Mwaka
1945 kijana mmoja alikuwa anakaribia kuhitimu masomo yake katika chuo
Kikuu cha Makerere huko Uganda akichukua shahada ya kwanza ya Elimu
iliyomruhusu kuendelea na taaluma ya ualimu mara baada ya kutoka chuo
katika mwaka huo huo. Lakini ilikuwa ni wakati huu akikadiriwa kuwa na
umri wa miaka 23 alipoanza kuungana na wenzake wengine kuanzisha
harakati za chini kwa chini. Hapana shaka kwa umri huo alikuwa ni kijana
mdogo sana kiasi cha kuwa na ndoto nzito za kushiriki na wengine
kuanzisha chama cha TAA (Tanganyika African Association) ili kiweze kuwa
chachu na sehemu ya mapambano ya kuifanya nchi yake ya nyumbani kuwa
huru kutoka katika ukoloni wa Mwingereza. Ilimchukua miaka kadhaa yeye
na vijana wengine kuendelea na harakati ambazo baadaye zilizaa matunda.
Lakini ni wazi haikuwa rahisi sana. Najaribu kuelewa kuhusu ari
ambayo alikuwa nayo yeye na wengine wakati huo, hasa ile dhamira ya
kwamba kuna jambo moja kubwa linapaswa kufanyika tena kwa gharama hasa.
Wengi wanajua haiwezekani mtu mmoja kufanya yote na kuwa shujaa kama
walivyo mashujaa wa kwenye filamu ambao hawashindwi kitu. Historia
inatueleza kuhusu wazee wengi wa maeneo tofauti walivyompokea kijana
huyu mwenyeji wa Uzanaki na kumkaribisha miongoni mwao na kumpa msaada
mkubwa ili kufikia yale malengo ya kuifanya Tanganyika kuwa huru.
Huyu ni Julius Kambarage Nyerere ambaye mwaka 1953 alichaguliwa kuwa
raisi wa chama cha TAA ambapo mwaka mmoja baadaye walikigeuza na kuwa
chama kamili cha siasa TANU (Tanganyika African Nation Union) chenye
lengo la kutimiza azma ya kuifanya Tanganyika iliyokuwa chini ya utawala
wa Waingereza wachache kuwa nchi huru yenye kutoa nafasi kwa watu wa
rangi zote kufurahia uhuru na kujitawala. Baada ya mageuzi hayo TANU
ikawa chama maarufu miongoni mwa wananchi wa wakati huo, kikipendwa na
kukubalika na wengi.
Wakati mambo yakiendelea katika Umoja wa Mataifa mwaka 1954, suala
kuhusu uhuru wa Tanganyika na namna wazalendo walivyokuwa wameamka
katika kudai uhuru lilikuwa miongoni mwa ajenda ambazo zilizungumzwa.
Jopo la wakaguzi kutoka UM likatumwa kuchunguza hali ya mambo na kujua
utayari wa Tanganyika kuwa huru, lakini likiondoka na kushauri mpango wa
miaka ishirini mpaka ishirini na tano kwa kulifanya taifa liwe huru.
Kwamba Tanganyika haikuwa tayari.
Bila shaka habari hizi hazikuwapendeza
miongoni wa wote waliokuwa na kiu ya kujitawala. TANU wakapiga kura na
kuamua kumtuma kijana wao Julius Nyerere kwenda kuhutubia katika baraza
la UM kuelezea azma iliyokuwa inafukuta katika mioyo ya waTanganyika ya
kutaka uhuru. Lakini kwa maombi ya serikali ya Uingereza basi Marekani
ikaweka vikwazo kumzuia Nyerere kufanya kwa ukamilifu kile
kilichompeleka UM ikiwemo kumtaka aondoke haraka mara tu baada ya
kuhutubia hadhira ya Umoja wa Mataifa.
Haidhuru kama hayo yote yalitimia kwa matakwa yao lakini cha msingi
kijana alifanya kazi yake na lililo kubwa zaidi ni kwamba uhuru
ulipatikana licha ya mizengwe yote hiyo. Hii ilikuwa ni miaka kadhaa
iliyopita ambayo ilijenga historia ya Tanganyika na baadaye Tanzania.
Ilikuwa ni wakati ambapo vijana waliendesha serikali, waliendesha chama
na kwa kiasi kikubwa walishika usukani katika nyanja nyingi.
