Saturday, 2 November 2013

TFF, Simba zimuadhibu Kibadeni kwa kutukana

2nd November 2013
Katuni
Fujo zilitokana na vurugu za mashabiki wa Simba kwenye Uwanja wa Taifa juzi ndizo zilizotawala mazungumzo ya wapenzi wa michezo kwa sasa nchini.


Katika mchezo baina ya Simba na Kagera Sugar mashabiki wa Simba walirusha vitu uwanjani kwa hasira, ikiwamo viti vilivyong'olewa jukwaani na tayari Bodi ya Ligi imeshasema itatoa adhabu kali ili iwe fundisho.

Ni jambo baya kwa mashabiki kufanya vurugu na ni jambo baya zaidi, pengine, kung'oa viti na kuvitumia kama silaha dhidi ya yeyote ambaye hasira za mashabiki hao zinaelekezwa kwake uwanjani.

Vurugu kwenye viwanja vya soka, kutokana na sababu yoyote ile, haziwezi kuwa na utetezi wenye mashiko na ndiyo maana Bodi mpya imeahidi kutoa adhabu kali ambayo, hatahivyo, hatuna uhakika Nipashe kama ipo kulingana na kanuni za sasa za uendeshaji wa ligi kuu ya Bara.

Adhabu za makosa kama yaliyofanywa na mashabiki wa Simba kwenye ligi kuu ya Bara huwa ni faini ambayo, kimsingi, huelekezwa kwa klabu ambayo kwa ukubwa wa Simba ni chenji ya mapato yatokanayo na mchezo wowote kwenye uwanja huo; siku yoyote.

Lakini wakati wapenzi wa michezo wakiwa wamejikita katika kujadili vurugu hizo za mashabiki, na wakati Bodi ya Ligi ikiwa imelirukia suala hilo na kuahidi adhabu ambayo itakuwa fundisho:

Sisi, Nipashe, tunaona kwamba vurugu za Simba kwenye Uwanja wa Taifa ni cha mtoto.

Vurugu za Simba kwenye Uwanja wa Taifa ni cha mtoto katika vipaumbele vya Bodi hiyo, tunaona Nipashe, kwa sababu kitendo cha mashabiki wa Simba si jambo la ajabu katika mazingira na mchezo huo duniani.

Ambacho ni jambo la ajabu na lenye kuhitaji hatua za haraka za Bodi, Nipashe tunaona, ni kitendo cha kocha wa timu kuwatukana matusi ya nguoni waamuzi waliotoka kuchezesha pambano la timu yake katika mkutano na waandishi wa habari; baada ya mchezo.

Tumeshuhudia katika ligi za wenzetu ambako ni kosa hata kule tu kulaumu makosa ya uamuzi hadharani, makocha wakiadhibiwa binafsi kwa kuponda maamuzi ya uwanjani wakati wakizungumza na waandishi wa habari.

Kama mwalimu, kanuni za ligi za wenzetu zinasema, kocha hutakiwa kujadili masuala ya ufundi ambayo yalijitokeza uwanjani na pale mhusika anapotoka nje ya eneo hilo hukumbana na adhabu hizi za faini na kufungiwa kukaa benchini kulingana na uzito wa shutuma alizotoa.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya sare iliyoambatana na vurugu hizo juzi, kocha mkuu wa Simba Abdallah Kibadeni aliwatukana waamuzi wa pambano hilo matusi ya nguoni na kudai kuwa kwa uchezeshaji wao alitaraji viti ving'olewe na vurugu zitokee kwenye uwanja huo.

Kutukana waamuzi matusi ya nguoni, tunaona Nipashe, ni utovu wa nidhamu wa hali ya juu kuliko hata kitendo cha mashabiki kuvunja viti uwanjani na kuvitumia kama 'makombora' dhidi ya yeyote ambaye hasira za mashabiki hao wa Simba zilielekea kwao.

Wakati Bodi ya ligi ikiwa ndiyo kwanza inaanza majukumu yake baada ya kuchaguliwa Jumamosi iliyopita, ielewe kuwa soka la Bara halijapata kuwa na tukio la kihuni la aina hii ambalo kwa vyovyote linataka kupeleka uhuni kwenye soka katika kiwango kipya na kibaya kuliko chochote ambacho mashabiki wamewahi kukivuka.

Tunasema kocha kutukana matusi ya nguoni kwenye soka ni uhuni katika kiwango kipya na kibaya kuliko chochote ambacho mashabiki wamewahi kukivuka kwa sababu katika vurugu, mara nyingi, matendo huongozwa na saikolojia ya wingi wa watu.

Lakini kama kocha, ambaye kwa vyovyote kitaaluma atakuwa mwenye uwezo mkubwa zaidi wa kuchambua baya na zuri kuliko saikolojia ya kundi, anatukana hadharani hali ikoje kambini kati yake na wachezaji?

Picha ya kambini ni mazingira ambayo yapo ndani ya uwezo na matakwa ya Simba pekee, lakini uongozi wa timu hiyo hauwezi kukwepa kuchukua hatua dhidi ya mwalimu huyu kwa sababu kwanza ameidhalilisha hata klabu; lakini pia ameudhalilisha mchezo huo mbele ya jamii akitumia jukwaa la Msimbazi.
CHANZO: NIPASHE