliwa kati ya Mei hadi Juni, 2012, kwa kushirikiana na asasi ya Afrobarometer ililenga kuchunguza hali ya uhalifu nchini na utayari wa wananchi kutoa taarifa za kihalifu kwa polisi.
Akiwasilisha ripoti hiyo, Mtafiti Msaidizi wa Repoa, Rose Aiko alisema kuwa vitendo vya watu kujeruhiwa kutokana na uhalifu vimeongezeka nchini na idadi ya watu walzojeruhiwa imeongezeka kutoka asilimia 10 mwaka 2003 hadi asilimia 44 mwaka 2012.
“Utafiti unaonyesha kuwa matukio ya mtu mmoja mmoja kupigwa na kujeruhiwa yameongezeka, huku wizi katika nyumba nao umeongezeka kutoka asilimia 22 mwaka 2005 hadi asilimia 36 mwaka 2012,” alisema Aiko.
Akifafanua namna ambavyo watu wana hofu ya kuibiwa kwenye nyumba zao, Aiko alisema kuwa vitendo vya kihalifu viliongezeka kuanzia mwaka 2008 na mwaka 2003 kulikuwa na matukio mengi kwa asilimia 48, lakini mwaka 2005 yalipungua hadi kufikia asilimia 34.
Hata hivyo, vitendo hivyo viliongezeka tena na kufikia asilimia 43 mwaka 2012.
Pia utafiti huo umebainisha kuwa ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki, Tanzania ina asilimia 32 ya watu waliowahi kuibiwa nyumbani, huku ikiwa na asilimia 26 ya watu hao katika Afrika.
Imebainika kuwa, asilimia 42 ya watu waliofanyiwa vitendo vya kihalifu kati ya mwaka 2011 na 2012, ndiyo waliotoa taarifa polisi huku ikielezwa kwamba wanaume ndiyo wanaoongoza kwa kutoa taarifa hizo polisi.
“Utafiti unaonyesha kuwa wanawake ni waoga zaidi wa matukio ya kihalifu ingawa imebainika kuwa sio wengi wanaokumbwa na matukio hayo. Hata hivyo, imebainika kuwa wengi wapo tayari kuripoti polisi taarifa za kuibiwa kuliko kupigwa,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.
Mtafiti Mwandamizi wa Repoa, Dk Abel Kinyondo alisema kuwa asilimia 18 ya waliohojiwa walisema hawakupeleka taarifa za uhalifu polisi kwasababu vituo vipo mbali, asilimia 15 walisema polisi wana tabia ya kutokusilikiza shida zao, asilimia 14 walisema polisi wangetaka rushwa huku asilimia 12 walisema walitoa taarifa kwa viongozi wengine walio karibu yao.

“Asilimia saba walisema hawana muda wa kwenda kuripoti polisi, asilimia saba walisema waliogopa watu waliowajeruhi wangeweza kuwatafuta tena wakati asilimia tano walisema polisi wasingefanya chochote,” alisema Kinyondo.
Afisa Mnajimu Mipango na Bajeti, Jeshi la Polisi, Beatus Silla alisema uelewa wa wananchi kuhusu namna huduma za polisi zinavyoendeshwa umechangia baadhi yao kushindwa kwenda polisi kutoa taarifa za kihalifu.
“Huduma za polisi ni bure, hakuna gharama zozote na hilo tumelitangaza kwenye mabango katika vituo vya polisi, namba za polisi pia zimetolewa ili kama mtu ana mashaka atoe taarifa,” alisema Silla.
Akizungumzia malalamiko kuwa polisi hawawajali wananchi wanapokwenda katika vituo kutoa taarifa mbalimbali, Silla alisema: “Kuna dawati ambalo linashughulikia malalamiko kwa wadau wa ndani ambao ni polisi wenyewe na wale wa nje ambao sisi tunawajibika kwao.”
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Profesa Samwel Wangwe alisema utafiti huo unaonyesha kuwa Tanzania ipo katika wastani wa kati katika uhalifu Afrika, ingawa watu wengi wameonyesha hofu na kutokuwa na amani na kushauri kufanyika marekebisho katika Jeshi la Polisi.
“Kitaalamu inamaanisha kwamba, tuangalie vizuri yale maboresho ya polisi na kwamba tufanye nini ili yafanye kazi zaidi. Pili, utafiti wa sasa haukuingia ndani kueleza kufanye nini na sababu ni nini,” alisema.
Kwa upande wake, Profesa Amoni Chaligha kutoka Idara ya Siasa na Utawala Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema kuwa utafiti huo unapinga na hali ilivyo mitaani kwa kuwa zipo baadhi ya nchi katika Afrika zinazofahamika kwa kuwa na kiwango kikubwa cha uhalifu kuliko Tanzania, lakini ama hazipo au zimewekewa asilimia ndogo.
“Sijui kwanini data zinaonyesha kuwa ipo katika hali hiyo kwa sababu ukienda katika miji mingine kama Johannesburg, Afrika Kusini hali ya uhalifu ni mbaya zaidi na hata wakati wa Kombe la Dunia, 2010 ilielezwa zaidi hali hiyo, lakini inashangaza kuona kama vile tupo sawa,” alisema Chaligha.
Chaligha alihoji pia: “Kinachowafanya watu kuwa na hofu ya uhalifu, ni kwa sababu wanasikia sana habari hizo kwenye vyombo mbalimbali vya habari?”

SOURCE: MWANANCHI