Jambo linalonivutia kwa yakini ni vile ambavyo wazee wa wakati huo
walipotumia hekima kubwa sana, lakini pia ujasiri wa kuweka matumaini
yao kwa vijana. Wakiamini na kutoa msaada mkubwa ili vijana waweze
kutimiza azma yao na kuikomboa nchi na pia kuindesha. Hili halikutokea
tu Tanzania bali mahali pengi katika Afrika. Vuguvugu la ukombozi wa
bara la Afrika lilishamiri sana na mapambano yalipata nguvu kwa kuwa
vijana waliamka na walikuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa jamii yao
inakuwa huru. Kwa jasho na damu Afrika ilikombolewa, japo kwa uhuru wa
bendera na kujitawala kwa kinadharia kama ambavyo tunaweza kushuhudia
leo. Wapo walioishia ama kuteseka katika magereza ya wakoloni na
watawala kama ilivyotokea kwa Nelson Mandela, Oliver Tambo, Walter
Sisulu na wengineo ama waliouawa kabisa kama Steve Biko, Thomas Sankara,
Patrice Lumumba na wengine. Haidhuru kama waliuawa kwa silaha yoyote
ama risasi zilifyatuliwa kutoka katika viwambo vya bunduki zilizokuwa
mikononi mwa weusi wenzao lakini inaeleweka kuwa kama si mapambano yao
bila shaka, umauti usingewakuta katika hali hiyo.
Leo miaka kadhaa baada ya mapambano haya ya ukombozi, lakini vita
bado haijaisha. Mapambano kwa vijana bado hayajaisha. Ukweli ni kuwa
uhuru umepatikana kwa jasho na damu ambalo vijana walitoa na kwa msaada
mkubwa wa hekima za wazee lakini mapambano yaliyobaki sasa ni ya
kitabaka na kiu ya kutafuta usawa miongoni wa jamii zilizo huru za
kiafrika. Inashangaza sana mara nyingine kuona ni kwa vipi hali ya mambo
iligeuka na kufikia shime kwamba vijana ni taifa la kesho.
Lakini baadaye watu wakijikosoa kwa kubadili msemo pasipo kubadili
muktadha mzima na kuanza kutia hamasa kwamba vijana ni taifa la leo. Leo
ambayo haipo. Inastaajabisha sana kuona mustakabali wa vijana
unavyokuwa na mashaka mengi. Nafasi ya vijana ni kama haipo ama
haieleweki kabisa katika mchakato mzima wa ujenzi wa jamii iliyo na
usawa na haki. Imezoeleka kwa namna ambavyo watu wamekuwa kwa vipindi
tofauti wakikejeli vile ambavyo kwa kipindi kirefu ni majina ya watu
wale wale yamekuwa yakijirudia katika duru za kiuongozi na kisiasa.
Hata
ilifika mahali ambapo imesemwa kuwa tangu kuzaliwa mpaka mtu anafikia
umri wa utu uzima anaweza kubashiri nafasi ambayo mtu fulani anaweza
kushika katika uongozi katika serikali nyingi za kiafrika na Tanzania
hususani.
Hoja kuu ni kwamba vijana hawapo tayari ama hawajaiva ili kuweza
kushika madaraka. Hii inashangaza sana kwa sababu ikiwa miaka ambayo
mapambano ya uhuru yalishamiri, ilikuwa ni vijana waliosimama katika
majukwaa ama katika maandamano ama ni Mau Mau waliotoka msituni
kuendeleza harakati za kujikomboa. Inakuwaje leo hii vijana wanapotea
kwa hoja ya kwamba wanahitaji muda kuweza kuiva na kuwa tayari. Lakini
kukiwa hakuna mipango madhubuti ya kuwafanya vijana waweze kujijenga na
kutambua nafasi yao katika jamii.
Ni rahisi sana kuonyesha upande mwingine wa vijana unaowaonyesha kama
kizazi kisichokuwa na mwamko katika kujiendeleza na kuendeleza jamii
yao, kwa sababu tu hatupo tayari kutambua jitihada mbalimbali
zinazofanywa na makundi ya vijana ama kwa makusudi ama kwa kukosa
dhamira. Katika jamii ambayo kiwango cha elimu kimeporomoka, ambapo
hakuna mfumo unaoeleweka wa kuwaandaa vijana huwezi kutegemea kuwa na
kizazi chenye kueleweka pia. Ikiwa kwa miaka kadhaa vijana wakipiga debe
na kusisitiza umuhimu wa kuwa na baraza la vijana kama chombo
kitakachowaunganisha kitaifa lakini madai hayo yakiwekwa kapuni, bado
hatuoni dhamira ya kweli ya kuwafanya vijana waweze kutimiza azma yao
hiyo.
Nyakati za sasa zimewagawa sana vijana katika makundi tofauti ya
kiitikadi pasipo kuwa na mfumo mmoja wenye kueleweka wa kuwaendeleza na
kutumia ipasavyo nguvukazi yao ili kusukuma mbele maendeleo ya taifa ama
mataifa mengi ya kiafrika.
Ikiwa vijana ni sehemu kubwa ya jamii na bado sehemu hiyo kubwa
inakosa nafasi ya kueleweka, jambo hili si ishara njema hata kidogo.
Tulizowea kusikia kuwa ili kuendelea tunahitaji watu, siasa safi na
uongozi bora. Sijui ni lipi kati ya haya matatu linatumika ipasavyo,
‘siasa safi, ‘uongozi bora’ na ‘watu.’ Watu hususani vijana, wako wapi
leo hii ili kutufanya tuendelee ikiwa kwa nyakati zote tunapata kuwa na
sura zilezile katika nyanja nyingi za kiuongozi. Hii ni kwa kuwa ‘hawapo
tayari’ na pia ‘vijana wa sasa si kama wa zamani’ kwa sababu ‘vijana wa
sasa wanaendekeza sana starehe kuliko kazi.’ Tumesikia sana kauli hizi.
