Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Posted Jumatatu,Novemba4 2013 saa 8:10 AM
Posted Jumatatu,Novemba4 2013 saa 8:10 AM
Kwa ufupi
Makamba ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu
(NEC) ya CCM alisema: “Kwanza ni kweli kwamba kuna ushawishi kuhusu
suala hilo kutoka kwa vijana walioko nje na ndani ya chama, wanataaluma,
baadhi ya wazee na watu wengine iwe kwa makundi au mtu mmoja mmoja
wamekuwa wakinishawishi kugombea kwa muda sasa.”
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba amesema kuwa anatafakari iwapo awanie urais
katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, kutokana na kuwapo kwa watu wengi hasa
ndani ya CCM, wanaomtaka kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
Makamba ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu
(NEC) ya CCM alisema: “Kwanza ni kweli kwamba kuna ushawishi kuhusu
suala hilo kutoka kwa vijana walioko nje na ndani ya chama, wanataaluma,
baadhi ya wazee na watu wengine iwe kwa makundi au mtu mmoja mmoja
wamekuwa wakinishawishi kugombea kwa muda sasa.”
Aliongeza: “Mwanzoni sikuona uzito sana, yaani
sikuzingatia sana, lakini kwa kadiri siku zinavyokwenda ni kwamba
ushawishi umekuwa mkubwa na hivyo niseme ni jambo ambalo sasa
ninalitafakari kwa kina”.
Alisema ikiwa ataamua kuwania urais, atafanya
hivyo wakati mwafaka kwa kuzingatia utaratibu utakaowekwa na chama
hicho, lakini akasema kwa sasa si wakati wake. Makamba alikuwa akijibu
hoja za gazeti hili lililotaka ufafanuzi wake kutokana na kuwapo kwa
taarifa kwamba ameanza harakati za kuusaka urais katika Uchaguzi Mkuu wa
2015.
Gazeti hili lilidokezwa kuwa hatua yake hiyo
imemwingiza katika mvutano usio rasmi na wanasiasa ambao tayari
wameonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini,
wakiwamo wale wa kambi ya urais aliyokuwa akidaiwa kuwa mmoja wao.
Awali iliaminika kuwa Makamba alikuwa katika kambi
ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini wachambuzi wa masuala
ya kisisa wanasema ‘katika siku za karibuni mwenendo wake unaashiria
kwamba si mmoja wa wanaomuunga mkono kiongozi huyo, bali ni mtu mwenye
mipango yake binafsi ya kisiasa”.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema
mwenendo wa Makamba umewakasirisha baadhi ya wanasiasa hususan
wanaomuunga mkono Lowassa ambao mara kadhaa wamesikika hadharani
wakimlalamikia kwamba ni msaliti.
Hata hivyo, Makamba katika maelezo yake anasema
hajawahi kuwa katika kundi lolote la kumuunga mkono mtu yeyote kwani
yeye haamini katika makundi. “Ninaamini katika kundi moja, nalo ni CCM,”
alisema.
Aliongeza: “Kwa hiyo mtu yoyote akinikasirikia kwa
sababu zozote zile za kisiasa nitamshangaa maana sijawahi mahali popote
na kwa namna yoyote kujitanabaisha kwamba mimi nipo kwenye kundi
fulani, au kundi la mtu yeyote.”
Sababu za mashaka
Miongoni mwa nyedo zinazotiliwa shaka za
mwanasiasa huyo ni hatua yake ya kushiriki katika Mkutano Mkuu Maalumu
wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) uliofanyika Zanzibar ambako pamoja na
mambo mengine aligawa simu zaidi ya 100 aina ya Samsung Galaxy kwa
wajumbe wa mkutano huo.
Imethibitika kwamba mpango huo ulikuwa ni wake
binafsi na haukuwashirikisha waliokuwa wakiamini kwamba wako naye katika
harakati za kumuunga mkono Lowassa.
Tukio jingine ni lile la vijana waliojitambulisha kuwa viongozi
wa vyuo vikuu nchini kutangaza katika mkutano wao mjini Morogoro kwamba
watamwomba Makamba awanie urais katika Uchaguzi Mkuu ujao, kutokana na
kile walichodai kwamba ni matokeo ya kura walizopiga baina ya kiongozi
huyo na viongozi wengine vijana; John Mnyika na Zitto Kabwe wa Chadema.
Wapinzani wake wanaamini kwamba tamko la vijana
hao zilikuwa mbinu binafsi za Makamba kutaka kuonyesha kwamba naye
anakubalika na pengine maandalizi ya kujiengua rasmi kutoka katika kambi
yake ya awali.
Wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 14 ya
kifo cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Makamba alikuwa Butiama mkoani
Mara ambako mbali na kushiriki Ibada ya kumwombea Baba wa Taifa, pia
alikuwa mgeni rasmi katika kongamano la kumuenzi kiongozi huyo.
Kuhusu baadhi ya makada wenzake kukasirishwa na
mwenendo wake kisiasa, Makamba alisema: “Hata mimi nimesikia kama wewe
unavyosema umesikia, inawezekana wanakasirishwa na mvumo maana ndani ya
chama chetu watu wanazungumza sana, tena hadharani kwa hiyo katika
mazingira hayo taarifa zinaweza kumfikia yeyote kama zilivyokufikia
wewe”.
Alitetea hatua yake ya kugawa simu kwenye mkutano
wa UVCCM akisema alikuwa akitimiza ahadi aliyoitoa wakati wa semina ya
vijana hao Februari mwaka huu mjini Dodoma, pale walipomuomba kuwasaidia
ili waweze kutekeleza matakwa ya ushauri wake wa kukitetea CCM katika
mitandao ya kijamii.
“Mimi kwa nafasi yangu nikiwa Naibu Waziri wa
masuala ya teknolojia, nikiombwa kusaidia lolote katika eneo langu ndani
ya chama sioni tatizo ilimradi niwe na uwezo nalo, kwa hiyo nilitimiza
ahadi yangu tena kwa uwazi sikufanya kwa kificho,”alisisitiza.
Makamba ni mwanasiasa wa tatu kijana kutajwa kuwa
huenda akawania urais, wengine wakiwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Wengine ambao wameishaonyesha nia ya kuutaka urais
ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Lowassa.
Vita ya urais imekuwa ikikiumiza CCM, ambapo
Makamu Mwenyekiti wake (Tanzania Bara), Philip Mangula aliwahi
kukaririwa akiwaonya makada wa chama hicho ambao wameanza kupiga mbio za
kuusaka uongozi huo kuwa hawatavumiliwa, kwani harakati hizo zimekuwa
kichocheo cha mgawanyiko ndani ya chama.
SOURCE: MWANANCHI
SOURCE: MWANANCHI