Thursday, 7 November 2013

'Polisi walinikamata wakinishuku kua gaidi'


 7 Novemba, 2013 - Saa 14:29 GMT

Ali Muhsin Ali
Ali Muhsin Ali, ni mwanafunzi mwenye umri wa miaka 17, nchini Kenya ambaye maisha yake yalitumbukia nyongo, tarehe saba Oktoba.
Polisi waliingia darasani mwao na kumfunga pingu mikononi, kumkamata mbele ya wanafunzi wenzake wakisema kuwa alikuwa mmoja wa watu waliohusika na shambulizi la kigaidi dhidi ya jengo la Westgate.
Alizuiliwa kwa siku kumi na kuchapwa kisha kuachiliwa bila kufunguliwa mashitaka, lakini sio kabla ya jina lake kuhusishwa na shambulizi la kigaidi, kidonda anachohisi hakitawahi kumtoka.
"nilikuwa nasomea mtihani wangu wa Fizikia, wakati watu watatu walipoingia darasani mwetu na mwalimu mkuu, '' aliambia BBC
"kisha waliniweka pingu mkononi na kuniingiza katika gari lao, na kilichonijia akilini ni kuwa huu ndio mwisho wa elimu yangu.''
Anasema kuwa jioni hiyo alichapwa vibaya na polisi bila sababu yoyote ingawa walimtuhumu kuhusika na shambulizi la kigaidi la Westgate.
Manusura wa shambulizi la Westgate Nairobi
Kundi la kigaidi la al-Shabab lilikiri kufanya shambulizi hilo la siku nne ambalo lilisababisha vifo vya watu 67.
"polisi wengine waliniambia kuwa naonekana sina hatia lakini wamenikamata tu kuonyesha kuwa wanafanya kazi kuhusiana na shambulizi hilo. ''
Polisi walikataa kujibu madai hayo walipoulizwa na BBC.
Usiku huo hali iliongezeka kuwa mbaya kwa Muhsin baada ya polisi mmoja kuja na kumtishia kwa bunduki alipokuwa kizuizini.
Nilipigia mayowe akiniuliza nilikoweka maguruneti niliyokuwa nayo pamoja na kumpa majina ya magaidi wengine.
Nilidhani kama ataniua lakini nilimwambia kuwa sina kitu wala simfahamu mtu.
Siku zilizofuata, alihojiwa na polisi wa kupambana na ugaidi ambao baadaye walithibitisha kuwa hana uhusiano wowote na shambulizi la Westgate wala kundi la Al Shabaab.
Lakini alisalia kuzuizini hadi tarehe 16 na kachiliwa kwake haikuwa mwisho mwa masaibu yake.
"waliponiachilia sikuhisi kuwa huru, kwa sababu waliponikamata waliambia watu ninakosoma, jina langu , umri wangu , '' alisema kijana huyo.
Babake Muhsin
Lakini waliponiachilia hawakuambia watu ikiwa walimkamata mtu asiye na hatia.
Kwa hivyo hakuna taarifa ya polisi ilitolewa kuonyesha kuwa sikuwa na hatia.
Kwa bahati nzuri anakoishi katika mtaa wa Pumwani nje kigodogo ya mji, anaishi katika jamii inayomfahamu kila jirani.
Ni eneo masikini lenye barabara mbaya , nyumba mbovu, wengi watahisi mahala hapa kuwa mtaa wa mabanda, lakini kulingana na Muhsin kila mtu hapa ni mchapakazi.
Ali, anasema kuwa hajawahi kukutana na mtu aliyemshawishi kujihusiaha na itikadi kali za kidini.
Na pia hakuna aliyeamini kuwa yeye ni gaidi.
Jirani yake Ali Hussein Kareithi anasema kuwa jambo hilo ni kawaida katika eneo hili wanaloishi wameona watu wakikamatwa na polisi bila sababu na wengine hata kutoweka.
Ali bado hajarudi shuleni hata baada ya wanafunzi wenzake kumuunga mkono.
Anahofia kuwa huenda akabaguliwa na walimu wake ingawa alikuwa anaheshimika sana shuleni na hata kuteuliwa kama kiranja wa darasa lake.
Na hatembei ovyo kutoka nyumbani kwao kwa hofu ya dhana ya watu waliyonyao kumhusu. Hata hivyo anasisitiza kuwa hana hatia.

SOURCE: BBC SWAHILI