Ni kweli huwezi kufananisha vijana wa sasa na vijana wa zamani kwa
sababu kadhaa. Mojawapo ni kuwa vijana wa zamani walipata kuungwa mkono
sana na wazee ambao kwa makusudi waliweza kuwekeza kwa vijana wao
ikiwemo kujenga misingi iliyo imara lakini pia wakijua kwamba vijana
wanafahamu mengi na ni wepesi kukabili upinzani na mabadiliko ya
kijamii. Hivyo hapa tunarudi nyuma na kutazama ni kwa kiasi gani vijana
wa sasa wamejengewa misingi inayowawezesha kusimama na kutumia nafasi
zao vizuri.
Wakati nilipokuwa mkoani Shinyanga jioni moja, tulikuwa watu wengi
wapatao thelathini tumezunguka katika moto uliokuwa umekokwa na mzee
mmoja wa kijiji. Moto huu unafahamika kama shikome, ama kikome maalum
kwa kuwaweka vijana na wazee pamoja ili kujadili na kwa nyakati za
zamani wazee kutoa maelekezo na maonyo kwa vijana. Lakini siku hiyo ni
vijana waliomba moto huo kukokwa kwa kuwa kabla yake tulijadili sana
kwanini mila hii ilipotea, bahati njema mzee mmoja aliridhia kuandaa
tukio hilo hasa kwa kuwa vijana wengi hawakupata kulishuhudia zaidi ya
kusikia tu habari zake.
Wakati wa maongezi wazee walielekeza sana lawama zao kwa vijana
kwamba si wasikivu na wanakiuka misingi ya mila ambayo wao waliiheshimu
na kwamba iliwakuza na kuwafanya kuwa wenye nidhamu. Lakini vijana
walijibu kwa kuhoji ni nani anapaswa kulaumiwa ikiwa moto wa shikome
ulizimwa na ilikuwaje wao hawakupata kuushuhudia mpaka walipoomba siku
hiyo. Ni wazi kwamba wazee waliacha, hivyo vijana hawakuwa na uwezo wa
kulinda mila ambayo iliharibiwa na wazee. Ilikuwa ni hoja ya msichana
mmoja mdogo iliyohitimisha mjadala alipohoji, vijana wanaweza kufanya
nini ama kupata wapi wasaa wa kuongea na wazee kama wazee hao wanatumia
muda mwingi kujijali wenyewe, kukaa na kupiga soga kilabuni huku
wakirejea usiku wakati watoto wameshalala.
Kwa namna hii pia, kizazi fulani kimeamua kulala kwa makusudi na
kusahau kutoa nafasi kwa vijana kujiimarisha na kujifunza na zaidi
kuchangia nguvu yao katika ujenzi wa jamii iliyo bora zaidi. Wanaobadili
mitaala ya elimu si vijana. Hata baadaye tunaanza kubishana kama kweli
kuna mitaala ama mihutasari tu katika mfumo wetu wa elimu. Napata shaka
kuamini kama ni vijana ndio wanashusha kiwango cha ufaulu ama kubinya
fursa zilizopo katika jamii.
Kwa namna moja ama nyingine tunakumbatia ukoloni mamboleo na kuruhusu
bila kuchuja mifumo mipya ya maisha ya utandawazi-wizi ambayo inaathiri
mila zetu na kukiacha kizazi cha sasa bila kuwa na mwelekeo
unaoeleweka. Si kwamba jamii ya vijana imeharibika kabisa, lakini
tunapolaumu kuwa suruali zinashushwa chini ya makalio tunapaswa
kuangalia ni nini tunachowaonyesha vijana katika runinga zetu katika
kile tunachoita uhuru wa kupata habari. Uhuru wa kupata habari usio na
mipaka katika kutambua athari za utandawazi na ukoloni mamboleo lakini
kwa habari za maana ukiwa umejaa ukakasi ni jambo lisiloeleweka.
Sasa tunakuwa na kizazi cha vijana waliohitimu kupiga debe. Kutoka
kizazi cha vijana waliokuwa mstari wa mbele katika kupigania ukombozi wa
bara za Afrika mpaka kufikia kizazi cha vijana wanaoshinda vijiweni,
bila shaka kuna mahali tumekosea, na mbaya zaidi tunaendelea kukosea,
ama kwa bahati mbaya ama kwa kujua.
Na: Churchill Shakim
Churchill ni mwanaharakati wa masuala ya vijana na muziki wa asili ya HipHop.Anafanya kazi na shirika la TAMASHA.
*Mawazo katika makala hii ni yake binafsi na si msimamo au mtizamo wa shirika la TAMASHA.
imenakiliwa kutoka kwenye tovuti ya wewrite.or.tz