Friday, 18 October 2013

Tusikubali `wauza unga` kuichafua Tanzania ughaibuni

18th October 2013
Taarifa kwamba kuna Watanzania 175 wanaoshikiliwa katika magereza tofauti nchini China baada ya kukutwa na makosa mbalimbali yakiwamo ya kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya si nzuri kwa taifa letu. Zinaichafua Tanzania.


Waziri Mkuu Mizengo Pinda ndiye aliyepewa taarifa hiyo ya kustusha wakati alipotua China juzi kuanza ziara yake ya kikazi. Alihuzunishwa sana.

Kwa mujibu wa Balozi wa Tanzania nchini China, Watanzania hao wamefungwa katika maeneo mbalimbali ya China, yakiwamo ya Hong Kong, Macao na China Bara.

Mbaya zaidi, waliokamatwa wala si watu wa jinsia moja, siyo vijana wa kiume pekee kama ilivyozoeleka. Bali, wapo pia wanawake ambao idadi yao ni kubwa sana kiasi cha kumshangaza hata Waziri Mkuu Pinda.

Alipokuwa akielezea suala hilo, Pinda alisema idadi ya watuhumiwa hao kutoka katika nchi moja pekee, hasa yetu ya Tanzania, ni kubwa sana. Inalitia aibu taifa hili ambalo wasifu wake kimataifa umekuwa ni wa kupigiwa mfano kwa miaka mingi.

Sisi pia tunaamini kuwa idadi hiyo ni kubwa, hasa kwa kujua kuwa idadi hiyo ni ya nchi moja tu ya China na haihusishi Watanzania wengine wanaoshikiliwa katika mataifa kama ya India, Pakistani, Saudi Arabia na kwingineko duniani.

Ni taarifa zinazoiharibia Tanzania sifa yake ya miaka mingi mbele ya jumuiya za kimataifa, sifa ya  kuwa taifa lenye watu walioshiba maadili na hivyo kutohusika mara kwa mara na matukio ya uhalifu mkubwa kama wa biashara ya dawa za kulevya.

Hakika, taarifa hizi zinateteresha heshima ya Tanzania. Zinaharibu taswira nzuri mbele ya nchi rafiki kama ya China, ambayo ni miongoni mwa washirika wetu wakubwa wa maendeleo.

Hakuna asiyejua athari za taifa changa kiuchumi kama Tanzania kukumbwa na taarifa mbaya za uhalifu. Mojawapo ya athari hizi ni kushuka kwa kiwango cha uaminifu. Kwa mfano, ni wazi kwamba sasa, maafisa wa usalama katika viwanja mbalimbali vya ndege nchini China watakuwa na ukaguzi wa ziada dhidi ya raia watokao nchini mwetu.

Ni wazi vilevile kuwa hata wafanyabiashara wa Tanzania watakuwa na wakati mgumu China kwani watalazimika kuwashawishi washirika wao kibiashara kuwa wao ni watu safi na siyo miongoni mwa wauzao dawa za kulevya.

Jambo hili linadhihirisha kuwa sasa hali ni mbaya. Kuna kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha kwamba aibu hii inakomeshwa na heshima yetu inalindwa kwa nguvu zote. 
Sisi tunatambua jitihada zinazochukuliwa na serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Tunatambua vilevile mpango wa serikali wa kutaka kuunda chombo maalum kitakachokuwa na nguvu zaidi kisheria, kifedha, kiteknolojia na hata rasilimali watu katika kukomesha janga hili. Ni hatua nzuri.

Hata hivyo, kama alivyosema Waziri Mkuu Pinda, tunadhani kwamba sasa kuna kila sababu ya kuongeza nguvu katika kukabiliana na tatizo hili.

Uzoefu unaonyesha kuwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya si watu wa kada ya chini. Wana ukwasi mkubwa na wamejipanga vya kutosha katika kufanikisha mipango yao mbalimbali, ikiwamo ya kusafirisha 'mizigo' kutoka eneo moja hadi jingine.

Umma unapaswa kuelimishwa kila uchao kuhusiana na madhara ya dawa za kulevya. Na hii inapaswa kuwa kampeni endelevu. Wananchi, hasa vijana waelimishwe vilevile juu ya hatari ya kujihusisha na biashara hii.
Kwa mfano, waambiwe kuwa wanapokamatwa katika baadhi ya nchi kama China, adhabu yake huwa kali ikiwa ni pamoja na vifungo virefu gerezani au hata kunyongwa.

Ulinzi katika maeneo ya viwanja vya ndege uimarishwe. Watumishi wanaohusika na ukaguzi katika maeneo hayo wapewe mafunzo zaidi ili kukabiliana na mbinu mpya zinazoibuka kila mara za kupitisha 'unga'; wapewe vitendea kazi vya kisasa na pia wafuatiliwe kwa karibu ili kuona kuwa hawapokei rushwa na kuwa sehemu ya mitandao hatari ya biashara za dawa ya kulevya.

NIPASHE tunaamini vilevile kuwa njia nyingine nzuri ya kukomesha biashara hii ni kuwafikisha mahakamani wale wote wanaokamatwa na pia kuendesha upelelezi makini utakaorahisisha mchakato wa kupatikana kwa haki mbele ya mkono wa sheria.

Shime, tukatae jina la Tanzania kuchafuliwa nje ya mipaka yetu kwa kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya.


 
CHANZO: NIPASHE